May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mrithi wa Maalim Seif, siri nzito

Spread the love

 

MCHAKATO wa kumtafuta mrithi wa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais Visiwani, umemalizika. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya chama cha ACT- Wazalendo, ofisi kuu Visiwani Zanzibar zinasema, kikao cha Kamati ya Uongozi cha kumpata mtu atakayerithi nafasi ya Maalim Seif, kimemalizika alfajiri ya kuamkia leo, Jumamosi, tarehe 27 Februari 2018.

Maalim Seif (77), alifariki dunia katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, tarehe tarehe 17 Februari na kuzikwa kijijini kwake, Mtabwe, kisiwani Pemba, tarehe 18 Februari mwaka huu.

Mwanasiasa huyo mkongwe Visiwani, alifikwa na mauti takribabi wiki tatu baada ya kuripotiwa kwa taarifa kuwa amepata maambukizi ya virusi vya Corona.

Alishika wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa siku 71, tangu alipoapishwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, tarehe 8 Desemba   mwaka   huu.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya chama hicho, kikao kilijadili majina ya vigogo watatu wandamizi na baadaye wakakubaliana kwa kauli moja, kupitisha jina mmoja wao, kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais Visiwani.

Vigogo ambao majina yao yajadiliwa na kupitishwa moja kwa ajili ya kulipeleka kwa rais wa Zanzibar, ni Juma Duni Haji, makamu mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Zanzibar); mwanasheria maarufu Visiwani, Othman Masoud na mwanasiasa mashuhuri, Masour Yusuf Himid.

Kikao   kilichopitisha jina la Makamo wa Kwanza wa Rais Visiwani,   kiliongozwa   na   Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Dorothy Semu, ambaye pia ni Makamu   Mwenyekiti   wake, Tanzania Bara.

Taarifa zinasema, jina la Duni lilitawala mjadala, kufuatia rekodi yake ya kutumia karibu robo ya maisha yake ya miaka 71 kushiriki moja kwa moja, harakati za kupigania demokrasia nchini.

Aidha, Duni ni mmoja wa viongozi waliotajwa sana kwa kupigiwa chapuo na baadhi ya wajumbe kuwa “ni mwandani wa Maalim Seif,” na kwamba kila nafasi ambayo kiongozi huyo alikuwa akiishikiria, Duni ndiye alikuwa msaidizi wake.

Hayati Maalim Seif Sharif Hamad

Duni amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), wakati Maalim Seif akiwa katibu mkuu; ameshakuwa makamu mwenyekiti mwenyekiti wa CUF na sasa ni makamu mwenyekiti wa ACT- Wazalendo.

Naye Othman Masoud, ambaye alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali ya Zanzibar (AG); naibu mwanasheria mkuu na Mwendesha Mashitaka (DPP), jina lake lilijadiliwa na kumwagiwa sifa kedekede, kwamba anaweza kuwa mrithi sahihi wa Maalim Seif.

Othman alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali ya Zanzibar kati ya Novemba 2010 hadi Oktoba mwaka 2014. Uteuzi wake utenguliwa, kufuatia uamuzi wake wa kupigia kura ya HAPANA, baadhi ya vifungu vya Katiba Pendekezwa.

Juma Duni Haji

Kutokana na msimamo huo, Othman alitimliwa ndani ya Bunge Maalum la Katiba, jijini Dodoma na kurejeshwa Zanzibar, ambako nako, alikutana na rungu la Dk. Shein la kumvua wadhifa wake.

Mwingine aliyejadiliwa, ni Mansour Yusuf Himid, ambaye amepata kushika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, wakati wa utawala wa Amani Karume.

Aliwahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM na Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho Zanzibar, pamoja na Katibu wa Fedha na Uchumi Visiwani.

Jina la Mansour lilijadiliwa kwa uzito mkubwa, kutokana na kuwamo kwake, kwenye Kamati ya Mwafaka iliyoongozwa na mwanasiasa mkongwe, Hassani Nassoro Moyo.

Katiba ya Zanzibar inakielekeza chama cha siasa chenye sifa ya kushika nafasi ya Makamo wa Kwanza wa Rais,   kupeleka   kwa   Rais   wa Zanzibar,   jina   la   mtu   atakayeteuliwa kushika nafasi ya Makamo wa Kwanza wa Rais.

Othuman Masoud

Kabla ya kuanza kikao hicho cha ndani, Mwanasheria mkuu wa ACT- Wazalendo, Omar Said Shaaban, alitaja sifa ambazo zinahitajika kwa mtu ambaye atateuliwa kushika nafasi hiyo.

Miongoni mwa sifa hizo, ni pamoja na kuwa na msimamo wa maridhiano wa kuiunganisha Zanzibar.

Alisema, “huo ndio ndio msimamo wa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad. Hivyo basi, hilo tutalizingatia kwa nguvu kubwa.”

Alitaja sifa nyingine, kuwa ni mtu anayependa haki, na kwamba “kamati ya uongozi, itateua mtu kutokana na vigezo hivyo.

“Kwanza awe mtu mwenye msimamo, na sio mwenye msimamo tu, bali mtu mwenye kupenda maridhiano sababu ni moja ya sifa kubwa aliyotuachia Maalim Seif. Tutachagua pia mtu mwenye kupenda haki, lakini mwenye maono pia,” alieleza Shaaban.

Mansour Yusuf Himid

Alisema, “tumemaliza siku saba za maombolezo, si rahisi kumsahau mwenyekiti wetu namna alivyojitoa katika demokrasia ya nchi hii.

“Lakini kwetu sisi kama viongozi wa chama, tunapaswa kusonga mbele kwa kupeleka jina la mrithi wake.”

Alisema, hakushangazwa na minong’ono iliyokuwa ikiendelea, kuhusiana na nani hasa atapitishwa kushika nafasi hiyo, lakini akaongeza, “Kamati ya Uongozi itapendekeza mtu sahihi wa kumrithi Maalim Seif.”

Shaaban amesema, kamati hiyo kabla ya itateua jina la mtu inayompendekeza kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, itajadili vigezo gani ambavyo mtu huyo anapaswa kuwa navyo.

MwanaHALISI limebahatika kudokezwa jina la alipendekezwa kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais Visiwani, lakini kutokana na unyeti wa jambo lenyewe, limeamua kuhifadhi jina hilo kwa sasa – Mhariri.

error: Content is protected !!