October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msimamizi Uchaguzi aliyetoweka, auawa na wasiojulikana

Daniel Mbolu Musyoka

Spread the love

 

OFISA wa uchaguzi wa Embakasi Mashariki kutoka nchini Kenya, Daniel Mbolu Musyoka (53) aliyetoweka tarehe 11 Agosti, 2022 amepatikana akiwa amefariki. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa… (endelea).

Msimamizi huyo alikuwa katika kituo cha kujumlisha kura cha East African School of Aviation alipotoweka muda wa saa nne kasorobo asubuhi. Taarifa ya kutoweka kwake ilikuwa ilitolewa kwa polisi.

Mwili wake ulipatikana jana tarehe 15 Agosti, 2022  kwenye kichaka katika eneo la Mariko lililopo katika Msitu wa Kilombero nchini humo na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha eneo hilo.

Polisi waliotembelea eneo la tukio walisema marehemu alionekana kuteswa hadi kufa. Familia ya marehemu na polisi kutoka Embakasi walitembelea chumba cha kuhifadhia maiti na kuutambua mwili huo. Nia ya mauaji na waliomuua Mbolu bado haijajulikana.

Aidha, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kulikuwa mipango kuhamisha mwili huo hadi Nairobi leo.

Hapo awali, maafisa wa polisi walipata picha za CCTV zinazoonyesha matukio ya mwisho ya Musyoka.

Picha hizo zilikuwa zikichunguzwa na kitengo cha uhalifu wa mtandaoni na polisi walisisitiza kuwa Musyoka alikuwa salama ingawa alikokuwa ilibaki kitendawili.

Alipotoa tangazo la kutoweka kwa Musyoka, Mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo -IEBC, Wafula Chebukati alisema walijaribu kumtafuta lakini hawakufanikiwa.

Wafula Chebukati, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC)

“Familia ya Musyoka na Tume wamekuwa wakijaribu kumtafuta bila mafanikio. Ripoti ya mtu aliyepotea imetolewa katika kituo cha polisi cha Embakasi,” Chebukati alisema Jumatatu akiongeza kuwa hajulikani aliko.

Aliongeza kuwa wafanyakazi wengine wengi wa tume wamenyanyaswa na kutishwa.

Mke wa marehemu, Tabitha Mbolu na bintiye Prudence Mbolu walizungumza naye mara ya mwisho kwa simu kabla ya kutoweka.

Prudence alifichua kwa wanahabari kwamba wafanyakazi wenza wa mumewe katika IEBC walimpigia simu baada ya kushindwa kumpata mumewe kwa njia ya simu.

Polisi kwa upande wao walisema walikuwa wakimtafuta bila mafanikio. Timu tofauti zilikuwa zimetumwa kuzunguka jiji na kutafuta njia tofauti katika nia ya kumtafuta afisa huyo aliyepotea ambaye hakuwa amelala kwa siku tatu baada ya mchakato wa kujumlisha kura kuanza.

error: Content is protected !!