Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bashe: Mvua za El-nino zimesababisha upungufu wa sukari, tani 100,000 zimeagizwa
Habari za SiasaTangulizi

Bashe: Mvua za El-nino zimesababisha upungufu wa sukari, tani 100,000 zimeagizwa

Spread the love

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema hali uzalishaji wa sukari katika viwanda saba nchini imeshuka hadi kufikia tani 1,000 kwa siku kutokana na mvua za El-nino zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Amesema mvua hizo zimeathiri hali ya uvunaji wa miwa mashambani na kupunguza kiwango cha sukari katika  miwa kwa zaidi ya asilimia 25.


Akitoa kauli ya serikali leo Jumamosi kuhusu hali ya sukari nchini, Bashe amesema  katika kukabiliana na uhaba wa sukari ambao sasa umefikia tani 30,000, serikali imetoa kibali kwa wenye viwanda kuagiza sukari tani 100,000 ambayo inatarajiwa kuwasili nchini tarehe 23 – 24 Januari mwaka huu.

Amesema mahitaji ya sukari kwa siku nchini ni tani 1,500  na kutokana na hali hiyo bei ya rejareja ya sukari imepanda kutoka 2,700, 3000 hadi kufikia 4000.

Amesema uhaba wa sukari sasa umefikia tani 30,000 ikilinganishwa na uhaba wa tani 200,000-150,000 kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

“Uzalishaji wa sukari katika taifa kwa kipindi cha miaka mitatu uliendelea kuongezeka kiasi kwamba sugar gap kwa mwaka jana ilishuka mpaka kufika wastani wa tani 30,000 na mwaka huu tulitarajia kumaliza kabisa gap ya sukari katika Taifa letu.

“Kwamba kufikia kipindi cha msimu wa Aprili mwaka huu tungeweza kufikia uzalishaji wa tani zaidi ya 500,000. Mwaka jana tulizalisha tani 460,000 tukawa na gap ya tani 30,000 ambazo tuliagiza na tulijua kwamba tunafika mahali pa kujitosheleza.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu Sugar gap yetu imeshuka kwa wastani wa tani 150,000- 200,000 mpaka kufika tani 30,000. Hizi ni kazi kubwa ambazo zimefanywa na sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali,” amesema.

Amesema mwaka huu wamepata ‘shock’ kutokana na uzalishaji wa viwandani kushuka.

Haya hivyo amesema kutokana na hatua zilizochukuliwa anaamini ifikapo katikati ya Februari hali ya upatikanaji wa sukari itaanza kurejea katika hali ya kawaida na kutokuwa na madhara yoyote.

“Tunaamini kwamba mvua hizi zitaendelea mpaka mwezi wa Februari na Machi, tutaendelea kutoa idhini ya uagizaji wa sukari ili kuendelea kumlinda mlaji na tumeagiza bodi ya sukari kufanya kazi kwa karibu na wenye viwanda kuhakikisha stability na bei ya sukari inarudi katika hali yake,”amesema.

Pamoja na mambo mengine amewaonya wenye viwanda na wasambazaji kwamba haki ya kuwalinda aliyopewa, wakiendelea na hali ya kuficha sukari na kuongeza bei ya sukari sokoni, serikali itaiondoa haki hiyo ya kuwalinda kwa sababu hawezi kuwalinda kwa gharama ya mlaji.

“Hivyo niwaombe watanzania tutarudi kwenye hali ya kawaida katikati ya Februari, kutakuwa na sukari ya kutosha. Binafsi nimetembelea mashamba na kiwanda cha Bagamoyo nimeona uvunaji ulivyokwama. Hili ni jambo la mpito na tutarudi kwenye hali yetu ya kawaida,” amesema.

Amesema wizara ya kilimo itaendelea kufuatilia kwa karibu usambazaji wa sukari lakini pia amewaomba wakuu wa mikoa na wilaya wasisite kuangalia hali ya sukari katika maeneo yao ili watambaue kama kuna tatizo la uhaba mkubwa mahali wawasiliana na wizara ili ipeleke eneo hilo kumlinda mlaji.

Baadhi ya makazi ya watu katika Kijiji cha Kipwa mkoani Rukwa, yaliyozungukwa na maji ya mafuriko kutoka Ziwa Rukwa

Akifafanua hali ya uzalishaji viwanda Bashe amesema katika viwanda saba ambavyo kimoja cha Manyara ndio kidogo, uzalishaji upo kama ifuatavyo;

Kiwanda cha Kilombero Sugar  ambacho kilikuwa kinazalisha tani 700 kwa siku sasa kinazalisha tani 250.

Kiwanda cha TPC ambacho kilikuwa kinazalisha tani 450 kimeshuka hadi tani 180 na sasa kimepata hitilafu kubwa ya mfumo wa umeme ambayo imesababisha kiwanda kusimama.

Kagera sugar kilikuwa kinazalisha tani 500 kwa siku sasa inazalishaji tani 200-300.

Mtibwa Sugar kilikuwa kina uwezo wa kuzalisha tani 450 kwa siku sasa inazalisha tani 120.

Bagamoyo Sugar kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 160  kimeshuka hadi tani 70 na sasa kimesimamisha shughuli za uzalishaji.

Kiwanda cha serikali Mbigiri au Mkulazi kilichoanza uzalishaji karibuni kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 250 sasa kinazalisha tani 46 kwa siku.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!