Monday , 4 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kikwete akwepa kuzungumzia alivyomuengua Lowassa 2015
Habari za SiasaTangulizi

Kikwete akwepa kuzungumzia alivyomuengua Lowassa 2015

Spread the love

RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa Hayati Edward Lowassa kiasi cha kupewa jina la ‘Boys II Men,’ amekwepa kuzungumzia namna alivyomuengua Lowassa katika kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa ya CCM kuteuliwa kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Licha ya kuzungumzia historia ya ukaribu wake na Lowassa tangu walipokuwa Chuo Kikuu Dar es Salaam, kuwania urais mwaka 1995 hadi alipojizulu uwaziri mkuu mwaka 2008, Kikwete amesema mengine yaliyotokea ni changamoto katika maisha.

Kikwete ambaye alikuwa amembatana na mkewe Mama Salma ametoa kauli hiyo leo Jumatatu baada ya kufika nyumbani kwa marehemu Lowassa, Masaki jijini Dar es Salaam kuhani msiba wa waziri mkuu huyo mstaafu.

Amesema mwanasiasa huyo enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa kwa Taifa na changamoto zilizowahi jitokeza dhidi yake hazifuti yale mema na mazuri aliyoifanyia nchi.

“Ninachoshauri tu tuendelee kumuombea kwa Mungu aipokee roho yake aiweke mahala pema peponi. Edward ametoa mchango mkubwa kwa Taifa letu, yaliyotokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti yale mema na mazuri aliyolifanyia Taifa letu,” amesema Dk. Kikwete.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini, amesema kifo cha Lowassa amekipokea kwa mshtuko mkubwa “nimepokea kwa mshtuko taarifa ya kifo, nilikuwa nafahamu kwamba alikuwa anaumwa lakini sikutegemea kwamba ingefikia hapa ilipofikia (kifo).”

Akizungumzia namna alivyomfahamu, Dk. Kikwete amesema alianza kumfahamu wakiwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo yeye alimtangulia kwa mwaka mmoja, kisha akafanya naye kazi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya yeye kwenda jeshini na hata aliporejea ndani ya chama hicho.

“Tumefanya kazi wote kwenye chama kwa muda wote na baadae mimi nikaendelea na shughuli za jeshi, nikarudi tena kwenye chama mwenzangu aliendelea moja kwa moja kwenye shughuli za chama na baadae yeye akawa mbunge na mie nikateuliwa kuwa mbunge na naibu waziri tukawa wote kwenye Baraza la Mawaziri na tulikuwa wote kwenye harakati za kisiasa,” amesema Dk. Kikwete.

Amesema 1995, Lowassa, Rostam Azizi na Hayati Samuel Sitta walimfuata nyumbani kwake kumshawishi yeye na Lowassa kwenda kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Amesema baada ya mabishano ya muda mrefu, walienda kuchukua fomu lakini mwenzake (Lowassa) hakufanikiwa kuingia tano bora wakati yeye akifanikiwa kushika nafasi ya pili huku Hayati Benjamini Mkapa akifanikiwa kuipeperusha bendera ya chama hicho.

“Kura zangu hazikutosha akapata Mzee Mkapa mimi nikaja kuwa waziri wake wa mambo ya nje na mwenzangu baadae akaja kuwa waziri, basi tumeendelea hivyo kuweka mikakati ya pamoja ya 2005, mwenzangu akaja kuwa waziri mkuu akateuliwa kuwa waziri mkuu tukapata changamoto katikati mwenzangu ikabidi akae penmbeni lakini tumeendelea kuwa pamoja, kuwa marafiki, kushirikiana kwa kila linalowezekana,” amesema Dk. Kikwete.

Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia mwaka 2005- hadi 2008, alifariki dunia Jumamosi iliyopita na mwili wake unatarajiwa kuzikwa tarehe 17 Februari mwaka huu nyumbani kwake Monduli, jijini Arusha.

Mwanasiasa huyo amefariki dunia huku akishindwa kutimiza ndoto yake ya kuwa Rais wa Tanzania, baada ya kuenguliwa na CCM iliyokuwa inaongozwa na Kikwete mwaka 2015 katika kinyng’anyiro cha kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Badala yake, aliyepitishwa ni Dk. John Magufuli huku Lowassa akihamia Chadema ambako nako alibahatika kushika nafasi ya pili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwinyi aungana na Samia kuuaga mwili wa baba yake

Spread the loveRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk....

Habari za SiasaTangulizi

Mtoto wa Mzee Mwinyi amwaga machozi

Spread the loveMtoto wa Hayati mzee Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi ameshindwa...

Habari za SiasaTangulizi

Mzee mwinyi alikuwa mwanademokrasia wa kweli

Spread the loveMtoto wa Hayati Ali Hassan Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Mwinyi alikuwa maktaba inayotembea

Spread the loveRais Samia Suluhu hassan amesema Hayati rais mstaafu, Ali Hassan...

error: Content is protected !!