ASKOFU wa Kanisa la Baptist Kanda ya Kati, Anthony Mlyashimba ametoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kukubali kuufumua mkataba wa uwekezaji wa bandari kwa kuwa unaligawa Taifa. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma… (endelea).
Askofu Mlyashimba ametoa wito huo leo Jumapili tarehe 23 Julai 2023 wakati wa ibada maalumu ya kuliombea Taifa iliyofanyika katika kanisa la Nzuguni Baptist City lililopo Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema kuwa kwa sasa taifa limegawanyika kutokana na kuwepo kwa mkataba huo ambao umesababisha taharuki kubwa kwenye jamii.
Amesema ni busara kwa viongozi kuhakikisha mkataba huo unasitishwa mara moja ili kutafuta ufumbuzi ambao utafanya kuwepo kwa umoja, amani, mshikamano na upendo tofauti na ilivyo sasa.
“Kwa sasa nchi imekuwa na pande mbili na kuna watu ambao wanasema bandari imebinafsishwa na wengine wanasema imeuzwa, kumesababisha kuwepo kwa mpasuko ambao unaweza kusababisha makubwa.
“Kwa kuzingatia maneno ya Mungu yanasema katika kitabu cha Zaburi 133 mstari wa kwanza; “Tazama ilivyo vyema na kupendeza ndugu wakae pamoja kwa umoja” kwa hiyo kuna mambo mawili ya kukaa pamoja na umoja lakini mnaweza kukaa pamoja na msiwe na umoja,” amesema.
Aidha, amesema kuna haja ya kuwatafuta wabobezi wa sheria za mikataba na kueleza umma ukweli.
Ameeleza kushangazwa na ukimya wa Prof Paramagamba Kabudu na George Simbachawene ambao ni watalaam wa sharia ndani ya Serikali.
Amesema kusitisha mkataba huo ni afya kwa taifa na kuendelea kushupaza shingo ni kulifanya taifa kuingia katika giza neno ambalo litasababisha matatizo katika kizazi kijacho pamoja na vijukuu kutokana na hali hiyo mkataba uondolewe.
Leave a comment