Thursday , 2 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Dk. Shoo amaliza mgogoro Konde, uchaguzi wafanyika, aliyeng’olewa agoma
Habari MchanganyikoTangulizi

Dk. Shoo amaliza mgogoro Konde, uchaguzi wafanyika, aliyeng’olewa agoma

Spread the love

MKUTANO Mkuu wa dharura ulioitishwa na kiongozi Mkuu wa kanisa la Kiinjiri la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo umemuondoa kwenye nafasi yake Dk. Edward Mwaikali ya kuwa askofu wa Dayosisi ya Konde na kumchagua Mchungaji Geofrey Mwakihaba kushika wadhifa huo kwa sasa. Anaripoti Kenneth Ngelesi, Mbeya …(endelea).

 

Uamuzi wa kufanyika uchaguzi ulifanywa na Wajumbe wa Mkutano mkuu wa dharura ulioitishwa na Dk. Shoo ambao ulikuwa kwa ajili ya kupokea taarifa ya tume chini mwenyekiti wake Dk. Alex Malasusa ambapo ulifanyika katika Usharika wa Uyole jijini Mbeya.

Tume hiyo iliundwa kwa ajili ya kufuatilia na kuchuguza kiini na kuja na mapendekezo juu ya mgogoro wa kuhamisha Makao makuu ya Dayosisi ya Konde kutoka Mjini Tukuyu kuja Mbeya Mjini ambao umedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja.

 

Akisoma taarifa ya tume hiyo Rogath Mollel ambaye pia ni katibu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria -Mwanza amesema walibaini mambo mengi mojawapo ni utaratibu wa kuhamisha Makao Makuu ya Dayosisi bila kuwashirikisha waumini licha ya kuwa ulikuwa na nia njema.

Aidha, katika taarifa hiyo Mollel amesema kamati pia ilibaini kuwa Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Konde imekuwa ikipuuza maamuzi ya Mkutano Mkuu ambacho ni chombo cha mwisho chenye maamuzi na Dayosisi kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo.

Hata hivyo, mbali na kubaini hilo tume hiyo imetoa mapendekezo kadhaa likiwemo la kurejesha makao makuu ya Dayosisi Mjini Tukuyu pamoja na kuwarudisha wachungaji wote waliofukuzwa.

Aidha, tume imesema kutokana na hali hiyo Askofu Dk Mwaikali amekosa sifa ya kuwa Askofu pamoja na wakuu wa majimbo matatu licha ya kuwepo utaratibu wa kuanzisha Dayosisi mpya ya Mbeya.

Baada ya taarifa ya tume wajumbe wa mkutano huo walioneshwa kutoridhishwa na uongozi wa Dk. Mwaikali pamoja na halmashauri ndipo wakaamua kupiga kura ya kutokuwa na imani na kiongozi huyo wa kiroho licha ya kutohudhuria mkutano huo.

Katika mkutano huo baada ya wajumbe kuonyesha kukosa imani na uongozi mzima, ndipo ikaamuliwa kupiga kura ambapo wajumbe 204 walionyesha kutokuwa na imani, kura tano walikuwa na imani naye huku kura mbili zikiharibika.

Akiongozi kikao hicho Dk. shoo amesema kwa mujibu wa taratibu kitendo cha wajumbe kuonyesha kutokuwa na imani, kuna haja ya kufanyika uchaguzi wa kuwapata Askofu, Msaidizi, wakuu wa Majimbo saba kutoka Dayosisi ya Konde pamoja na wakuu idara.

Mkutano Mkuu huo umemchagua aliyewahi kuwa msaidizi wa Askofu Dk. Mwaikali kabla ya kujiuzulu kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wa kuhamisha Dayosisi.

Pia umemchagua Mchungaji Geofrey Mwakihaba kuwa Askofu Mteule wa Doyosisi ya Konde kwa kura 149 dhidi ya kura 55 za Mchungaji Dk. Meshack Njinga.

Mwakihaba aliibuka mshindi katika duru ya pili ya upigaji kura baada ya ule wa awali kupata kura 124 ambapo kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi hakufikisha robo tatu ya wajumbe wa mkutano.

Dk. Njinga alipata kura 61 na Dk. Andrea Mwalilimo alipata kura 24.

Aidha, mkutano mkuu ulimchagua Dk. Njinga kuwa Msaidizi wa Askofu kwa kupata kura 187 baada ya washindani wake katika nafasi hiyo Dk. Ipyana Mwagobole na Dk Michael Ambangile kuyaondoa majina yao katika kinyang’anyiro hicho.

Dk. Shoo amesema sababu ya kuitisha Mkutano huo ni baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa waumini wa kanisa hilo na licha ya kutoa ushauri wa kuumaliza mgogoro huo kutofanyiwa kazi.

Aidha, Dk. Shoo amesema wanakonde hawana budi kufuata mapendekezo yalitolewa na tume ya kuirejesha Dayosisi Mjini Tukuyu kama ambayo ilishauriwa awali.

Dk. Shoo pia amekemea tabia ambayo imekuwa ikiibuka juu ya ukabila katika Dayosisi ya konde na kwamba wanapaswa kutambua kuwa konde ni mali ya wana KKKT wote na si wanyakyusa, wakinga wala wasafwa.

Ameongeza kuwa kauli hiyo imekuwa ikitolewa kwa lengo la kuhalalisha uovu.

“Niwaombe kwamba mtoe ushrikiano kwa wateule lakini naomba nikemee tabia inayoelezwa ya ukabila… Dayosisi ya konde ni ya waamini wa KKKT wote,” amesema Dk. Shoo.

Aidha, aliipongeza tume hiyo kwa kufanya kazi nzuri na utulivu wa wanakonde wote licha ya vurugu za hapa na pale.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa Mchungaji Mwakihaba amesema mgogogoro huo ulikuwa ni darasa kwa wanakonde wote lakini mwalimu wa hilo alikuwa Yesu Kristo na ndio maana limeisha.

“Mgogoro umetufundisha kufahamiana na kujuana nani ni nani kwa sisi wanakonde lakini nisema tu hapa tutahitaji wazee kwa ajili ya kuindesha Dayosisi kwani safari ilikuwa ya maumivu na majeraha katika mioyo,” amesema Mwakihaba.

Naye Dk. Mwaikali akizungumzia kuhusu uchaguzi na mabadiliko hayo, kuwa mkutano huo hautambui kwani hakupata mwaliko wake, lakini pia hajapata barua yoyote yenye kueleza mabadiliko.

“Siwezi kuongea jambo lolote kwa sasa kwa sababu huo mkutano sikupewa barua ya mwaliko na sijui kilichofanyika, kama itakuja barua yenye maelezo hayo nitaongea rasmi na kuweka msimamo,” amesema Dk. Mwaikali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

Habari MchanganyikoKimataifa

Ruto amteua Kahariri kuwa mkuu wa majeshi

Spread the loveRAIS wa Kenya, William Ruto, amemteua Jenerali Charles Muriu Kahariri,...

Habari Mchanganyiko

Chongolo aonya viongozi vijiji kutouza NIDA kwa wageni

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amewaonya viongozi wa...

Habari Mchanganyiko

TUCTA, OSHA wataka kampuni za madini kuiga ubunifu wa GGML

Spread the loveSHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) pamoja na Wakala...

error: Content is protected !!