Spread the love

 

HAKUNA shaka kuwa Rais wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassan, anaweza kulifanyika mabadiliko mengine baraza lake la mawaziri, muda wowote kutoka sasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mabadiliko yaweza kutokea, kufuatia hatua ya Rais kumteuwa mwanasiasa mashuhuri Visiwani Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, kuwa Mbunge wa Bunge la Muungano.

Shamsi amewahi kuwa waziri kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na waziri wa ulinzi na jeshi la Kujenga Taifa (JKT), pamoja na waziri wa mambo ya ndani, katika serikali ya Muungano.

“Ni jambo ambalo halitakuwa na afya, ikiwa Mama Samia (Rais Samia), ataishia kumfanya Nahodha kuwa mbunge. Ni lazima atamuingiza serikalini, ili kuweza kumsaidia kuendesha serikali, kutokana na udhoefu wake mkubwa katika mambo ya Muungano na Zanzibar,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali.

Ameongeza, “pamoja na kwamba Nahodha ni mstaafu, lakini bado ni kinana na ana nguvu za kusaidia katika uendeshaji wa serikali. Sitarajii kama Rais ataishia katika ubunge. Bila shaka atamuingiza kwenye baraza la mawaziri.”

Mbali na Nahodha, Rais Samia alimteuwa Humprey Polepole, mbunge wa kuteuliwa na Rais, kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.

Polepole, ambaye alikuwa kipenzi cha Dk. John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri kati ya Novemba 2015 na Machi mwaka jana, aliwahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, Itikadi na Uenezi.

Shamsi Vuai Nahodha, Mbunge wa kuteuliwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Katika siku za hivi karibuni, Polepole alikuwa maarufu sana, kutokana na mijadala mbalimbali aliyokuwa akiendesha kupitia alichokiita, “Somo la Uongozi.”

Tangu Rais Magufuli kufariki dunia, takribani mwaka mmoja uliyopita, Polepole amekuwa mstari wa mbele kukikosa chama chake, hatua ambayo ilisababisha kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya wabunge wa CCM.

Polepole aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, aliteuliwa na Rais Magufuli kuchukua nafasi ya Katibu Mwenezi wa CCM, akitokea kwenye wadhifa wa mkuu wa wilaya ya Ubungo.

Uteuzi wake uliibua manung’uniko kutoka kwa baadhi ya makada wa chama hicho, kwa maelezo kuwa hakuwa na sifa.

Aidha, manung’uniko kuhusu Polepole yalihusisha na uteuzi wa Dk. Bashiru Ally, kuwa katibu mkuu wa CCM, hoja kuu ikijikita kwenye uanachama wao; jambo ambalo  Magufuli mwenyewe aliwahi kulielezea.

Akijibu malalamiko hayo, Magufuli ambaye alikuwa pia mwenyekiti wa chama hicho, alieleza kuwa amepata taarifa za watu kuhoji uhalali wa kumtea Dk. Bashiru kushika nafasi hiyo kubwa na kuongeza, “nilitaka mchapa kazi na si chama.”

Dk. Bashiru aliteuliwa kushika wadhifa huo, siku chache baada ya kukabidhi ripoti ya uchunguzi wa mali za chama hicho kikongwe, ambapo ripoti iliwataja baadhi ya viongozi wandamizi kuhusika na ubadhirifu wa mali zake.

Humphrey Polepole

Kama hiyo haitoshi, akichangia katika Bunge la 12 mjini Dodoma, mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alitaka kufanyika uchunguzi wa kiasi cha dola za Marekani 9 bilioni (sawa na zaidi ya Sh.20 trilioni), ambazo zilizokopwa wakati wa utawala wa miaka mitano ya Magufuli.

Alisema, “miaka mitano hadi sita iliyopita, zilikopwa dola 9 bilioni, bahati mbaya mikopo hiyo ni ya kibiashara. Hivyo inaiva haraka, hali ambayo inafanya nchi kulipa deni la Sh. 8000 bilioni kwa kila mwezi, jambo ambalo huathiri vibaya shughuli zingine za serikali.

“Kwa hizi za nyuma ambazo zimekopwa na hakuna uwazi mkubwa, twende tukafanye ukaguzi kwenye akaunti ya deni la Taifa. Tunataka kujua kilikopwa nini na kimekwenda wapi. Thamani yake nini na uhalisia wa miradi inayotekelezwa na thamani tuliyoambiwa, iwekwe mezani, kama hizi za Rais Samia, Sh. 1.3 trilioni zilivyowekwa mezani.”

Akijibu hoja hiyo, Polepole alihoji dhamira ya mbunge huyo kutaka uwazi huo, akisema kama wakati zinakopwa ziliwekwa wazi; na kama njia ya kuweka wazi ni moja au nyingi.

“Mimi ni mbunge, taarifa zote za mikopo ya fedha zinakuja bungeni. Je, kwa nini aulize sasa wakati mwulizaji alikuwa kwenye Bunge la 11, ambalo yeye alikuwamo, kwa nini anataka taarifa hizo zije wakati huo?” alihoji.

Alisema fedha hizo za mikopo hata Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa wakati huo, Prof. Mussa Assad hakuzihoji na alipohoji kuhusu Sh. 1.5 trilioni, majibu yake yalitolewa haraka na likaisha.

Popole ambaye alikuwa ameanzisha kampeni ya kuondoa wale aliowaita, “wahuni kwenye chama na serikali.” Alisema, Rais Magufuli hakumaliza kuondoa wahuni ndani ya Serikali na CCM.

Nehemiah Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)

Alisema: “Mimi nilitamani sana kwenye uongozi wa miaka mitano ya Rais Magufuli, tuwe tumeshughulika na wahuni wengi na kuwamaliza. Ukiuliza udhaifu, nitakwambia hatukuwamaliza wahuni, ilikuwa ndoto yangu tungeshughulika na wahuni ulalo ulalo na kuwamaliza.”

Polepole hakuwahi kutaja aliowaita wahuni, badala yake alisema, “hao wanaonishambulia ndio wahuni wenyewe.”

Aliongeza: “Kwa wana CCM wasio na ‘baba walezi’ kataeni matabaka kwenye chama chetu, maana ndio msingi wa usawa wa binadamu ambayo ni imani ya kwanza ya chama chetu na wanachama.

“Matabaka ni mbinu moja ya wahuni kudhoofisha chama chetu kwa maslahi yao, tukatae tabia hiyo,” aliandika Polepole.

Alisema anashangaa kuwapo Serikali ya Awamu ya Sita, jambo ambalo yeye haamini na kusema, “hii ni Serikali ya Awamu ya Tano yenye Rais wa sita.”

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, hatua ya Rais Samia kumuondoa Polepole bungeni, kunaashiria kuwa safari ya mwanasiasa huyo sasa inaelekea ukingoni.

“Tunataka kuona hilo somo la uongozi sasa linatokea Malawi. Hii ni ishara nyingine kuwa safari ya Polepole, inaelekea ukingoni,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya CCM.

Mbali na Nahodha na Polepole, Rais Samia alimrejesha kwenye wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, huku aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la mawasiliano (TTCL), Waziri Kidamba, kuwa mkuu wa mkoa wa Njombe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *