October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watano mbaroni kwa kukutwa na dawa za kulevya Uwanja wa Ndege Dar

Spread the love

WATU watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege Tanzania, kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, ACP Jeremia Shila, watuhumiwa hao wamekamatwa kati ya tarehe 17 Machi  hadi 8 Agosti 2022, katika Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Taarifa ya Kamanda Shila imesema, tukio la kwanza lilitokea tarehe 17 Machi 2022, kwenye eneo la ukaguzi wa mizigo ambapo Polisi wa  JNIA  waliwakamata watu wawili (Mtanzania na Mchina), wakiwa na kifurushi kimoja chenye chaja saba.

Ambazo sita ndani yake zilikuwa na unga mweupe wenye uzito wa gramu 234.54 wa dawa za kulevya aina ya Methamphetamine, yaliyotumwa kutoka Johannesburg Afrika Kusini, kuja mkoani Singida.

Taarifa ya Kamanda Shila, imesema mtuhumiwa mwingine ambaye ni raia wa Tanzania, alikamatwa tarehe 4 Aprili 2022,  JNIA akitokea jijini Delhi India, kupitia Adis Ababa Ethipoia, akiwa amemeza pipi mbili za dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye uzito wa gramu 34.79.

“Vilevile, mnamo tarehe 7 Aprili 2022, huko JNIA eneo la abiria wanaoondoka, Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, tulimkamata mtuhumiwa mmoja raia wa Tanzania, miaka 28, aliyekuwa akisafiri kwenda Instabul Uturuki akiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi, zenye uzito wa kilogramu 4.44, aliyaficha ndani ya begi lake mkononi,” imesema taarifa ya Kamanda Shila.

Taarifa ya Kamanda Shila imesema, Polisi JNIA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, tarehe 8 Aprili 2022, ilimkamata mtuhumiwa raia wa Italia, aliyekuwa akisafiri kwenda Paris Ufaransa kupitia Nairobi na Amsterdam kwa Shirika la Ndege la Kenya, akiwa na dawa za kulevya kilogramu 4.30 aina ya heroine, ambayo aliyaficha kwa kushonea kwenye kitako cha begi lake la nguo.

Taarifa ya Kamanda Shila imesema, jitihada za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao zinaendelea.

“Upelelezi wa kesi hizi bado unaendelea ili kuweza kubaini wanaowapa madawa hayo ya kulevya watuhumiwa waliokamatwa na vilevile wanaopelekewa,” imesema taarifa ya Kamanda Shila.

error: Content is protected !!