Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif aliacha siri nzito
Habari za SiasaTangulizi

Maalim Seif aliacha siri nzito

Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo
Spread the love

 

MANSOUR Yusuf Himid (53), mmoja wa wanasiasa machachari visiwani Zanzibar, ndiye aliyekuwa chaguo la kwanza la Maalim Seif Sharif Hamad, kutaka kurithi mikoba yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online anasema, Mansour ndiye alikuwa chaguo la kwanza la Maalim Seif wa kumkabidhi mikoba yake, mara atakapostaafu.

Maalim Seif ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, alipanga kustaafu wadhifa wake wa Makamu wa Kwanza wa Rais, miezi 18 ijayo. Alifariki dunia tarehe 17 Februari 2021, jijini Dar es Salaam na kuzikwa kijiji kwake, Mtambwe, kisiwani Pemba.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, Maalim Seif, alitaka kumkabidhi Mansour mikoba yake yote, “kama angekuwa bado yuko hai na mwenye nguvu.”

Mansour ni mtoto wa Brigedia Jenerali, Yusuf Himid, ambaye alikuwa mkuu wa kwanza wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), mara baada ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964.

Amepata kuwa waziri katika serikali ya Dk. Amani Abeid Karume na Alli Mohammed Shen, akianzia wizara asiyekuwa na wizara maalum na kisha kufanywa kuwa waziri wa ujenzi, nishati na ardhi.

Aliondolewa kwenye baraza la mawaziri, mwaka 2012 na Agosti mwaka huo huo, akafukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kutofautiana juu ya muundo wa Muungano.

Mbali na kushika nafasi za uwaziri, Mansour amepata kuwa Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM Zanzibar na mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki, Unguja.

Aidha, Mansour amekuwa mjumbe wa Kamati ya Maridhiano, iliyokuwa ikiongozwa na mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassoro Moyo.

Kabla ya wimbi maarufu la “ulipo tupo,” kumburuza na kumfikisha ACT – Wazalendo, Mansour alikuwa mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF).

Amewahi kuwa mshauri mwandani wa Maalim Seif, kabla ya kiongozi huyo, kukutwa na mauti.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo ambaye ni kiongozi wa juu wa chama hicho, Maalim Seif alieleza bayana kuwa Mansour ndiye anayestahili kushika mikoba yake.

“Lakini Maalim Seif (77), alionya kuwa ikiwa angefariki mapema, basi mtu sahihi kabisa wa kutuvusha hapa tulipo, ni Othman Masoud Othman Sharif,” ameeleza.

Othman aliapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Jumanne iliyopita ya tarehe 3 Machi 2021 na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Akimnukuu Maalim Seif, kiongozi huyo alisema, “alituambia, ‘nikifariki mapema, mchukueni Othman. Yeye ataweza kuwaunganisha na kuendelea kubaki wamoja katika kipindi ambacho mimi sitakuwapo ulimwenguni; na au kutokuwa nguvu ya kusimamia maamuzi tofauti na hayo.’”

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa walipewa maelekezo hayo na mwanasiasa huyo nguli Zanzibar, ni pamoja na kiongozi mmoja mstaafu wa kisiasa Visiwani ambaye aliwahi kuwa karibu na Maalim Seif, wakati wakiwa CUF.

Mwingine aliyebahatika kupewa wosia huo na Maalim Seif, ni mmoja wa wanasiasa vijana Zanzibar, ambaye alipata kuwa karibu mno na kiongozi huyo tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuapishwa Othman alisema, Wazanzibari walibeba matumaini makubwa kwa Maalim Seif na hivyo naye ana kila sababu ya kuendeleza pale alipoishia kwa kuwaunganisha kuwa kitu kimoja na kuondosha ubaguzi wa hali zote.

Alisema, “sote ni mashahidi kuwepo kwa maridhiano kumechangia kusaidia kuleta utulivu ndani ya nchi na hivyo kuna kila sababu ya kuendelezwa maridhiano hayo ya umoja uliopo ambao wote wawili Maalim Seif na Rais Mwinyi, wameonesha dhamira njema. Tunapaswa kuendeleza yale ambayo ametuachia.

Othman Masoud Othman

“Hakuna nchi hata moja duniani yenye mfano kama wa kwetu ambayo imeendelea bila ya kuanza na umoja, Singapore iliendelea baada ya kujenga umoja na ndio wakafikia hapo walipofikia.

“Mimi ni muumini wa umoja na sikuanza leo tokea nipo serikalini hata ilipotengenezwa Vision 2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA), katika mchango wangu hata ukiwauliza wahusika watakwambia, mimi ndio niliotoa mawazo hayo nilisema tunatengenezaje vision 2020 bila ya kuingiza suala la utaifa? Nilisema hayo kwa sababu naelewa umuhimu wake na msingi wake.”

Akihutubia wafuasi wa chama chake, Vuga, mjini Uguja, Makamo huyo wa Kwanza wa Rais, aliwashukuru wote waliofanikisha kumteuwa kushika nafasi hiyo, lakini akawasihi wafusi wao, kujitahidi kuendelea kuwa wamoja kama alivyowaachia Maalim Seif.

Akaongeza, “Maalim Seif hakuacha zambarau nyingi. Maalim Seif hakutuachia Zambarau Kaskazini na Kusini wala hajatukuachia Zambarau Nyeupe na Nyeusi Alituacha tukiwa wamoja na madhubuti.

“Maalim hajatuachia Unguja na Pemba. Ametuacha tukiwa wamoja. Tafadharini tuendeleze umoja huo.”

Alisema, “…niishukuru kamati ya uongozi kwa kauli moja kukubali kumpata mridhi mmoja wa kuendeleza mapambano haya ya kiongozi wetu aliyekuwa akituongoza, ni heshima kubwa kwa Maalim kwa kiongozi ambaye alikuwa akituongoza” alisema.

Katika baadhi ya habari tulizoandika, tuliandikwa kuwa Othman ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, kufuatia kubahatika kupenyezewa taarifa na mmoja wa viongozi wajuu wa chama hicho, kuwa ndio maelekezo ya Maalim Seif.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, uteuzi wa Othaman Masoud, kushika nafasi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Visiwani, utaweza kuisaidia Zanzibar, hasa katika masuala nyeti yanahusu haki za visiwani hivyo kwenye Muungano.

Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais ya Mapinduzi Zanzibar, akiapa mbele ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi Ikulu Zanzibar

Msimamo wa Othman unafahamika katika masuala ya Muungano na kwamba wakati wa Bunge Maalum la Katiba, alipigia kura ya HAPANA, Ibara ya 73 ya Katiba Pendekezwa, inayoeleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakuwa na muundo wa serikali mbili.

Aidha, gwiji hilo la sharia, lilipinga Ibara 74 inayoeleza kuwa “shughuli zote za mamlaka ya nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji na vyenye mamlaka ya kutunga na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.”

Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vilivyotajwa na Katiba Pendekezwa, ni ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; vyombo vyenye mamlaka ya utoaji haki vitakuwa ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Kuu ya Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Nayo Ibara 75 ya Katiba ya Pendekezwa, ambayo inaeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya utekelezaji katika Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano na kwa mambo yote yasiyo ya Muungano yanayohusu Tanzania Bara, ilipigiwa kura na Othman, ambaye wakati huo, alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar (AG).

Akizungumza katika hafla ya kumpokea Makamu huyo wa Kwanza wa Rais, Vuga, Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo, Zitto Zubeir Kabwe, aliishukuru kamati ya uongozi kwa kumpitisha Othman kwa sauti moja, lakini akasisitiza kuendelezwa maoni ya Maalim Seif ya kuleta umoja na mshikamano ndani ya chama kwani umoja na maridhiano ndio ulikuwa msingi mkuu wa kiongozi huyo.

Zitto alisema, “nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ni ya ushauri kwa kazi za serikali ya Zanzibar, hivyo Othman amesema anaweza kufanya kazi na kila mtu kwa kuwa historia yake inaonesha hivyo ameanza kufanya kazi na marais wengi akianzia na Dk. Salmin Amour, Amani Karume na Dk Ali Mohammed Shein. Na sasa tunaamini atafanya kazi hiyo na Rais Mwinyi.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

M/kiti bodi ya wadhamini Chadema afariki dunia

Spread the loveMWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Zitto: Nikifa Ado atavaa viatu vyangu

Spread the love  KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe...

error: Content is protected !!