MKUU wa Majeshi nchini (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, amesema kuna tishio la ongezeko la vijana wa kitanzania kujiunga na vikundi vya kigaidi katika mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Msumbiji na Somalia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
CDF Mkunda ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Januari 2024, katika mkutano wa saba kati yake na makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jijini Dar es Salaam, ambao umefunguliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine, CDF Mkunda amesema katika mikoa ya Tanzania upande wa magharibi, inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la wakimbizi na waomba hifadhi wa muda mrefu kutoka Burundi, Rwanda, DRC, kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi kwa kuwa baadhi yao wanafanya njama kuhakikisha wanapata uraia na nafasi nyeti za uongozi serikalini.
“Waomba hifadhi bado wanaendelea kuishi vijijini na kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha uzao wao unapata uraia wa Tanzania bila kufuata sheria. Kuanzia Januari hadi Disemba 2023 watu 138149, waomba hifadhi walipokelewa Tanzania na kutokana na mahojiano wamebainika wamekuja kwa sababu za kiuchumi na zinawakosesha sifa ya kupewa hadhi ya ukimbizi,” amesema CDF Mkunda.
Amesema “Ni maoni yetu kwamba, kuendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa waomba hifadhi na wakimbizi nchini ni tishio la kiusalama kwani taarifa zilizopo ni kwamba baadhi ya waomba hifadhi au familia zao wameajiriwa serikalini kwa nafasi mbalimbali na wengine wamepewa teuzi serikalini katika nafasi nyeti za maamuzi.”
CDF Mkunda amesema matishio hayo yameendelea kudhibitiwa kwa ushirikiano wa jeshi na vyombo vingine vya usalama.
Kuhusu hali ya usalama katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji, CDF Mkunda amesema iko shwari baada ya vikosi vya kijeshi vya SADC na vya serikali ya nchi hizo mbili kufanya kazi kubwa.
Aidha, amesema vikosi vya SADC vinatarajiwa kuondoka Machi mwaka huu kitendo kinachoweza hatarisha usalama wa mpaka huo kutokana na kikundi cha kigaidi bado kuendelea kuwa na nguvu.
Akizungumzia mkutano huo, CDF Mkunda amesema utafanyika kwa muda wa siku tano ambapo lengo lake ni kujadili namna ya makanda hao kutekeleza majukumu yao ya msingi ya ulinzi wa nchi.
Leave a comment