Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Gambo avutana na Dk. Nchemba kuhusu mfumuko wa bei, Spika atoa agizo
Habari za Siasa

Gambo avutana na Dk. Nchemba kuhusu mfumuko wa bei, Spika atoa agizo

Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha mjini, (Ccm)
Spread the love

 

MBUNGE wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, amekataa kupokea taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, iliyoeleza kwamba mfumuko wa bei za vyakula unasababishwa na vita kati ya Ukraine na Urusi, mabadiliko ya tabia ya nchi na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), akidai kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti upandishaji holela wa bidhaa hizo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Tukio hilo limetokea leo Jumanne, tarehe 31 Januari 2023, bungeni jijini Dodoma baada ya Dk. Mwigulu kumpa taarifa Gambo ya kwamba Serikali haitumii kisingizio cha sababu hizo kukwepa jukumu lake dhidi ya mfumuko wa bei.

“Serikali haijajificha kwenye anachosema Ukraine wala UVIKO-19 wala tabia ya nchi, nimempa taarifa kwamba haya mambo ni uhalisia wala si kisingizio na Serikali imechukua hatua ambazo kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na SADC hakuna nchi imechukua hatua hizo za kutoa Sh. 100 bilioni kila mwezi kwa ajili ya kupunguza gharama ndiyo maana unaona nchi jirani wanakimbilia kuchukua vitu hivi katika nchi yetu,” amesema Dk. Mwigulu.

Waziri huyo wa fedha amesema kuwa, Serikali inaendelea kuchukua jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei ya vitu.

Hata hivyo, Gambo aligoma kupokea taarifa hiyo akidai “mimi siipokei sababu ni wajibu wake kuitetea Serikali, unaweza ona Serikali imetoa ruzuku ndiyo maana tukafika bei ya mchele Sh. 2,090 kwa kilo, tunasema baada ya hapo mbona hamuangalii kwa wananchi kunavyoendelea watu wanaamua kujiuzia wanavyotaka?”

Gambo aliitaka Serikali iangalie namna ya kupunguza mfumuko wa bei ili kuondoa manung’uniko yanayotolewa na wananchi kuhusu mfumuko wa bei za vyakula.

“Sisi tunatokana na Serikali hii na chama chenye serikali, lakini tunaowajibu wa kuwasemea wananchi sio kutetea kila kitu. Naomba Serikali kwa ujumla watusaidie kufanya utafiti na kuangalia kama kuna mahali kokote wafanyabiashara walikuwa wanaongeza gharama waende wakasimamie huko,” amesema Gambo.

Awali, Gambo alisema mfumuko wa bei ya vyakula umefanya maisha ya wananchi kuwa magumu kwa kuwa baadhi yao hawana ajira na hata wenye ajira vipato vyao ni vidogo haviwezi kumudu gharama za maisha.

Kufuatia mchango huo wa Gambo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameitaka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, ipeleke bungeni takwimu zinazoonyesha namna Serikali inavyochangia kupunguza mfumuko wa bei hususan za vyakula.

“Naamini upande wa Serikali mtapata fursa ya kuchangia, itakuwa vizuri kuliweka vizuri jambo hili kama alivyosema waziri wa fedha. Kama bei ni zile baada ya Serikali imewekeza fedha kiasi fulani, bei zingekuwaje kama serikali ingekuwa haijaweka pesa yake ili wananchi wapate picha ya mchango wa serikali kwenye hicho ambacho mbunge amekuwa akichangia,” amesema Spika Tulia na kuongeza:

“Ziwekwe takwimu pia, sababu mbunge ameweka takwimu na serikali ikiweka takwimu mwananchi ataelewa zaidi.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!