CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewasilisha mapendekezo makuu manne mbele ya Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, juu ya miswada ya marekebisho ya sheria za uchaguzi, iliyowasilishwa na Serikali bungeni jijini Dodoma Novemba 2023. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Mapendekezo hayo yamewasilishwa leo tarehe 10 Januari 2024 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, mbele ya kamati hiyo bungeni jijini Dodoma baada ya wadau mbalimbali ikiwemo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (THRDC), kuwasilisha kuwasilisha maoni yao.
Pendekezo la kwanza lililowasilishwa na Chadema ni Serikali kuondoa bungeni miswada hiyo kwa madai kuwa haijajibu matatizo ya msingi ya muundo wa tume ya taifa ya uchaguzi wala sheria za uchaguzi, wakati la pili likiitaka Serikali iwasilishe bungeni muswada wa kukwamua mchakato wa upatikanaji katiba mpya.
Pendekezo la tatu, ni Serikali iwasilishe bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpito ya katiba ya sasa ili kuwezesha upatikanaji wa chaguzi huru na za haki baada ya kuondoa vifungu vya kikatiba vyenye mapungufu.
La mwisho ni, Serikali kupeleka muswada wa sheria itakayowezesha tume ya taifa ya uchaguzi kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa badala ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Chadema kimetaja maeneo ya katiba yenye mapungufu ambayo yanatakiwa kurekebishwa ili kuboresha mfumo wa uchaguzi, ikiwemo Ibara ya 39 (2) ya katiba, ili kuondoa ulazima wa mtu kuwa mwanachama wa chama cha siasa ndipo awe na sifa za kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chama hicho kimependekeza ibara ya 41(7) ya katiba ifanyiwe marekebisho ambayo inakataza matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, ili wapiga kura au wagombea wawe na haki ya kuhoji matokeo hayo kwenye Mahakama ya Rufani.
Leave a comment