Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Nimekumbuka Samia wa miaka 3 iliyopita
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nimekumbuka Samia wa miaka 3 iliyopita

Spread the love

WAKATI naandaa makala ya safu hii wiki hii, nimejikuta nakumbuka kuwa leo (19 Machi 2023), ni miaka mitatu kamili tangu Rais Samia Suluhu Hassan aape na kukabidhiwa uongozi wa taifa letu.

Nchi ilikuwa katika majonzi makubwa na mwili wa rais kipenzi cha Watanzania, John Pombe Magufuli, ulikuwa chumba cha maiti kule hospitali ya jeshi ya Lugalo.

Kwanza, nampongeza Rais Samia kwa kutimiza miaka mitatu ndani ya Ikulu yetu. Kwamba, tangu aingie madarakani, tarehe 19 Machi 2021, serikali ya Rais Samia, imefanya mambo ambayo yanaweza kufanyiwa tathmini na kuonesha mwelekeo wake katika nyanja mbalimbali, ikiwemo demokrasia na utawala bora.

Aliyoyafanya katika nyanja ya demokrasia na utawala bora, yanaweza kutumika kama kipimo cha kuweza au kushindwa kutimiza yale aliyoahidi mara baada ya kuapishwa.

Katika hotuba yake ya kulihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, Rais Samia aliahidi Serikali yake kuendelaza mazuri ya mtangulizi wake na kuanzisha yake mapya yanayolenga kuleta umoja wa kitaifa na kuponya majeraha.

Lakini pili nakiri wazi kwamba Samia yule siyo huyu wa sasa. Yule alijiona ni rais wa mpito na huyu anajiona ni rais wa kudumu. Aliyoyosema wakati ule, anaweza kuwa anayajutia hivi sasa. Samia yule akikutana na Samia huyu wanaweza kupigana na kuumizana.

Mwandishi nguli ninayependa kusoma makala zake katika taifa hili, Askofu Dk. Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), huko Karagwe, aliandika makala ya ushauri kwa rais Samia.

Nimeirudia mara nyingi na leo naona niitumie katika makala yangu ya wiki. Kilichoandikwa kimeandikwa, na ninaona maoni ya Askofu huyu yana nguvu kubwa hadi leo. Yanalifanya taifa lijione bado liko msibani.

MAADILI YA KUONGOZA MPITO (Transitional Management).

Rais wetu ameishaapa. Tunaye Rais mpya Ikulu. Nampongeza sana na kumtakia heri katika jukumu zito lenye hukumu alilotwishwa na Katiba.

Wosia wangu kwake ni kumshauri aiogope na kutetemeka nafasi hiyo kama sisi raia tunavyomuogopa na kumtetemekea mtu aitwaye Rais.

Kiongozi mkuu wa Nchi asiyeuogopa urais, ni hatari kwa nchi na kwake mwenyewe binafsi. Rais asiyeuogopa urais lakini anataka aogopwe, ni hatari na msiba usiokwisha kwa taifa lolote. Sasa tuyatazame baadhi ya maadili ya kipindi cha mpito.

Samia Suluhu Hassan, Tanzania’s president, during an interview at Chamwino State House in Dodoma, Tanzania, on Monday, March 28, 2022. The second phase of negotiations with a group of companies led by Equinor ASA and Shell Plc for building the long-delayed LNG terminal are expected to conclude by June, Hassan said in an interview in her office on Monday. Photographer: Neema Irene Ngelime/Bloomberg

Mh Rais amesema huu ni wakati wa “Kuzika tofauti zetu.” Kazi hii hufanyika vema endapo haya yatazingatiwa:

  • Kutohamisha viapo kwa karatasi. Wateule-Kiini waliopo waweke viapo vipya vya UTII kwa Rais mpya Samia.
  • Kwa umakini wa kutosha, wateule wenye hulka-mpasuko (zealots) wabadilishiwe majukumu. Taifa linahitaji kupona na kuzika tofauti.
  • Bila kuathiri katiba wala kuingilia Uhuru wa mihimili mingine, Rais Samiah kama Mkuu wa nchi aelekeze kuondoa mipasuko katika vyombo vingine. Taifa linahitaji kupangusana machozi.
  • Toka kale, mwaka mpya, Mfalme mpya na Sikukuu ya kitaifa, huja na habari njema kwa wananchi. Rais afungue box la zawadi kwa makundi mbalimbali yaliyonuna na kushika tama kwa sababu yoyote ile. Makundi hayo yapate tabasamu mbele ya mwezi mwandamo. Taifa letu limevimba na kununa, linahitaji mshikamano.
  • Wateule wenye hulka na rekodi ya kukanyaga sheria na Katiba kwa kisingizio cha uzalendo wapumzishwe kwa heshima. Hawa ni hatari kwa Rais kuliko walivyo hatari kwa nchi. Rais wetu aimbe wimbo wa Haki tu, Kazi tutafanya na Taifa litainuka.

Kanuni kuu nyuma ya mapendekezo haya ni ukweli kuwa: Yawezekana wapo wasiopenda kuendelea kumsaidia Rais mpya, waruhusiwe kwa heshima.

Yawezekana wapo wasiopenda maridhiano ya kitaifa, wapumzike kwa heshima.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan

Yawezekana wapo wanaopenda kumtumikia rais kuliko kulitumikia Taifa, wajue Rais na Taifa haviachani.

Yawezekana wapo wanaopenda kutumikia vyama vyao kuliko Taifa lililoshikamana, wajue vyama hupita Taifa hubaki.

Yawezekana wapo wanaoishi kwa kutegemea Rais anavyowategemea wao kuliko anavyoitegemea katiba. Kazi ya kushauri itenganishwe na tumbo.

Kwa ajili hiyo ni muhimu kwa Rais kufanya mabadiliko ya haraka ili kutekeleza mambo matano aliyoyaahidi katika hotuba yake fupi yaani, Kuzika tofauti, bila kutazama nyuma, kushikamana, Kufuta machozi na kusonga mbele.

Mwisho, Rais yeyote mpya huingia Ikulu akiwa na hati safi hata kama alikuwa katika safu iliyopita. Rais Samia kwa sasa ana hati safi. Tumsaidie abakie msafi hadi anaondoka madarakani.

Wasaidizi wake wajaliwe hekima ya kutunza na kuhifadhi usafi wa Rais. Njia moja ya rais kutunza usafi wake, ni kukataa uwongo anaoambiwa na wasaidizi wake hata kama ni uwongo mdogo wa kuepusha rabsha fulani.

Mdomo wa Rais huifadhi kweli hata kama kwa kufanya hivyo, serikali yake itaaibika kwa muda. Ukweli huweka huru. Mungu Ambariki Sana Rais wetu.

Mwandishi wa Makala haya ni Kondo Tutindaga… (endelea).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Samia awataka watanzania kudumisha muungano

Spread the loveRais wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendeleza Muungano kwa...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

error: Content is protected !!