MKOA wa Dodoma umeshika nafasi ya kwanza kati ya mikoa 31 kwa mwaka 2023 katika miradi iliyokaguliwa na kuzinduliwa na mbio za Mwenge nchini. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma… (endelea).
Hayo yamebainishwa na leo tarehe 29 Novemba 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule katika kikao kazi kilichofanyika jijini humo na kujumuisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wataalam mbalimbali wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Amesema mkoa huo umepanda kutoka nafasi ya 22 kati ya 31 kwa mwaka 2022 na kushika nafasi ya kwanza kati ya mikoa 31 kwa 2023.
Ni katika ukaguzi, uzinduzi wa miradi na shamrashamra za namna viongozi walivyoshiriki katika kukimbiza Mwenge wa Uhuru mkoani Dodoma.
“Tumetumia siku ya leo kufanya tathmini kama ambavyo huwa tunafanya miaka yote ya kuona namna ambavyo tumetekeleza ubora wa miradi na vigezo vingine vilivyowekwa katika shughuli za Mwenge wa Uhuru.
“Tunamshukuru Mungu halmashauri tano za Dodoma Jiji, Kondoa DC na TC, Mpwapwa na Kongwa zimeingia katika 10 bora ya Taifa.
“Mwaka jana 2022 mkoa ulishika nafasi ya 22 hatukupendezwa na matokeo hayo, tulipeana shime ya kuifaharisha Dodoma na tukaungana kupambania mkoa na tunamshukuru Mungu kwa mara ya kwanza tumeshika nafasi ya kwanza kitaifa tumeifahalisha Dodoma na makao makuu ya nchi,” amebainisha Senyamule.
Katika kuelekea msimu wa kilimo Afisa kilimo wa Mkoa wa Dodoma, Bernald Abraham amesema wapo tayari kwa uzinduzi wa msimu wa kilimo unaotarajiwa kuzinduliwa Novemba 29 mwaka huu katika kata ya mazae wilayani Mpwapwa.
Leave a comment