Wednesday , 8 May 2024
Home Kitengo Biashara NMB yafuturisha Unguja, Pemba, SMZ yaahidi ushirikiano
BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yafuturisha Unguja, Pemba, SMZ yaahidi ushirikiano

Spread the love

BENKI ya NMB imeendeleza utamaduni wa kufuturisha wateja wake walioko kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, baada ya kufanya hafla mbili tofauti za Iftar katika visiwa vya Unguja na Pemba, ambako mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hemed Suleiman Abdulla. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Makamu wa Pili wa Rais, alihudhuria hafla iliyofanyika Alhamisi, mjini Unguja, ambako NMB iliongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wake, Ruth Zaipuna, na Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk. Edwin Mhede, huku Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahoro Masoud, akiiwakilisha SMZ katika Iftar ya Pemba.

Katika hafla hizo mbili, NMB imewafuturisha takribani waalikwa 1,000, wakiwemo wateja, wadau viongozi wa SMZ, pamoja na watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu, kati yao waalikwa karibu 600 wakihudhuria hafla ya Unguja na wengine wapatao 400 wakijumuika pamoja Kisiwani Pemba.

Mjini Unguja, Makamu wa Pili wa Rais, alisema SMZ inaipongeza NMB kwa kudumisha utamaduni huo, na kwamba inatambua na kuthamini mchango wa taasisi hiyo katika maendeleo visiwani humo, huku akisema siri ya mafanikio ya ongezeko la mapato Zanzibar ni ushirikiano wa kimfumo baina ya benki hiyo na Serikali yake.

“Tunaishukuru Menejimenti ya NMB kwa kulifanya tukio hili la Iftar kuwa endelevu, mmekuwa mkifanya hivi kwa muda mrefu, naamini huu ni muendelzeo wa kaulimbiu yenu ya ‘Karibu Yako’ kwa kuwa karibu na wateja wenu, kuwa karibu na wananchi ili kuwashawishi wale ambao hawajajiunga nanyi, kufanya hivyo.

“Niwahakikishie kwamba tutaendelea kuimarisha mifumo kupitia NMB, kwani naelewa kuwa kuna kazi kubwa sana za SMZ mmezifanya na zimetusaidia sana na hapa nikiri kwamba, ongezekola makusanyo ya Mapato ya Serikali ya Zanzibar, moja ya siri za mafanikio hayo ni mchango wa NMB,” alisema.

Aliongeza kwa kutoa ahadi, akisema SMZ itaendelea kuwapa NMB ushirikiano na kuwa pamoja nao katika hali zote, ili kuhakikisha benki hiyo inafanya kazi zake kwa ufanisi na kwamba imani ya Serikali yake ni kuwa wateja waliohudhuria Iftar na wale ambao hawakupata fursa hiyo, wanaendelea kuheshimu na kuthamini huduma zao.

Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abullah (mwenye koti jeusi) akikabidhi msaada wa vyakula kwaajili ya Futari kwa watoto waishio katika Mazingira magumu uliotolewa na Benki ya NMB wakati wa Ibada maalum ya Futari iliyoandaliwa na Benki hiyo Visiwani Zanzibar. Kushoto ni Meneja wa Biashara za Zanzibar wa Benki ya NMB, Naima Said Shaame, wapili kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, kulia na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede na wengine ni watoto kutoka vituo vililivyopokea msaada huo.

Ukiondoa Makamu wa Pili wa Rais hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mawaziri, wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakiwemo Waziri wa Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo Zanzibar, Shamata Shaame Khamis.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Zaipuna alikiri kuwa kusanyiko hilo ni faraja kubwa kwa NMB kujumuika pamoja na wananchi wa Zanzibar, hususani wateja wa benki yake walio kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wadau na viongozi wa Serikali.

“Tunaamini kwamba katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani, ni wakati sahihi na mzuri wa sisi sote kutafakari juu ya maadili yanayotuunganisha binadamu wote, upendo kwa familia zetu, shukrani kwa Mwenyezi Mungu, lakini pia toba na kuzidisha ushirikiano katika ibada.

“Pamoja na kuwaalika wateja wetu, viongozi na wadau mbalimbali, leo pia NMB imetumia fursa hii kujumuika na watoto kutoka katika vituo vya yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu, ambao wameungana nasi na tuko pamoja nao hapa katika futari hii, lakini watapokea misaada mbalimbali,” alibainisha Zaipuna.

Akaongeza ya kwamba NMB inaamini kuwa uwepo wa Watoto hao ni fursa ya wao kujifunza na kuendelea kuhamasika katika kutenda mema na kuwa wakarimu kwa jamii, huku akiwaombea kukua katika imani, wamtegemee Mungu na wazidishe juhudi katika kila kitu wanachokifanya, ikiwemo masomo.

Meneja Mwandamizi wa idara ya Wateja Binafsi NMB, Ally Ngingite, ndiye aliyeongoza jopo la viongozi wa benki hiyo katika Hafla ya Iftar ya Pemba, ambaye alimuahidi mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahoro Masoud kuwa benki yake itadumisha utaratibu huo wa kuitenga siku moja ya kujumuika nao.

“Huu ni utamaduni endelevu, NMB inaahidi kuudumisha katika vipindi vijavyo vya ibada hii, ambayo ni moja kati ya Nguzo Tano za Kiislamu. Wito wetu kwa Waislamu Tanzania, nao wadumisha wema huu na utekelezaji wa ibada wanaoufanya katika Mwezi Mtukufu, huku tukiwatakia kheir katika siku zilizobaki,” alisema Ngingite.

Naye RC Mattar Zahoro, aliishukuru NMB kwa kuratibu hafla hiyo inayolenga kurejesha kwa jamii, program ambayo benki hiyo imejipambanua kwa kufanya makubwa katika sekta za elimu, afya na kilimo, huku akiwataka Waislamu kukimbilia ibada zote zinazofungamana na Ramadhani katika siku zilizosalia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

error: Content is protected !!