Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Miaka 28 watumishi UDSM yaliwa na nzige, madumadu
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 28 watumishi UDSM yaliwa na nzige, madumadu

Spread the love

GEORGE Francis anasikitika; anatembea akiwa na mawazo mengi, hajui la kufanya. Kinachomfanya awe katika hali hiyo ni baada ya kujikuta miaka 18 aliyotumika kama mnadhifu au mtunza usafi katika idara ya mahesabu kitivo cha Sayansi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) imeliwa na nzige. Anaripoti Regina Mkonde… (endelea).

Baada ya miaka mitatu alipanda cheo kuwa msaidizi wa ofisi daraja la II. Baadaye alipandishwa cheo na kuwa afisa msimamizi kisha akabadilishiwa kazi akawa mtunza nyaraka za uhasibu na bohari hadi alipostaafishwa.

Hivi sasa George yuko nyumbani, anakumbuka miaka miwili aliyofanya kazi UDSM kama kibarua na miaka mingine 16 kama mwajiriwa kuanzia mwaka 1981 hadi 1996. Kanisani ndiko kuliko na faraja. “Nitawarudishia miaka ile iliyoliwa na nzige, kila kitu kilicholiwa na tunutu, parare na matumatu, hilo jeshi kubwa nililowaletea!” asema BWANA (Yoeli 2:25).

George ni mmoja wa waliokuwa watumishi 638 wa UDSM, walioombwa kustaafu kwa hiari mwaka 1996. Tangu mwaka huo hadi leo, wanahangaikia mafao yao yaliyosalia kati ya Sh. 1.7 bilioni walizopaswa kulipwa, kwa muda wa miaka 28 sasa.

Watumishi hao hawajafika Ikulu tu, lakini ofisi zote za chini zinazohusika na mgogoro wao wa mafao wamefika bila mafanikio. Sasa wanaomba MwanaHALISI ipaze sauti ili kilio chao kifike kwa mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan.

Hatua yao ya kuomba msaada wa vyombo vya habari ni baada ya UDSM kutoonesha nia ya kuwalipa madai yao, licha ya Wizara ya Utumishi pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuiagiza taasisi hiyo ya elimu ya juu kuwalipa madai yao.

Profesa William Anangisye

“Wahadhiri hawakuwepo hata mmoja hamna,  sana sana ma-admin wachache ,  wale wa usafi  na sekta ndogo ndogo  na wasaidizi wa ofisi na watu wa mabomba. Tumeguswa sisi watu wa chini wahadhiri hawakuwepo ndio maana tukaonewa kwa sababu sio wasomi kama wao wakaona watuondoe. Lakini wao wasomi hawajaguswa hata mmoja na hela zetu wamezichukua kama walituondoa basi wangeutupa hela zetu, lakini wakazitamani wakazichukua,” alisema George.

Kwa mujibu wa wastaafua hao wakati wanastaafu kwa hiari walikubaliana walipwe fidia ya kiasi cha Sh. 1.7 bilioni fedha za wakati huo na kwamba walilipwa nusu mwaka 1996 na kusalia Sh. 488.9 milioni ambazo kwa thamani ya sasa wanadai ni zaidi ya Sh.1 bilioni.

“Wakati tunastaafishwa mwaka 1996 tuliweka makubaliano ya kulipwa fidia na stahiki mbalimbali ikiwemo mshahara wa mwezi mmoja baada ya kustaafu ambapo kwa wafanyakazi wote ilikuwa Sh. 19.7 milioni. Fedha za mishahara ya miezi 40 baada ya kustaafu kazi ni kiasi cha Sh. 757.07 mmilioni na fedha za usafiri Sh. 208.12 milioni. Hizo fedha zote tulilipwa ambazo ni kati ya Sh. 1.7 bilioni ya mafao yote,” alidai George.

George alisema “lakini kuna pesa ambazo hatujalipwa tunazisotea kwa miaka 28 sasa za michango yetu ya PPF kiasi cha Sh. 167.56 milioni, hizi hazikulipwa licha ya UDSM kukabidhiwa na PPF ili watulipe.”

