November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo yalia na uvamizi wa tembo, migogoro ya wakulima

Spread the love


CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeomba Serikali ichukue hatua za haraka kutatua changamoto za uvamizi wa wanyama katika makazi  na mashamba ya wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za wanyamapori. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tunduru … (endelea).

Akizungumza katika ziara yake ya kichama, iliyofanyika leo Jumatatu, tarehe 3 Oktoba 2022, Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema kuna wimbi kubwa la Tembo wanaotoka mbuga ya Selous, kuvamia maeneo ya wananchi.

“Mwaka huu nimefanya ziara katika maeneo yanayozunguka Mbuga ya Selous. Kuna wimbi kubwa sana la tembo wanaotoka mbugani na kuvamia mashamba na vijiji hasa kwenye mikoa ya Lindi na Ruvuma.Hapa Tunduru kwa mfano, tembo wanavamia vijijini mara kwa mara, kuharibu mazao ya wakulima, kujeruhi na kuua watu,” amesema Shaibu.

Shaibu ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, ifanye utafiti wa kina kubaini chanzo cha matukio hayo ili kuyatafutia ufumbuzi.

“Hali hii haikubaliki. Ni lazima Serikali iwajibike. Mosi, ni lazima Wizara ya Maliasili na Utalii ifanye utafiti wa kina kubaini chanzo cha kuongezeka kwa matukio ya tembo wengi kukimbia maeneo ya mbugani na kuvamia vijiji katika miaka ya hivi karibuni,” amesema Shaibu.

Shaibu amesema “pili, ni lazima Serikali iimarishe Idara ya Wanyamapori kuwezesha uwepo wa Askari wanyamapori wa kutosha kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi. Tatu, ni lazima wananchi wapewe mbinu na uwezo na kujihami na pale mazao yao yanapoharibiwa, wapewe fidia ya kutosha na ya mapema.”

Katika hatua nyingine, Shaibu kupitia ziara yake aliyoifanya jana Jumapili, wilayani humo, aliiomba Serikali kuchukua hatua kukomesha migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima, yanayosababisha baadhi ya wananchi kujeruhiwa na hata kupoteza maisha.

“Hivi karibuni nilifanya ziara Mkoani Lindi. Karibu kila Kata niliyokwenda hasa Wilaya ya Kilwa, nilikuta visa vya mapigano ya wakulima na wafugaji ambapo watu wengi wamejeruhiwa na kuuawa,” amesema Shaibu na kuongeza:

“Hali hiyo ilinitisha sana nikaomba kuonana na Waziri Mkuu. Ninashukuru alinikubalia tukakaa chini na kuzungumza. Nilimweleza Mh. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kama hatua za upesi hazitachuliwa, mapigano yatasambaa maeneo mengi na kuhatarisha usalama nchini.”

error: Content is protected !!