MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nchini Tanzania, Charles Kichere amebaini uidhinishaji na uhakiki wa malipo ya Sh.797.2 milioni uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) bila kufuata taratibu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Ripoti hiyo ni yam waka 2020/21 inayoishia Juni 2021 ambayo leo Jumanne, tarehe 12 Aprili 2022 imewasilishwa bungeni jijini Dodoma na baadaye CAG Kichere amezungumza na waandishi wa habari.
CAG amesema Afisa Masuuli wa chama cha siasa pamoja na mambo mengine anatakiwa kuhakikisha taratibu za fedha za chama chake zinafuatwa kwa namna ambayo rasilimali za chama hicho zitalindwa.
Amesema miongozo ya taratibu za kifedha inayotumiwa na vyama vya siasa inamtaka Afisa Masuuli kupitia, kuchunguza, kukagua na kuidhinisha malipo au shughuli yoyote inayotekelezwa na Chama chake.
CAG Kichere amesema, ili kufikia lengo hilo, CCM kilianzisha Kitengo cha uhakiki, ambacho humsaidia Afisa Masuuli katika jukumu la kukagua malipo ya awali kabla ya kibali cha mwisho kutolewa.
“Pamoja na kuwa na kitengo cha uhakiki, niligundua kuwa CCM kililipa Sh. milioni 786.44 bila ya kufanyiwa ukaguzi wa awali na kuidhinishwa na Afisa Masuuli,” amesema
Aidha, amesema “nilibaini kuwa Chadema kililipa Sh. milioni 9.75 bila ya kuwa na kibali cha Afisa Masuuli.”
Amesema, kutokana na dosari hizo zilizobainika, kuna hatari ya rasilimali za vyama kutumika vibaya iwapo malipo yataendelea kufanyika mara kwa mara, bila kupata kibali kutoka kwa Maafisa Masuuli.
“Kwa maana hiyo, ninapendekeza uongozi wa CCM na Chadema kusimamia udhibiti wa ndani ili malipo yasifanyike bila ya kuwa na kibali cha Afisa Masuuli,” amesema CAG Kichere
Leave a comment