Wanadai kuwa kinachofanya wasilipwe stahiki zao licha ya wizara ya utumishi kuelekeza walipwe ni uongozi wa UDSM. Kuna madai kwamba fedha hizo zilitolewa na hazina muda mrefu ili walipwe lakini zililiwa na baadhi ya viongozi waliokuwepo wakati suala lao limetokea.

Mwaka 2002 walikwenda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa ajili ya kushtaki lakini hawakupata haki yao. Mwaka 2004 walikwenda iliyokuwa Wizara ya Elimu kudai haki yao ambayo iliuagiza uongozi wa chuo hicho kuwalipa fedha zao, lakini hawakulipwa.

“Wakati tunahangaika kuitafuta haki yetu, kuna kiongozi mmoja wa UDSM wakati huo alidai hata tukienda mbinguni kuidai haki yetu hatuwezi kuipata, hiyo kauli ilitushtua sana tukaja kujua jeuri hiyo inatoka wapi,” alisema George.

Mwaka 2018 walijikusanya tena na kufunga safari hadi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili ifanye uchunguzi kujua hatima ya fedha zao. Mwaka 2020 taasisi hiyo ilitoa majibu yaliyoonesha kwamba mafao yao yote yalitolewa, lakini baadhi yake yalitafunwa na baadhi ya waliokuwa vigogo wa UDSM. Takukuru haikutoa msaada zaidi.

Baada ya Takukuru kutoa ripoti ya uchunguzi huo,  Julai 2022 walikwenda Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira kujua hatma ya haki zao. Huku walipewa barua iliyowaelekeza waende Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambao waliiandikia barua UDSM kuielekeza kulipa fedha hizo, lakini chuo hiko hakikufanyia kazi.

“Hadi tunakuja hapa MwanaHALISI tumeshazunguka sana na inachoonekana UDSM haitaki tulipwe fedha zetu, sababu licha ya kupewa barua za maelekezo na wizara hizo bado ilipuuza kufanyia kazi na hata tulipokwenda kuzungumza na Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. William Anangisye, naye hakutusikiliza,” alidai George.

Sasa watumishi hao wameamua kumwangukia Rais Samia Suluhu Hassan wakimuomba aingilie kati wapate haki zao, kwa kuwa baadhi yao wamekufa huku hawajalipwa stahiki zao, lakini umoja wao bado una orodha ya warithi wao ambao watalipwa kama fedha hizo zitatoka.

MwanaHALISI lilipozungumza hivi karibuni na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa UDSM, Asha Aeshi, alidai wastaafu hao hawadai kitu kwani stahiki zao walipewa kulingana na mikataba yao ya kustaafishwa kazi ambayo waliiridhia 1996.

Asha alisema, sakata hilo limeibuka tena kwa kuwa wastaafu hao wanadai vitu ambavyo havipo katika mkataba wao wa kustaafishwa kazi na kwamba kama wanaona wana haki waende mahakamani kudai haki yao badala ya kwenda katika vyombo vya habari.

“Wanasema kwamba walienda Wizara ya Utumishi na Wizara ya Fedha kudai haki zao, lakini hakuna mamlaka yoyote imeelekeza walipwe. Tumejitahidi kukaa nao mezani kuwaelewesha lakini jitihada hazikuzaa matunda. Walishawahi kwenda mahakamani, mahakama ikaamua kwamba hawadai chochote na kama hawajaridhika wakate rufaa lakini hadi leo hawajakata rufaa,” alisema Asha.

Anasema kuwa “hizo fedha wanazodai walishalipwa wanavyodai ni vitu ambavyo havipo kwenye mkataba lakini vilivyopo katika mkataba vyote walilipwa na kama ni wakweli waambie wakuonyeshe mkataba wa kustaafishwa uone kama hivyo wanavyolalamikiwa vipo. Hatuwezi lipa vitu ambavyo viko nje ya mkataba.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!