October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Kahangwa: Hi ndio tofauti kati ya uchaguzi wa Kenya, Tanzania

Spread the love

 

YAPO masuala ya kijiografia, kihistoria, kijamii na kiuchumi yanayofanya nchi mbili za Afrika Mashariki; Kenya na Tanzania zifanane na kuwa na udugu wa karibu.

Kijiografia, nchi hizi mbili zinapakana moja kwa moja kwa mpaka wenye urefu wa kilometa 769 kuanzia ndani ya ziwa Victoria hadi Bahari ya Hindi.

Majirani hawa hufanana pia kwa kuwa katika ukanda wa kitropiki. Kihistoria, hizi ni nchi ziliwahi kuwa chini ya utawala wa Mwingereza, zikapata uhuru katika miaka ya 60 na kuamua kuwa washirika kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki ya awali.

Kijamii, Tanzania na Kenya huzungumza lugha moja ya kitaifa, yaani Kiswahili. Pia baadhi ya makabila katika nchi hizi, kama vile wajaluo na wamasai hupatikana kotekote.

Kiuchumi, nchi hizi mbili zina mahusiano ya kibiashara kuanzia kuuziana bidhaa, kuwekeza katika pande zote na kuzungumza juu ya soko la pamoja kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata linapokuja suala la kisiasa, wanasiasa wa pande zote mbili hawako nyuma katika kushirikiana, kushauriana na wakati fulani kuigana. Zaidi ya hayo, nchi hizi mbili zinafuata mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa.

Ni katika muktadha huo kwamba kulinganisha na kutofautisha yanayojiri katika nchi hizi kunafaa sana katika kutoa mwanga wa nini wanaweza wakasomeshana na hivyo kusaidiana kupiga hatua za kimaendeleo katika nyanja zote.

Makala haya yanaangazia uwanja wa siasa, hususan chaguzi za kitaifa na za kidemokrasia za viongozi wa nchi katika vipindi vya miaka mitano mitano.

Uchaguzi wa hivi karibuni zaidi katika eneo hili la Afrika Mashariki, ni ule uliofanyika nchini Kenya, mnamo tarehe 9 Agosti 2022, kwa ajili ya kuitafuta serikali ya awamu ya tano.

Kwa jinsi uchaguzi huo ulivyoripotiwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, imekuwa katika namna ya wazi sana na ya kuvutia kuhusiana na taratibu zinatumiwa na watu wa Kenya kwenye jambo nyeti kama hili.

Mambo ya kiutaratibu na mfumo yaliyoonekana wazi ni pamoja kwamba, wakenya wanachagua viongozi wa serikali za chini na serikali kuu kwa wakati mmoja.

Wanapiga kura zisizopungua tano, kumchagua Rais pamoja na naibu wake, Gavana, Seneta, wabunge na wawakilishi katika kaunti.

Hii ni tofauti na uchaguzi wa Tanzania ambapo japo nako kuna kura zisizopungua tano;  watanzania huchagua Rais wa Muungano  na makamu wake, Rais wa Zanzibar, Wabunge na wawakilishi.

Mtanzania wa Bara hupiga kura mbili kwa wakati mmoja na mzanzibari hupiga kura tatu, katika uchaguzi mkuu. Tofauti na Kenya, uchaguzi wa serikali za mitaa za Tanzania hufanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu kwa ajili ya kuwapata madiwani wa kata.

Hapa jambo mojawapo linalojionesha katika tofauti za kimfumo, ni kwamba wakati wakenya wanawachagua magavana wao wa kaunti na wanadumu kwa miaka mitano, nchini Tanzania wakuu wa mikoa (wanaofanana magavana) huteuliwa na Rais tena katika namna ambayo hawana kipindi maalum cha kukaa ofisini.

Inategemea na Rais atakavyoona. Tofauti katika eneo hili zinachangiwa pamoja na mambo mengine, muundo wa nchi kutofautiana. Wakati Tanzania ni jamhuri ya Muungano, Kenya haina mfumo wa namna ya muungano unaohitaji kuwepo kwa marais wawili kama Tanzania.

Aidha, mengi ya yanayofanyika Kenya, mathalani uchaguzi wa magavana ni zao la Katiba Mpya ya chini hiyo iliyopitishwa rasmi mwaka 2010, ilihali Tanzania inaendelea kutumia katiba ya mwaka 1977 baada ya mpango wa kuwa na katiba mpya uliopamba moto mwaka 2014, kuzorota.

Tofuti hii inabaki kuwa ni moja ya mambo yanayofikirisha linapokuja suala la katiba mpya. Ni ama Tanzania iendelee na utaratibu wake wa kumpa Rais madaraka makubwa, hata ya kuteua ‘magavana’ wa mikoa, au madaraka hayo yarudi kwa wananchi wa mikoa husika.

