Spread the love

MAKADIRIO ya Bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kwa mwaka wa fedha 2022/23, yanatarajia kutoa neema kwa wabunge, kutokana na kuongezwa kwa fedha katika Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Hayo yamebainika leo Alhamisi, tarehe 14 Aprili 2022, bungeni jijini Dodoma, baada ya Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa, kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya 2022/23.

Kwa mujibu wa makadirio hayo, bajeti ya mfuko huo imeongezeka kwa Sh. 4.99 bilioni kutoka Sh. 11.00 bilioni iliyokuwa kwenye bajeti kuanzia 2016/17 hadi 2021/22, kufikia Sh. 15.99 kwa 2022/23.

“Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, umeongezewa Sh. 4.99 bilioni kutoka Sh. 11.00 bilioni iliyokuwa katika bajeti ya kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 – 2021/22, hadi Sh. 15.99 bilioni, kwa mwaka wa fedha 2022/23. Sawa na ongezeko la asilimia 45.36, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi,” amesema Bashungwa.

Mbali na ongezeko la bajeti ya mfuko wa jimbo, wizara hiyo imetenga Sh. 607.57 milioni kwa ajili ya kuchangia mchango wa mwajiri katika bima ya fya, kwa madiwani.

“Serikali ilianza kulipa posho za madiwani kwa 2021/22, ambapo mchango wa bima ya afya haukujumuishwa kwenye posho hizo. Kwa 2022/23, Serikali imetenga fedha ya kuchangia mchango wa mwajiri kwa ajili ya madiwani, Sh. 607.57 milioni,” amesema Bashungwa.

Katika hatua nyingine, Bashungwa amesema mikoa imeongezewa fedha za uendeshaji vikao vya kamati za usalama za mikoa kwa Sh. 364 milioni, kutoka Sh, 416.00 milioni hadi Sh. 780.00 milioni.

“Mikoa 12 inayopakana na nchi jirani imetengewa jumla ya Shilingi milioni 730.00 kwa ajili ya kuimarisha usalama mipakani,” amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema, ofisi za wakuu wa wilaya, zimeongezewa fedha za matumizi mengineyo, kutoka Sh. 17.13 bilioni, hadi Sh. 26.68 bilioni, sawa na ongezeko la Sh. 9.55 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *