May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jina la mrithi wa Maalim Seif, lafikishwa kwa Rais Mwinyi

Spread the love

 

KIONGOZI Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe amesema, chama chake, tayari kimekabidhi kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, jina la mtu ambaye atakuwa Makamo wa Kwanza wa Rais Visiwani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Zitto alisema, “tayari tumeshapendekeza jina kwa Rais wa Zanzibar la mtu ambaye atarithi majukumu ambayo Maalim Seif alikuwa anayafanya.

Aliongeza: “Bahati nzuri, Maalim Seif alikuwa ni Kiongozi. Alijua kuna siku Mwenyezi Mungu atamchukua, kwa sababu sisi sote lazima turejee kwa Mwenyezi Mungu kama tulivyoambiwa na mafunzo ya dini yetu na dini zote.

“Kwa hiyo, aliacha ametupa maelekezo ya nini kitokee iwapo atatangulia mbele ya haki.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba viongozi wa chama wamefuata yale maelekezo yake kwa namna ambayo Kiongozi wetu alituelekeza. Sasa umebaki wajibu wa Rais wa Zanzibar wa kuyatekeleza hayo.”

Mchakato   wa   kumtafuta   mrithi   wa Maalim   Seif   Sharif   Hamad,   aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais Visiwani, ulianza Alhamisi iliyopita na kumalizika juzi Ijumaa, mjini Unguja.

Taarifa   kutoka   ndani   ya   chama   hicho zinasema, Kamati ya Uongozi  ACT-Wazalendo, imepitisha jina la mmoja wa viongozi watatu mashuhuri Visiwani, kumrithi kiongozi huyo.

Gazeti hili limefanikiwa kupata jina la kiongozi huyo, lakini kutokana na unyeti wa suala hilo, limeamua kulihifadhi kwa sasa.

Maalim   Seif   (77),   alifariki   dunia katika   hospitali  ya   taifa   ya   Muhimbili, tarehe   tarehe   17  Februari   na  akazikwa siku iliyofuata, kijijini kwake, Mtabwe, Pemba.

Mwamba   huyo wa siasa nchini    alifikwa   na   mauti baada ya kuwa hospitali kwa  takribani wiki tatu, kufuatia kupata maambuziki ya virusi vya Corona.

Kwa mujibu wa Zitto, ambaye alikuwa akizungumza kwenye ibada ya hitima ya kumuombea kiongozi huyo, wanaamini kuwa huyo ambaye wamempendekeza kurithi nafasi ya Maalim Seif, “ataweza kusimamia maridhiano na haki za Wazanzibari kama ambavyo Maalim Seif mwenyewe alikuwa akifanya.”

Alisema, “tunawaomba muendelee kutuombea duwa ili tusitoke kwenye mstari, tuendelee kupigania demokrasia, haki na kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa ya amani ili iweze kupata maendeleo ya watu.”

error: Content is protected !!