Pengine hili la mwisho lina faida zake; moja wapo ni uimara (stability) katika kuongoza mkoa na uwezo wa watu kumuwajibisha mkuu wao wa mkoa.

Tofauti nyingine iko katika sura ya tume. Kupitia uchaguzi wa juzi, tumeweza kukumbuka kuwa nchini Kenya tume waliyonayo inaitwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hii ni tofauti kwa jina na mantiki ikilinganishwa ile ya Tanzania inayoitwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.  Tume ya Kenya inaitwa huru kwa sababu kupatikana kwa Mwenyekiti wake, Mkurugenzi wa uchaguzi na maafisa wengine wa tume, hakutokani na uteuzi wa Rais, ilihali kwa Tanzania wanateuliwa na Rais.

Uhuru wa tume, licha ya kuwa ni zao la katiba inayojenga demokrasia zaidi, kunaondoa uwezekano wa tume kupokea maelekezo kutoka kwa mhimili fulani wa dola, kiongozi fulani, au chama fulani cha siasa.

Tume inabaki kuwa refa tu katika mchezo wa kugombea madaraka. Kinyume chake, katika mazingira ya tume kuteuliwa na Rais, uwezekano wa kumtii wakati anagombea au anapounga mkono mgombea fulani huwaweka mashakani wagombea wengine. Naam, hata mashaka haya yaweza kuondolewa kwa katiba mpya iliyochota somo kutoka Kenya.

Vile vile imejitokeza tofauti katika uwazi wa kupiga na kuhesabu kura. Wakenya wamekuwa wazi katika kukusanya, kuhesabu kura na kutoa ripoti, wameweka kura zinazokusanywa katika mtandao wa tume, ambapo kila anayehitaji kuziona alimeruhusiwa kupakua na kujumlisha mwenyewe.

Hakukuwa na katazo kwa mgombea kujijumlishia kura na kujua hali yake, hali kadhalika vyombo vya habari navyo viliruhusiwa kwa wakati wao kujumlisha kura hizo na kuuhabarisha umma katika namna ambayo hata tusiokuwa wakenya tumeweza kufuatilia namba kwa namba.

Jambo pekee ambalo tume haikuliruhusu wengine wafanye katika mchakato huo, ni kutangaza mshindi.  Hili nalo ni somo la uaminifu na uwazi kwa Tanzania ambapo hayo hatujawahi kuyafanya.

Raila Odinga

Pengine ni muhimu tukifika mwaka 2025 (wakati wa uchaguzi mkuu mwingine wa Tanzania) nchi iwe na ukomavu huo, utakaowezesha pamoja na mambo mengine kuondoa hisia za kuibiana zinazotokana na usiri usio wa lazima.

Kenya imeonesha pia kupiga hatua katika kutumia Teknolojia. IEBC imekuwa na mfumo wa kielektroniki wa kupiga, kukusanya na kujumlisha kura kama yafanyavyo mataifa mengine ya nje ya bara la Afrika.

Matumizi hayo sio tu yanaendana na wakati wa sasa, bali yanarahisisha kazi ngumu sana ya kuendesha uchaguzi na kupunguza makosa ya kibinadamu. Ingawa upo uwezekano wa wahuni kucheza na mfumo, tume ya Kenya ilijidhatiti vilivyo kuhakikisha mfumo wao huo haudukuliwi.

Wakati umefika kwa Tanzania kutumia pia teknolojia hii. Ili Tanzania iweze kuliendea hilo kwa kasi, somo la uzoefu linaweza kuchukuliwa Kenya, na pengine kuanza kwa majaribio wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2014.

Wakati tukiusubiri huo mwaka, laweza pia kuwa jambo jema kuwapeleka sasa, maafisa wa tume zetu za uchaguzi (NEC na ZEC) wakajifunze moja kwa moja kutoka kwa maafisa wenzao wa nchini Kenya.

Kenya imejitahidi kutumia mfumo huo kwa namna ambayo matokeo yaliweza kuhakikiwa kwa kulinganisha fomu za namna tatu tofauti (34A, 34B na 34C) na kuwa na jopo la wathibiti-ubora.

Kenya imekuwa pia na kasi katika kukamilisha mchakato wa uchaguzi. Mathalani, ndani ya wiki moja tangu kupigwa kwa kura, IEBC sio tu ilitakiwa kisheria kutangaza mshindi, bali ilifanikiwa kufanya hivyo siku moja kabla ya makataza (deadline).

Kasi hii hapana shaka imechagizwa na matumizi ya teknolojia na umahiri wa waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi.  Hata hivyo, kasi yao imezidiwa na ile ya NEC ambapo mwaka 2020 iliweza kumtangaza mshindi wa Urais siku mbili tu baada ya kura kupigwa.

Watanzania tulipiga kura tarehe 28 Oktoba 2020 na Hayati Dk. John Magufuli alitangazwa mshindi tarehe 30 Oktoba 2020. Katika hilo, Kenya inaweza kujiuliza kwa Tanzania ni namna gani muda unaweza kutumika kwa ufanisi kiasi hicho bila kuwaweka wananchi na wagombea roho juu kwa muda mrefu.

Uchaguzi wa 2022 nchini Kenya umeshuhudia wakenya waishio nje ya nchi yao (Diaspora) wakitumia haki yao ya kuchagua viongozi kwa kupiga kura kule kule waliko. Ingawa sio nchi zote, angalau wakenya walioko katika mataifa 12 waliweza kupiga kura.

Mataifa hayo ni Afrika Kusini, Burundi, Rwanda, Tanzania na Uganda (kutoka bara la Afrika); Canada na Marekani (kutoka bara la Amerika ya Kaskazini); Falme za Kiarabu na Qatar (kutoka bara la Asia); kadhalika Uingereza na Ujerumani (kutoka bara la Ulaya).

Hata hivyo, ushiriki huo bado si mzuri kwa sababu wakenya wa Diaspora wanafikia zaidi ya milioni, ilhali waliopiga kura ni zaidi kidogo ya elfu kumi.

Aidha, kwa kuwa Kenya iko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, ingependeza kama wanachama wote wa jumuiya hii wangekuwa na vituo vyao vya kupigia kura. Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini zisingeachwa nyuma.

Kama hili nalo ni somo kwa Tanzania, kwa maana ya kuwapa haki ya uchaguzi watanzania waishio nje basi tunaye jirani wa kutupatia uzoefu wa kuendesha utaratibu huo kama sio bila shida basi kwa changamoto kidogo. Ifikapo 2025, hili linawezekana.

Vile vile kwa mujibu wa sheria na taratibu za uchaguzi nchini Kenya, kuna fursa ya matokeo ya urais kupingwa mahakamani.

Kenya tayari ina uzoefu wa kufanya hivyo, kwani mwaka 2017 uchaguzi ulipingwa mahakamani na ukafutwa, kabla ya kurudiwa tena na kumpa kibali Rais Uhuru Kenyatta kuendelea na muhula wa pili wa uongozi.

Wakenya pia hupinga matokeo ya ngazi za chini mahakamani. Katika uchaguzi wa juzi, wapo ambao wamekwisha kujiandaa kwa hilo. Kwa Tanzania, udiwani na ubunge waweza kupingwa kisheria, ila la kupinga ushindi wa Rais bado hatujafika huko.

Tanzania inalo somo hapo. Mahakama zipo kusimamia haki, kama haki ya mgombea mmojawapo inakandamizwa au kama taratibu za uchaguzi zimekiukwa haki itendeke kupitia muhimili wa kutafsiri sheria. Hayo yatawezekana kupitia katiba ijayo na kwa kurekebisha sheria zetu za uchaguzi.

Jambo jema jingine lililojitokeza Kenya, ni ruksa ya ushirika wa vyama vya siasa kusimamisha mgombea wa pamoja.

Katika uchaguzi uliomalizika kwa mfano, kumekuwa na ushirika wa Kenya kwanza (ukiweka pamoja vyama vya UDA, ANC, FORD – Kenya, EFP, TSP, UMP, TWP, CCK, DPK, FP na DP) na ushirikia wa Azimio la Umoja (uliojumuisha vyama vya ODM, Jubilee, WDM, KANU, NARC, MP, MCC, DAP-K, DEP, UPIA, UDM, PAA, KUP, UDP, NLD na vingine). Tume ya uchaguzi ilitambua umoja wa vyama.

Kwa upande wa Tanzania, jaribio la umoja wa vyama liliwahi kuwepo. Mathalani, mwaka 2015 vyama vinne vya siasa viliunda UKAWA (CHADEMA, CUF, NCCR na NLD).

Hata hivyo, NEC haikuutambua umoja huo na hivyo haukuwa kwenye karatasi za kupiga kura. Ili Tanzania iweze kwenda huko pia (kama kuna haja), basi lazima sheria ya uchaguzi ibadilike.

Kenya imemaliza lake na kufanikiwa kuionesha dunia wakenya ni akina nani. Zamu ya Tanzania yaja. Itakuwa heri ifikapo, hatua kadhaa ziwe zimepigwa katika maendeleo ya kidemokrasia na namna bora zaidi ya kufanya chaguzi.

 Makala haya yameandaliwa na Mhadhiri Mwandamizi wa Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa.

error: Content is protected !!