BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekanusha madai ya taarifa kwamba mwaka jana wabunge wamejiongezea mishahara kutoka Sh 13 milioni hadi Sh 18 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kudai katika mkutano wake wa hadhara Mjini Babati Mkoani Manyara kuwa wabunge hao wamejiongezea kiasi hicho cha mshahara.
Taarifa hiyo ya Mbowe ilisambaa katika mitandao ya kijamii kwa njia ya video na kuibua mjadala kuhusu uweledi wa wawakilishi hao wa wananchi hasa ikizingatiwa makundi mbalimbali ya watumishi wa umma wanalia mishahara kiduchu wanayolipwa na Serikali.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa leo Jumamosi na Kitengo cha Bunge cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa imesema madai hayo ni uzushi na upotoshaji .
“Hakuna Mbunge aliyeongezewa mshahara kama alivyodai. Hivyo, tunapenda kuwashauri na kuwasihi wananchi kupuuza madai hayo ambayo lengo lake ni kuleta taharuki pamoja na kuwagombanisha wananchi na wawakilishi wao.
“Nyongeza ya mshahara ni suala linalozingatia bajeti na hakuna utaratibu wa aina
yoyote kama huo ambao umefanyika kwa ajili ya kuwaongezea waheshimiwa wabunge mishahara,” imesema taarifa hiyo.
Leave a comment