Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi CAG apewe ulinzi atake asitake
Makala & Uchambuzi

CAG apewe ulinzi atake asitake

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nchini Tanzania, Charles Kichere
Spread the love

 

FIKIRIA unarudi nyumbani kwako, unakutana na kisanga cha vijana wawili wameraruriwa na mbwa wako, na wako taabani. Unauliza unaambiwa ni vibaka wameruka ukuta kutaka kuiba. Anaandika Joseph Kulangwa, Dar es Salaam … (endelea).

Unawapongeza mbwa wako kwani bila wao, hali ingekuwa mbaya. Unawapa chakula unawaacha wapumzike. Hao ni mbwa ni wanyama wasaidizi wa binadamu katika masuala ya usalama.

Lakini baada ya muda ukishasahau, ukakutana na mtu ukakorofishana naye akakuita mbwa, utachanganyikiwa kwa hasira na unaweza kumshambulia na hali ya hewa ikachafuka.

Najiuliza, ni kwa nini mtu akiitwa mbwa anakasirika au akifananishwa na mnyama huyo anajisikia vibaya, lakini mbwa huyo huyo anapofanya mazuri ya kumsaidia anajisikia vizuri?

Linapokuja suala la Kiingereza, ndipo utasikia mtu anafurahia kuitwa ‘watchdog’, kwamba ni mwenye jukumu la kufuatilia mambo, hususan linapokuja suala la utendaji wa Serikali.

Nachelea kumwita Mdhibiti wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mbwa, lakini namwita ‘watchdog’, kwa kazi anayoifanya kila mwaka na kumwachia mmiliki wa mbwa kumalizia kilichosalia.

Lakini kazi anayoifanya ni sawa kabisa na yule mbwa aliyewararua wale vibaka. Vibaka wamo serikalini na CAG ndiye huwasaka na kuwararua na wakishalegea, anawaachia wakubwa au mabwana kufanya kazi ya kuwawajibisha.

Yawezekana kabisa Watanzania wengi hawajui CAG ni nini na anafanya kazi gani na kwa vipi. Ni kweli kabisa taasisi hii inaonekana kama jidubwana linalotumwa tu kufukua na kufukunyua na kuja na ripoti ya kushangaza.

Hivi nani alijua kuwa CAG, Charles Kichere angeibuka na madudu yale ambayo yeye hataki kuyaita madudu, bali matokeo ya ukaguzi wake, hususan katika kipindi kile tukiongozwa na Hapa Kazi Tu?

Ukifuatilia ripoti yake utajua kuwa ana kazi kubwa na ngumu kama si nzito, tena yenye hatari fulani hivi. Si kazi ndogo kuchokonoa nyoka pangoni akakuacha salama. Lakini CAG kamchokonoa na kumweka hadharani na hata sumu yake kuibainisha.

Kwa msiojua, CAG huteuliwa na Rais wa nchi, kwa ajili ya kufanya kazi za ufuatiliaji utekelezaji wa mambo mbalimbali ya Serikali na kuhakikisha yanakwenda vizuri na kwa maslahi mapana ya nchi.

Uteuzi wake huzingatia taaluma, uzoefu na ujuzi katika uongozi, hivyo bila mambo hayo muhimu sifa ya kuwa CAG inakosekana kabisaa, kwani kinyume chake asiye na sifa atababaisha na kuiingiza nchi matatizoni.

CAG ndiye mwidhinisha malipo kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, na hiyo ni baada ya kuhakikisha, kwamba fedha zinazokusudiwa kutokewa mfukoni humo, zina kibaki na idhini ya Bunge.

Hivyo mkiona mtu anatapanya fedha barabarani, mjue kuna jambo nyuma yake, bila shaka hakuna Bunge linaloweza kuidhinisha mapesa yamwagwe ovyo hadharani kwa wapita njia, kwa lengo la kiki!

Akimaliza hapo, CAG pia anahakikisha matumizi ya fedha hizo yanakwenda sambamba na malengo kusudiwa. Hapo maana yake si kuwa basi fedha zimeshatolewa kwa ajili ya mradi fulani wewe unakwenda kununulia sidiria, gagulo, boksa au nepi ya mwanao.

Baadaye hupitia kila matumizi kukagua kama kweli yalifanywa ilivyopangwa na kisha hutoa taarifa ya ukaguzi wake, unaohusu hesabu za Serikali, Mahakama na Bunge, yaani mihimili mitatu ya Dola. Na hufanya hivyo angalau mara moja kwa mwaka.

