Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli: Sijaingilia uhuru wa Mahakama
Habari za Siasa

Rais Magufuli: Sijaingilia uhuru wa Mahakama

Dk. John Magufuli, Rais wa Tanzania
Spread the love

RAIS John Pombe Magufuli, amedai kuwa hajawahi kuingilia utendaji wa kazi za muhimili wa Mahakama. Amesema, “katika uongozi wangu, sijaingilia muhimili wa Bunge wala Mahakama.” Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Akizungumza leo tarehe 6 Februari 2018, kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, Rais Magufuli alisema, “katika uongozi wangu, mimi nimejitahidi sana kutoingilia muhimili wowote. Sijaingilia muhimili wa Bunge. Sijaingilia muhimili wa mahakama. 

Alisema, “…hata mtu mtu akikutukana, ninazima Tv (televisheni).” Ameitaka pia mahakama kutokubali kuingiliwa na mammlaka yoyote.

Haya yanaibuka takribani mwaka mmoja tangu Rais Magufuli amtake Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwashughulikia aliowaita, “wabunge wakorofi.” Aliahidi kuwa yeye (Ndugai), akimaliza kuwashughulikia wabunge wakorofi ndani ya Bunge, yeye (Rais) atawashughulikia nje ya Bunge.

Aidha, haya yanaibuka miezi michache tangu Rais Magufuli amuagize waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa, “kuwafunda” viongozi wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ili kuheshimu sheria. Vinginevyo Rais Magufuli alisema, “viongozi hao wataishia gerezani.”

Sherehe za “Siku ya Sheria,” zilifanyika katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Aliongeza, “ninajua fika kuwa wapo wanaoingilia mhimili huu kwa hasira tu; lakini nyie msiruhusu kuingiliwa. Ni muhimu kwa kila mhimili ujisimamie wenyewe kwa mujibu kwa Katiba.”

Akiongea huku akimtolea macho Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, Rais Magufuli alisema, serikali itaendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na mahakama na kwa sasa inaendelea kushughulikia matatizo yaliyopo.

Aliitaka Idara ya Mahakama kutokatishwa tamaa kwa “changamoto zinazowakabili.” Alisema, “hakuna kazi isiyo na changamoto. Hata tukimaliza za sasa, zitajitokeza zingine.”

Rais amesema, amekerwa na tabia ya baadhi ya wapelelezi anadai kuwa wanapeleleza kesi zilizo na vidhibiti vilivyo wazi.

Alisema, “mtu unakuta ameshikwa na meno ya tembo, au dawa za kulevya.  Halafu eti upelelezi unaambiwa unaendelea. Unaambiwa lazima tupeleke jambo hili kwa Mkemia Mkuu  wa Serikali na yanapoendelea kukaa huko wanasema ni majivu.”

Kiongozi huyo wa nchi amewataka majaji na mawakili, kutimiza wajibu wao kwa kuwa wanaposimamia haki, kazi yao inapata baraka kutoka kwa Mungu.

Alihoji: “Wapelelezi kapelelezeni haraka. Unapokiona kitu, unakwenda kupeleleza nini? Mtu ameiba na kitu anacho bado unakwenda kupeleleza? Unakwenda kupeleleza ili kujua wakati anaiba alikuwa ameinama ama amelala?”

Amesema, wanasheria wana pande mbili, upande wa mshitaki na mshitakiwa; wakati mwingine wanasheria huzungumza namna ya kuruka vipengele ili mshtakiwa aachwe huru.

Alidai kuwa wanasheria wanapowatetea wateja wao kwa mambo ambayo yako wazi, hawazikosei roho zao tu, bali wanamkosea hadi Mungu. Alisema, “kesi zingine zina ushahidi wa kutosha lakini zinafutwa.”

Amemsifu Prof. Juma, kwa kueleza ukweli kuhusu matatizo yaliyopo katika Idara ya Mahakama. Ameahidi kuyafanyia kazi matatizo hayo kadri atavyoweza.

Alisema, “ndio maana nikakwambia baada ya kumaliza hotuba yako, unikabidhi ili niendelee kupitia na nitayoweza kutatua haraka nitatue na mingine yanaweza kusubiri mpaka pale hali itakaporuhusu.”

Rais Magufuli amesema, ni muhimu kujenga jamii yanye kuheshimu haki, kudumisha amani na kuondoa migogoro kwenye jamii.

“Tupo hapa leo na tumekaa kwa Amani, kwa kuwa zipo sheria zinatulinda. Zisingekuwepo pengine tusingekuwa hivi,” ameeleza.

Naye Jaji Mkuu Ibrahim akizungumza kwenye sherehe hizo aliwashauri wananchi wasome sheria ili kuweza kuzijua sheria na kuwaomba wadau wengine wa Mahakama wasaidie wananchi kutafsiri sheria.

Amesema, “nawasihi wananchi wasome sheria walau kwa uchache, Idara ziwasaidie wananchi kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili.” Prof. Ibrahim ametaka wananchi kutojichukulia sheria mkononi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kasekenya aipa Tanroads wiki kukarabati barabara Morogoro

Spread the loveNaibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wiki moja...

Habari za SiasaTangulizi

‘Aliyemtonya’ Lissu kuhusu rushwa arejea madarakani

Spread the loveMwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Tutaendelea kupigania malengo ya afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Tanzania...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NHC yadai bil. 2.1 taasisi za Serikali, Waziri atoa maagizo

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii...

error: Content is protected !!