Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, imemkamata Michael George Clement, mkazi wa Ndala Manispaa ya Shinyanga kwa tuhuma za kuhujumu miondombinu na kuiba maji kinyume cha sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu…(Shinyanga).
Clement alikamatwa usiku wa tarehe 3 Septemba 2023 kutokana na uchunguzi uliofanywa na timu ya SHUWASA kwa kushirikiana na wasamaria wema.

Ni baada ya kutilia shaka matumizi yake ya maji kutoendana na kiasi cha ankara za mwezi.
Akizunguumza na waandishi wa habari mara baadaya tukio hilo, Afisa Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa SHUWASA, Nsianel Gerald, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anaiba na kuuza maji kinyume cha taratibu na pasipo kibali cha biashara ya maji.
“Tulianza kutilia shaka matumizi yake ya mwezi (bill) baada ya kuonekana ni ndogo ikilinganishwa na biashara ya kuuza maji ambayo nayo alikuwa akiifanya kinyume cha taratibu,” alisema Nsianeli na kuongeza;
“Pamoja na kuuza maji lakini bili yake haikuwahi kuzidi Sh 6,000 kwa mwezi kwa kipindi cha miaka minne na ndipo tukaanza kumfuatilia na kumchunguza na hatimaye usiku wa tarehe 3 Septemba, 2023 tukabaini amechepusha maji kabla ya dira ya maji,” alisema.
Clement anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa taratibu zaidi za kisheria.
Akifafanua kuhusu utaratibu wa kuuza maji alisema, usajili wao ni tofauti na watumiaji wa majumbani na bei zao za maji ni tofauti.
“Mteja wa majumbani hapaswi kuuza maji na kama mtu anataka kuuza maji anapaswa kusajiliwa kama gati la kuuzia maji na bei za maji zinakuwa tofauti,” alisema Gerald.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuacha kuhujumu miundombinu ya maji na kuiba maji kwani ni kosa kisheria na adhabu yake ni faini kuanzia Sh. 500,000 hadi Sh Milioni 50 na/au kifungo jela.
Pia aliwasihi wananchi kutoa ushirikiano kwa timu ya SHUWASA kwa kuripoti watu wanaowatilia shaka kuwa ni wezi wa maji ili kuweza kuwafuatilia na uchunguzi na kuwakamata.
Leave a comment