Friday , 3 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Ajali Tanga- RC awakomalia madaktari waliosimamishwa, aibua shangwe miili ikiagwa
Habari Mchanganyiko

Ajali Tanga- RC awakomalia madaktari waliosimamishwa, aibua shangwe miili ikiagwa

Spread the love

MKUU wa mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amesema Serikali haikumsimamisha Mganga Mfawidhi Halmashauri ya Mji Korogwe na daktari mteule wa hospitali ya wilaya hiyo kwa kutokwenda kwenye eneo la ajali, bali imewasimamisha kwa sababu ya kutofika kwenye kituo chao cha kazi.

Amesema licha ya watu kusema wasamehewe, wengine kudai wameonewa, Serikali ipo tayari kuonea watumishi wa aina hiyo kwani uzembe waliouonesha hauvumiliki kamwe. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Mgumba ametoa kauli hiyo leo tarehe 5 Februari 2023 wakati akizungumza katika ibada ya kuaga miili ya watu 19 kati ya 20 waliofariki kwenye ajali iliyotokea juzi usiku maeneo ya Korogwe mkoani Tanga.

Kutokana na madaktari hao kuchelewa kufika katika kituo chao cha kazi ambacho ni Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, jana Mgumba alitangaza kuunda kama kuchunguza madaktari wa wilaya hiyo pamoja na kuwasimamisha wawili hao kwa muda wa siku 14 ili kupisha uchunguzi.

Amesema madaktari hao wote wanaishi umbali usiozidi mita tano kutoka katika hospitali hiyo lakini cha ajabu licha ya kupigiwa simu mara kadhaa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Calist Lazaro muda wa saa saba usiku, walimjibu taarifa za ajali hiyo wanazo kisha wakaja kwenye kituo cha kazi saa 11 alfajiri.

“Mkuu wa wilaya anaishi kilomita 70, alitoka Lushoto akafika eneo la ajali, lakini madaktari hawa wamefika hapa hospitali saa 11 asubuhi.

Amesema Kamati ya ulinzi na usalama inayojumuisha Kamanda wa usalama barabarani na Kamanda wa polisi wa mkoa huo, kuwa wanaishi kilomita 100 kutoka kwenye eneo la ajali, walifika eneo hilo na kufanya uokozi lakini walipofika hospitali madaktari hao hawakuwepo.

“Mimi nimepata taarifa ya kwanza kutoka kwa DC amenipigia saa 10:11 usiku, nikaamka. RPC amenipigia saa 10:29 usiku baada ya hapo nikawapa taarifa crew yote ya mkoa. Tukaenda Bombo maana DC aliniambia imemlazimu kutoa rufaa waletwe Bombo kwa sababu madaktari wa wilaya hawajafika.

“Kwenye hili kama mwakilishi wa rais, hata ningebaki peka yangu bado tungeendelea kuchukua hatua kwa watumishi hawa, kwanza tangu jana nimeagiza waandikie maelezo kwamba kwanini hawakufika kwenye kituo chao cha kazi lakini mpaka sasa sijapata maelezo yao. Nimewapa siku 14 wakae pembeni kupisha uchunguzi, baada ya taarifa hiyo ya uchunguzi tutajua nini cha kufanya,” amesema Mgumba na kushangiliwa na waombolezaji katika ibada hiyo.

Awali mwakilishi wa familia alitoa shukrani kwa wanafunzi wanaosomea uuguzi katika chuo cha Korogwe kwa kuwapatia msaada kwenye hospitali hiyo ya wilaya na eneo la ajali jambo ambalo Mgumba amesema hiyo ilithibitisha uzembe wa madaktari hao.

“Marehemu waliokufa eneo la tukio ni wanane, waliobaki wote wamefia hapa hosptali ya wilaya ya Korogwe. Mnasema tuwasamehe, madaraka mabaya! mtuhukumu ila hatuwezi kurudi nyuma katika kutetea uhai wa watanzania wenzetu,”amesema.

Aidha, ametoa wito watumishi wa Serikali kutumia viapo vyao vizuri kutumikia Watanzania kwani haitakuwa na maana kwa serikali kuboresha miundombinu ilihali watumishi hawaheshimu viapo vyao.

Pia ametoa wito kwa Jeshi la polisi kugeukia udhibiti mwendo kwa malori na magari ya mizigo yanayotembea usiku kwa sababu sasa wamefanikiwa kwenye mabasi yanayotembea mchana.

Ajali hiyo ilitokea tarehe 3 Februari 2023 muda wa saa 4:30 usiku, eneo la Magila Gereza, katika barabara ya Segera – Buiko, ilihusisha gari aina ya Fuso na basi dogo aina ya Toyota Coaster, iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Basi hilo, lililokuwa na abiria 26, lilikuwa limebeba mwili wa Athanas Cosmass Mrema, aliyefariki dunia katika hospitali ya Bochi – iliyopo Kwa Msuguri katika Kata ya Saranga – Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

Habari MchanganyikoKimataifa

Ruto amteua Kahariri kuwa mkuu wa majeshi

Spread the loveRAIS wa Kenya, William Ruto, amemteua Jenerali Charles Muriu Kahariri,...

Habari Mchanganyiko

Chongolo aonya viongozi vijiji kutouza NIDA kwa wageni

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amewaonya viongozi wa...

error: Content is protected !!