Friday , 3 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Kisa kusalimia wanaume, Mwanakwaya daiwa kuua mkewe, anaswa
Habari Mchanganyiko

Kisa kusalimia wanaume, Mwanakwaya daiwa kuua mkewe, anaswa

DC Kyela - Josphine Manase
Spread the love

MWIMBAJI maarufu wa kwaya kwenye kanisa moja la kiroho kijiji cha Ikulu kata ya Ipinda wilayani Kyela mkoani Mbeya, Aliko Mwakalibule (38) aliyekuwa anasakwa kwa tuhuma za kumuua mkewe Metrida Kyoma (22) kwa kumkatakata na panga kwa wivu wa mapenzi, amenaswa akiwa bwawa la Mtera mkoani Iringa. Anaripoti Ibrahim Yassin, Mbeya … (endelea).

Akizungumza tukio hilo Mwenyekiti wa kijiji cha Ikulu, Brasto Mwandunga amesema mtuhumiwa huyo alidaiwa kumuua mkewe tarehe 1 Januari 2024 baada ya kutoka naye kwenda kunywa pombe kijiji jirani cha Kafundo wakiwa na mtoto wa miaka minne.

Amesema ilipofika saa nne usiku walianza kurejea nyumbani wakipita njia ya mkato kwenye vichaka ambavyo alikuwa amepanga kufanya mauaji kwani alipofika katika moja ya vichaka hivyo alichomoa panga alilokuwa amelificha kwenye kichaka kimojawapo na kumkatakata sehemu mbalimbali.

“Kijana huyo ni mtanashati muumini wa kanisa la kiroho na muimba kwaya maarufu, ameshangaza watu juu ya mauaji hayo.

“Nakumbuka kabla ya kutekeleza mauaji aliuza kiwanja akanunua panga akalificha kichakani, fedha zingine alizitenga kwa ajili ya safari ya kutoroka,’’ amesema Mwandunga.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Ikulu, Jackson Mwang’onda amesema baada ya kupigiwa simu na mwenyekiti alifika eneo hilo na kupiga simu polisi ambao walifika na kumchukua mwanamke huyu akiwa hajiwezi na alifariki wakiwa njiani kuelekea hospitali.

Amesema mtuhumiwa Aliko Mwakalebule alikuwa na wivu wa kupindukia kwani alikuwa anagombana na mkewe kila anasalimiana na mwanaume mwingine.

Ameongeza kuwa mwanamke huyo aliyeuawa, ni wa tano kuishi naye kwani wapo wanawake wanne waliishi na mwanakwaya huyo kwa nyakati tofauti na kuachana naye kutokana na matendo yake.

Afisa mtendaji wa kata ya Ipinda, Ally Joel amesema baada ya tukio walianzisha msako kwa kuweka mitego sehemu mbalimbali hadi ilipofika jana Jumatano walipopatiwa taarifa kuwa yupo Migoli kwenye bwawa la Mtera linalotumika kwa uvuvi wa samaki mkoani Iringa.

Amesema baada ya kupata taarifa hizo kwa kushirikiana na uongozi wa Migoli likiwemo Jeshi la polisi walifanikiwa kumnasa na kumuweka rumande na taratibu za kumsafirisha kuja Kyela zinaendelea.

Joel amesema hilo ni tukio la pili mfululizo kutokea katika Kijiji cha Ikulu kwani katika siku za hivi karibuni Erasto Kikali (43) alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe kwa kipigo.

Kikali anadaiwa kuwa alitumia njia ya kumpaka sumu ya kuulia magugu mdomoni  na  kuweka chupa hiyo pembezoni mwa mwili ili ijulikane alijiua.

Anasema uchunguzi wa madaktari ulibaini marehemu hakunywa sumu bali aliuawa kwa kipigo baada ya kuona alama za vimbo mgongoni.

Mkuu wa wilaya ya Kyela, Josphine Manase licha ya kusikitishwa na matukio hayo ya mauaji ya kikatili amesema wataendelea kutoa elimu mara kwa mara katika ngazi zote ili kumaliza vitendo hivi.

Amesema katika wilaya hiyo wanaume wengi huwajeruhi wake zao kwa wivu wa mapenzi na kukimbilia nchini Malawi.

Kamanda wa polisi mkoani Iringa, Alan Bukumbi akizungumza kwa njia ya simu amesema bado hajapewa taarifa na mkuu wa polisi wilaya kuhusu kukamatwa kwa mtuhumiwa Mwakalibule.

Amesema atalizungumzia kwa kina sakata hilo pindi atakapopewa taarifa ili taratibu za kumsafirisha mtuhumiwa kwenda Kyela zifanyike.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

Habari MchanganyikoKimataifa

Ruto amteua Kahariri kuwa mkuu wa majeshi

Spread the loveRAIS wa Kenya, William Ruto, amemteua Jenerali Charles Muriu Kahariri,...

Habari Mchanganyiko

Chongolo aonya viongozi vijiji kutouza NIDA kwa wageni

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amewaonya viongozi wa...

error: Content is protected !!