December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

BBC na VOA wapigwa marufuku tena Burundi    

Spread the love

SERIKALI ya Burundi, imewapiga marufuku waandishi wa shirika la BBC na Sauti ya Marekani (VOA), kutofanya kazi nchini humo. Baraza la taifa la mawasiliano nchini humo limesema, “halitaruhusu mwandishi yeyote, akiwa raia wa Burundi ama yule wa kigeni kutoa habari yoyote kwa mashirika hayo mawili ya habari.”

Baraza hilo limeeleza kuwa mashirika hayo yametangaza habari za uongo kuhusu mauaji yaliotekelezwa na vikosi vya usalama katika nyumba ya siri ndani ya mji mkuu wa Bujumbura.

Hatua hii, inaashiria shambulio jipya kwa uhuru wa vyombo vya habari kwa kutangaza kuwa itaendelea kusimamisha vipindi vya Voice of America (VOA) na kukifutia leseni ya utangazaji kituo cha BBC nchini humo. Maamuzi haya ya kimabavu ni jaribio jingine la kuzuia ulimwengu kujua ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea Burundi.

Serikali imeishutumu VOA kwa kuendelea kumuajiri Patrick Nduwimana, Mkurugenzi wa zamani wa redio ya Bonesha FM.Nduwimana alilazimika kukimbia Burundi mnamo mwaka 2015 baada ya vituo vya redio kuharibiwa punde tu baada ya uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kuwania urais katika hali ya utata kwa kipindi cha tatu mfululizo na kusababisha uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu.

BBC inashutumiwa kuharibu jina la nchi ya Burundi, kwa kutoa waraka ulioelezea mateso na maeneo ya vificho yanayotumika kuwatesa watu nchini Burundi, na hivyo kukiuka sheria ya vyombo vya habari.

BBC na VOA, vyombo viwili muhimu nchini Burundi, zimewahi kupitia adha hii hapo awali. Wiki chache kabla ya kura ya maoni ya Katiba yaliyogubikwa utata mnamo mwezi Mei 2018, Baraza la Mawasiliano la Taifa (CNC) lilivisimamisha vyombo hivyo vya habari.

Wakati huohuo, Human Rights Watch iligundua kwamba kitengo cha Usalama wa Taifa nchini humo pamoja na umoja wa vijana wa chama tawala waliwaua, kuwabaka, kuwapiga na kuwatishia wapinzani walioshukiwa kuelekea kura ya maoni.

Lakini sasa, serikali ya Burundi imekwenda mbali zaidi, kwa kukataza mwandishi wa habari yeyote nchini humo kutokutoa taarifa kwa BBC au VOA. Ingawa bado haijawa hawazi, huenda katazo hili likawagusa hata wale waandishi wa habari wanaotoa habari kupitia mitandao ya kijamii nchini humo.

Uamuzi huu unakuja siku mbili tu baada ya kuachiwa kwa wasichana watatu wanafunzi mnamo tarehe 27 Machi 2019 ambao walifungwa gerezani mwezi huu kwa madai ya kuchora mfano wa kikaragosi cha sura ya Rais Nkurunzinza katika madaftari yao.

Kukamatwa na kufungwa kwao viliibua hisia za wengi duniani na kuhamasisha watu wengi kuchora picha za rais huyo na kuziweka kwenye mtandao ya kijamii, tukio lililotangazwa na BBC pamoja na vyombo vingine vya habari kimataifa.

Kwa miaka michache iliyopita, serikali ya Burundi imeonekana kupiga vita kukosolewa kwa nguvu zote.

Mwandishi wa habari mmoja bado hajapatikana na wengine wengi wamekimbilia uhamishoni. Kuelekea uchaguzi mkuu mwakani, hali ya sasa inatia shaka kuwa serikali ya Burundi inadhamiria kuuminya maradufu uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza nchini humo.

error: Content is protected !!