CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakihitaji ushindi wa makandokando katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024 na kwamba kinajipanga kuandaa wagombea bora pamoja na kuongeza idadi ya wapiga kura ili kishinde kwa misingi ya kidemokrasia. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Akizungumza katika mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Emanuel Nchimbi na viongozi wa chama hicho Mkoa wa Katavi, leo Jumamosi, Katibu wa Oganaizesheni CCM, Issa Gavu, amesema uchaguzi wao ni wa kidemokrasia ambao unakwenda na hesabu ya wingi wa kura za wananchi.
“Katika uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji, kitongoji ama mtaa tunachohitaji CCM ni ushindi, hatuhitaji ushindi unaotokana na makandokando tunahitaji ushindi unaotokana na wagombea wenye sifa na utayari wa kupeperusha bendera ya chama chetu. Tukipendekeza wagombea wazuri hatuna sababu ya kuendekeza rushwa wala kuendekeza wachache wasiotaka maslahi ya wengi,” amesema Gavu.
Aidha, Gavu amesema CCM kinawaonya wabunge na madiwani wenye tabia ya kupanga safu za viongozi wa serikali za mitaa kupitia uchaguzi huo, huku akiwatahadharisha wajumbe kutopitisha wagombea wenye makandokando.
“Tunayo nafasi ya kupima viongozi wetu wenye dhamira kugombea, uongozi wa wilaya ndio tumewapa majukumu ya katiba kutuorodheshea wagombea wa nafasi za wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji tunawaomba hakikisheni haki inatendeka acheni kupanga safu kwa kuogopa madiwani na wabunge, pangeni safu ya ushindi,” amesema Gavu.
Gavu amesema “ tunataka tuhakikishe kwamba kila mgombea anayetoka CCM hatupati mwenye makandokando tunataka mgombea yuko safi akikwekwa asubuhi tayari saa nne CCM tumeshinda. Tukikumbatia watu wenye makandokando likitajwa tatizo la ardhi mwenyekiti yumo huyo hana nafasi ndani ya CCM.”
Gavu amewataka wanachama wa CCM kuongeza juhudi za kupata wanachama wapya pamoja na kuwahimiza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwani ndio njia pekee ya kupata ushindi “idadi ya wana CCM iwe nyingi na kubwa maana yake ushindi wa chama chetu utakuwa wa wazi.”
Leave a comment