April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Habari za hivi punde: Iran yakiri kuangusha ndege ya Ukraine

Spread the love

HATIMAYE Serikali mjini Tehran, imekiri madai kuwa imeidungua ndege ya abiria Ukraine, runinga ya taifa ya Iran imeripoti.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jeshi nchini humo limekiri kuwa ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 iliyotengenezwa nchini Marekani – nchi ambayo ni hasimu wa Iran –ilidunguliwa “kimakosa,” baada ya kupita karibu na “eneo nyeti” linalomilikiwa na Kikosi cha Mapinduzi (Revolutionary Guards).

Ndege hiyo ya kimataifa ya Ukraine yenye namba za usajili PS752 iliyokuwa inaelekea Kyiv ilianguka siku ya Jumatano, wakati ilipokuwa ikiruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Imam Khomeini, na kuuwa watu wote 176 waliokuwamo.

Serikali ya Iran inasema, mkasa huo umetokana na “makosa ya kibinadamu,” na kwamba maafisa waliofanya kosa hilo wataadhibiwa.

Kukiri kwa jeshi la Iran kutungua ndege hiyo, kumekuja takribani siku tatu baada ya serikali ya Tehran, kukana kwa nguvu madai kuwa makombora yake yaliidungua ndege ya abiria ya Ukraine, Jumatano iliyopita.

Hata hivyo, nchi hiyo ilikabwa koo baada ya Marekani na Canada kudai kuwa taarifa za kijasusi walizonazo zinaonesha kuwa Iran iliidondosha ndege hiyo kwa bahati mbaya na moja ya makombora yake.

Kuanguka kwa ndege hiyo kulitokea saa chache baada ya Iran kushambulia kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq kwa makombora ya masafa marefu.

Vyombo vya habari vya Marekani vinadai kuwa Iran ilidhani kuwa ndege hiyo ilikuwa ya kivita ya Marekani, wakati taifa hilo lilipokuwa ikijiandaa kujibu mashambulio dhidi ya Marekani baada ya wao kushambulia vituo vyake vya kijeshi nchini Iraq kwa makombora.

Iran ilirusha makombora kwenye kambi za Marekani Jumatano iliyopita, kama sehemu ya kisasi chake baada ya Rais Donald Trump kuagiza shambulio la anga lililomuua Jenerali wa Iran, Qasem Soleimani.

Jenerali Qasem aliuwa tarehe 3 Januari mwaka huu, mjini Baghadad, nchini Iraq.

Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Alhamisi alisema: “nina mashaka” juu ya (kuanguka) kwa ndege. “Inawezekana kuna mtu amefanya kosa kubwa.”

Kanda ya video iliyopatikana na gazeti maarufu la Marekani la New York Times, ilionenesha jinsi makombora yalivyokuwa yakipita katika anga la Tehran na baadae kulipuka ilipokutana na ndege.

Karibu sekunde 10 baadae mlipuko mkubwa ulisikika ardhini. Ndege iliyokuwa imeanza kushika moto, ikiendelea kupaa.

Kituo cha habari cha CBS imevinukuu vyanzo vya kijasusi vya Marekani vinavyodai kuwa picha za satelaiti zinaonesha mwanga wa makombora mawili ambao ulifuatiwa na mwanga wa mlipuko.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na shirika la habari la

CBS, mitambo ya rada ya Marekani ilibaini makombora mawili yakirushwa muda mfupi kabla ya ndege hiyo kulipuka. Inaaminika kuwa ndege ilidunguliwa na makombora ya Kirusi aina ya Tor M-1 ambayo Nato huyaita Gauntlet.

Maafisa wawili kutoka makao makuu ya jeshi la Marekani wameithibitishia kuwa shambulio hilo lilikuwa la bahati mbaya.

Iran inafahamika kuwa na mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora iliyotengenezwa Urusi.

Mkuu wa mamlaka ya anga wa Iran, Ali Abedzadeh amesema, ana ”uhakika” kuwa ndege hiyo haikushambuliwa na kombora.

Alisema: “Ndege hiyo ambayo awali ilikuwa ikielekea magharibi baada ya kupaa ilikata kona kulia kutokana na hitilafu ya kiufundi na ilikuwa ikirejea uwanja wa ndege pindi ilipoanguka.”

Abedzadeh ameongeza kuwa mashuhuda waliona ndege hiyo “ikiwaka moto” kabla ya kuanguka na kuwa marubani hawakutoa taarifa yoyote ya dharura kabla ya kujaribu kurudi uwanja wa ndege wa Imam Khomeini.

“Ndege kadhaa za ndani na nje zilikuwa zikipaa katika anga la Iran katika usawa wa futi 8,000 (kama ndege ya Ukraine). Hivyo suala la kupigwa na makombora haliwezi kuwa na ukweli wowote,” alieleza afisa huyo wa masuala ya anga.

Alikuwa akijibu madai yaliyotolewa na viongozi wa nchi za Canada, Uingereza, Sweden na Marekani kuwa ndege hiyo ilidunguliwa na makombora ya Iran kimakosa.

Ndani ya ndege hiyo kulikuwa na abiria 82 wa Iran, 63 wa Canada, 11 Ukraine pamoja na wafanyakazi 11 wa ndege, 10 Sweden, wanne Afghanstan, watatu Britons na watatu Wajerumani.  Kumi na tano kati ya waliokufa ni watoto.

Viongozi hao wakiongozwa na Canada na Uingereza, wanataka uchunguzi wa kina ufanyike, kubaini chanzo halisi kilichosababisha ajali iliyowaua watu wote 176 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Mamlaka za Iran zilidai kuwa ndege hiyo ya Ukraine iliyoanguka Iran ilitaka kusitisha safari yake kutokana na kuwapo kwa hitilafu katika moja ya injini zake.

Ikaongeza kuwa haitakabidhi kisanduku cheusi cha kuhifadhi taarifa za ndege kwa kampuni ya ndege ya Boeing ama serikali ya Marekani kwa uchunguzi wa ajali hiyo.

Hatua hiyo inatokana na mzozo uliokomaa baina ya Marekani na Iran, hasa baada ya Trump kuagiza shambulio la anga lililomuua Jenerali wa Iran Qasem.

Kufuatia tukio hilo, maombolezo ya kuwaombea wafanyakazi na abiria waliokuwamo kwenye ndege hiyo yameendelea kwenye jumba la makumbusho yaliyoko katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kyiv’s, Boryspil.

error: Content is protected !!