Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Corona yatinga Z’bar, Rais Mwinyi: Imeathiri watu wetu
Habari za SiasaTangulizi

Corona yatinga Z’bar, Rais Mwinyi: Imeathiri watu wetu

Rais Hussein Ali Mwinyi
Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekiri hadharani kuwa visiwa hivyo, ambavyo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vinakabiliwa na janga hatari la corona (COVID-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu, mara baada ya swala ya Ijumaa, jana tarehe 5 Machi 2021, katika Msikiti wa Mfereji wa Wima, Unguja, Dk. Mwinyi alisema, Zanzibar imeingiliwa na corona, jambo ambalo limeathiri uchumi wa nchi.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Zanzibar, ambaye kitaaluma ni daktari, kukiri hadharani kuwapo kwa ugonjwa huo nchini.

Amesema, “ndugu zangu, tumekabiliwa na tatizo hili la ugonjwa huu wa COVID ambao umeathiri afya za watu wetu na uchumi wa nchi yetu.”

“Ndugu zangu, tumekabiliwa na tatizo hili la ugonjwa wa COVID, ambao umeathiri afya za watu wetu na uchumi wa nchi yetu.”

“Lakini mwelekeo unaonekana ugonjwa huu unapungua na Inshallah kwa dua zetu ugonjwa huu utakwisha na uchumi wetu utarudi katika hali ya kawaida,” alisema Rais Mwinyi.

Hatua ya Rais Mwinyi kukiri kuwapo kwa corona Zanzibar, imekuja takribani wiki tatu, tangu aliyekuwa Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.

Maalim Seif alikutwa na mauti, tarehe 17 Februari 20121, katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Alizikwa siku iliyofuata – Alhamisi ya tarehe 18 Februari 2021,– kijijini kwake Mtabwe, mkoa wa Kaskazini Pemba.

Kabla ya kufariki dunia, chama chake kilieleza kuwa Maalim Seif amelazwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja, baada ya kugundulika kuwa na maradhi ya corona.

Taarifa ya chama hicho, iliyotolewa na Nassoro Mazrui, naibu katibu mkuu wa ACT- Wazalendo (Zanzibar), ilieleza kuwa mbali na Maalim Seif, wasaidizi wake kadhaa, nao wamepata maambukizi ya ugonjwa huo.

Naye Maalim Seif, siku tano baadaye, akakiri kulazwa hospitali kwa maradhi ya corona; na akathibitisha baadhi ya wasaidizi wake, akiwamo mkewe, Awena kuumwa maradhi hayo.

Hata hivyo, Rais Mwinyi amesema, “kwa sasa, maambukizi ya ugonjwa huo, yameanza kupungua.”

Haya yanatokea katika kipindi ambacho, vyama vya upinzani nchini Tanzania na mashirika ya kidini, yakipaza sauti, kushinikiza serikali kutoa takwimu sahihi za waathirika wa ugonjwa huo, pamoja na vifo.

Akizungumza jana Ijumaa, na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, Katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, aliitaka serikali kutoa hadharani takwimu za vifo vya watu walioambukizwa Korona.

Naye Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, katika waraka wake kwa wanachama na viongozi wa chama chake, ameeleza kuwa ni muhimu wanachama hao kujikinga na virusi vya corona kwa kutumia njia za kitaalamu, badala ya njia za kienyeji zinazohimizwa na viongozi wa serikali.

Amesema, tiba hizo asili zinazopigiwa chapuo na baadhi ya mawaziri wa serikali ya Rais John Magufuli, “hazina ithibati ya kitaalamu na kitabibu juu ya usalama; na ufanisi wa kukabiliana na Korona.”

Aidha, chama hicho ambacho ni mshirika wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani (SUK), kimetaka serikali kuchukua hatua zinazopendekezwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ikiwamo kutambua Korona kuwa janga la dharura.

Ado Shaibu, Katibu Mkuu ACT-Wazalendo

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), kupitia katibu mkuu wake, Padri Dk. Charles Kitima, limesema kuwa ndani ya siku 60 zilizopita, kanisa limepoteza mapadri zaidi ya 25 na masista na manesi 60, kutokana na matatizo ya kupumua.”

Padre Dk. Kitima aliwaambia waandishi wa habari, Jumatano iliyopita, kwamba wingi huo wa vifo katika kanisa hilo, haujapata kutokea.

Alisema, “corona ipo, na kwamba wananchi wasifanye mzaha katika hilo.”

Hata hivyo, TEC imesema, wao kama kanisa, hawafahamu vifo vinavyotokea kwa sasa kama ni corona au la, kutokana na hospitali wanazomiliki kutokuwa na vifaa vya kisasa vya upimaji, lakini wanaambiwa “watu wanafariki kwa tatizo la kupumua.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

error: Content is protected !!