August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Milioni 160 zajenga shule pekee ya ghorofa Mbeya

Spread the love

JUMLA ya Sh milioni 160 zimekamilisha ujenzi madarasa nane ya shule ya sekondari Ihanga na kumaliza adha ya mrundikano wa wanafunzi katika darasa moja.

Shule hiyo iliyopo jijini Mbeya ndio shule pekee ya ghorofa iliyojengwa kupitia Mpango wa Serikali wa Kuinua Uchumi na kukabiliana na janga la Korona (UVIKO -19) unaotekelezwa kwa mkopo nafuu uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani kwa Tanzania (IMF). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, wameeleza furaha yao hasa ikizingatiwa awali ilishindikana kujengwa madarasa ya chini kutokana na ufinyu wa eneo la shule.

Mwanafunzi Mickson John amesema awali walikuwa wanakaa chini kujifunza.

“Hata kwenye madarasa tulikuwa tunajirundika wanafunzi wengi kwenye darasa moja. Katika darasa moja tulikuwa tunafika wanafunzi 90 ndio maana hata ufaulu wetu kitaaluma haukuwa mzuri,” amesema.

John ameungwa mkono na Mwanafunzi mwenziye aliyejitambulisha kwa jina la Lulu Andende kwamba wakati anaanza kidato cha kwanza mwaka 2019, walikuwa wengi kiasi cha kwamba katika darasa moja walikuwa tunakaa zaidi ya 50.

“Kutokana na mrundikano huo, baadhi ya wazazi waliamua kuwahamisha watoto wao katika shule hii na kuwapeleka kwingine… lakini sasa tumejengewa hili ghorofa na madarasa yapo ya kutosha,” amesema.

Aidha, Afisa Mtendaji wa kata hiyo ya Mbeya mjini, Faraja Willa naye amesema awali alikuwa akichangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, jambo ambalo lilikuwa linampa changamoto sana.

“Hata mwaka jana nilikuwa ninawaza kwamba hivi nitaanzaje kuchangisha hasa ukizingatia hili jengo lilikuwa la muda mrefu na watu wamechoka kuchanga michango.

“Kwa kweli alivyoingiza hizo fedha tarehe 21 Oktoba, mwaka 2021 binafsi nilifurahi sana.

“Napenda kumuambia Rais Samia Suluhu Hassan kwamba kazi inaonekana na aendelee kuchapa kazi kwa sababu katika maisha, si wote wanaweza kukukubali, lakini aamini kabisa asilimia 90 tupo nyuma yake,” amesema

Kwa upande wake Mkuu wa Shule, Theresia Mwaifwani amemshukuru Rais Samia kwa kuelekeza kiasi hicho cha fedha Sh milioni 160 ambazo zimewezesha kukamilisha hayo madarasa nane.

Aidha, wakazi wa eneo hilo Edwin Mwanahapa na Anyembisye Mwaisunda wamemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia fedha hizo za ujenzi wa shule na kuongeza kuwa sasa wanafuraha isiyo na kifani.

error: Content is protected !!