Sasa jambo la msingi nikwambieni ni kuwa. Mtu huyu CAG akiwa anatekeleza majukumu yake hayo, ni marufuku kulazimishwa na idara au mtu yeyote kufuata maelekezo yake, maana yake ana uhuru wa kutenda aonayo yanafaa bila kuhojiwa au kuelekezwa,

Akiona umri wake wa kufanya kazi hiyo umekwenda, atajiondokea mwenyewe, lakini akiwa amefikisha miaka 65, na anaweza kuhudumu katika nafasi hiyo kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

Lakini hiyo haizuii kuondoka madarakani endapo atakumbwa na maradhi au utovu wa nidhamu kazini, hapo kwa kweli hakuna mtu atakayevumilia, hasa hilo la utovu wa nidhamu, lakini hili la maradhi lazima madaktari wahusike.

Ngoma sasa ni pale Rais atakapolala na kuamka, akaona jamaa hamfai na akataka kumng’oa! Unajua nini? Lazima iundwe Tume maalumu ya majaji au waliowahi kuwa majaji wa Mahakama Kuu kutoka nchi yoyote ya Jumuiya ya Madola.

Mnajua kwa nini? Hawa majaji watafanya uchunguzi na kumshauri Rais kabla ya kufanya uamuzi wa kumwondoa madarakani au la. Sikumbuki kama kwa Profesa Mussa Assad hili lilifanyika, pengine sikuwa nchini. Mtanikumbusha.

Lakini mjue kuwa sheria ya ukaguzi inampa mamlaka CAG kuchunguza na kufanya ukaguzi wa hesabu za maofisa masuuli wote kuhusu mapato na matumizi ya Serikali kwa niaba ya Bunge. Hivyo CAG akishafanya yake, huwasilisha bungeni taarifa na kusubiri mtanange wa walionasa.

Huyu mtu wa aina yake-CAG, hufanya ukaguzi na kutoa ripoti za Serikali Kuu, mashirika ya umma, serikali za mitaa, miradi ya maendeleo, mifumo ya TEHAMA na ufanisi.

Hatimaye hutoa hati; inayoridhisha, ambayo hii huonesha kuwa mkaguzi ameridhishwa na kuwa taarifa za fedha zinaonesha hali halisi ya taasisi liyokaguliwa kwa mujibu wa viwango na miongozo ya uandaaji taarifa za fedha.

Lakini ukisikia hati safi, haimaanishi kuwa hapana upungufu uliobainika wakati wa ukaguzi, bali uliopo ni himilivu kulinganisha na uendeshaji wa taasisi husika.

Kuhusu hali yenye shaka, inatolewa pale ambapo mkaguzi amejiridhisha kama hapo juu, lakini sasa kuna kuwa na mambo machache yenye dosari, mfano kukosekana vielelezo au nyaraka za kutisha, kuthibitisha matumizi ya fedha yanayoonekana katika taarifa.

Hiyo inamaanisha kutumia fedha za Serikali bila kufuata taratibu husika, kutumia nje ya vifungu.

Kuna pia hati ya kushindwa kutoa maoni, ambayo inatokana na mkaguzi kushindwa kupata vielelezo vya kutosha kuthibitisha kuwa taarifa ya fedha, inaonesha hali halisi ya taasisi husika. Hasa kukosekana nyaraka kwa sababu za kupotea au kuungua na sababu zingine.

Ni mengi ya CAG, yanaweza kuhatarisha maisha yake, lakini Kichere anasema haogopi kitu, haogopi mtu. Bila shaka wala ubishi, anastahili ulinzi kama tunavyoona hivi sasa, kila mtu ana mlinzi, ana msafara.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & Uchambuzi

Ruth Zaipuna: Sekta ya kibenki imeimarika maradufu miaka miwili ya Dk. Samia

Spread the loveTarehe 19 ya mwezi Machi, ni siku muhimu sana kwa...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Miaka miwili ya Rais Samia, TMA yaimarika, yatoa utabiri kwa usahihi

Spread the loveMACHI 19, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan anatamiza miaka miwili...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Zanzibar inahitaji sheria kumaliza udhalilishaji na ukatili wa kijinsia

Spread the love  DAKTARI Sikujua Omar Hamdan anaamini Zanzibar inahitaji “sheria za...

Makala & Uchambuzi

Uthubutu, uwezeshaji kielimu unavyopaisha wanawake GGML

Spread the loveMTU anapojitambulisha kuwa anafanya kazi mgodini, watu wengi hudhani kuwa...

error: Content is protected !!