Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Tanzania yapandishwa uwezo wake wa kukopa Kimataifa
Habari Mchanganyiko

Tanzania yapandishwa uwezo wake wa kukopa Kimataifa

Rais Samia Suluhu Hassan
Spread the love

 

TANZANIA imepandishwa kwenye orodha ya kimataifa ya viwango vya nchi vya kukopa kutokana na kuimarika kwa uchumi wake ndani ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kukadiria uwezo wa mataifa wa kuchukua mikopo liitwalo Moody’s.

Sababu kubwa iliyotajwa kwa Tanzania kupanda hadi kiwango cha B1 kutoka B2 ni uchumi himilivu, mageuzi chanya yanayofanywa na Serikali ya Rais Samia na ongezeko kubwa la uwekezaji wa ndani na nje.

Kwa mujibu wa Moody’s, Tanzania sasa iko kwenye kiwango cha B1 (stable outlook), kutoka kiwango cha B2 (positive outlook).

Maana ya Tanzania kupanga viwango hivyo ni kuwa Serikali inaweza kukopa mikopo ya kimataifa kwa riba nafuu zaidi kwani uchumi wake unaonekana kuwa himilivu na Serikali inaweza kulipa deni lake.

Kwa sasa Tanzania ina kiwango cha juu zaidi cha kukopesheka kwa nchi zote za Afrika Mashariki, ikiwa juu ya Kenya (B3 negative), Uganda (B2 negative) na Rwanda (B2 stable).

Kiwango hicho kizuri cha Tanzania pia kitasaidia kuchochea wawekezaji kutoka nje wazidi kuja nchini kwani wanakuwa na uhakika wa utulivu wa uchumi.

Moody’s imesema katika taarifa yake jana kuwa uamuzi wa kuipandisha Tanzania kiwango cha ukopeshaji unatokana pia na ukuaji imara wa uchumi na deni la taifa ambalo ni himilivu.

“Kupandishwa kwa kiwango cha Tanzania hadi B1 kunaashiria rekodi nzuri ya uhimilivu wa uchumi wake miaka hii ya karibuni licha ya misukosuko kadhaa duniani na hivyo kujenga imani kuwa uchumi wake una uwezo wa kukabiliana na changamoto zozote siku zijazo,” Moody’s wamesema.

Kwa mujibu wa Moody’s, uchumi wa Tanzania umekuwa kwa kasi kubwa ya wastani wa asilimia 6 kwa mwaka kati ya mwaka 2015 hadi 2022, ukiongozwa na sekta za kilimo, utalii, madini na ujenzi.

Ongezeko la mauzo ya nje ya bidhaa na huduma, deni la taifa himilivu na sera madhubuti za fedha zimechangia Tanzania kupandishwa kiwango hadi B1, taasisi hiyo imesisitiza.

Moody’s imesema kuwa mageuzi ya kiuchumi yameshika kasi chini ya uongozi wa Rais Samia, ikiwemo kujenga taasisi imara.

Taasisi hiyo imesema kuwa Tanzania inapaswa kuendelea na mageuzi ya kiuchumi kama inataka kupanda zaidi kwenye kiwango chake cha kukopesheka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

error: Content is protected !!