Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kifo cha Magufuli: Mabeyo ‘akaanga’ wenzake
Habari za SiasaTangulizi

Kifo cha Magufuli: Mabeyo ‘akaanga’ wenzake

Spread the love

NANI aliyetaka kupindisha Katiba, ili aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, asiapishwe kurithi kiti cha urais baada ya John Magufuli, kufariki dunia, jioni ya 17 Machi 2021, jijini Dar es Salaam? Anaripoti Saed Kubenea … (endelea).

Aliyekuwa mkuu wa majeshi nchini (CDF), Jenerali Venance Mabeyo, ndiye aliyerejesha swali hili vichwani mwa wananchi, kufuatia mahojiano yake na chombo kimoja cha habari nchini.

Katika mahojiano hayo yaliyoanza kusambaa Jumapili iliyopita, ikiwa ni kumbukumbu ya miaka mitatu tangu kifo cha Magufuli, mstaafu huyo wa Jeshi la JWTZ anasema, “Kulikuwa na ugumu wa kutangaza nani atarithi kiti hicho, licha ya Katiba ya kuanisha wazi.”

MwanaHALISI limeelezwa na baadhi ya wachambuzi wa kisiasa, kwamba wengine wanaoweza kuwafahamu waliokuwa katika njama za kuvunja Katiba, ili Rais Samia asiapishwe kuwa rais, ni Diwani Athuman, aliyekuwa mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na Simion Sirro, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IJP).

Katika orodha ya wanaoweza kuwafahamu waliotaka kuzuia urais wa Samia, ni Dk. Bashiru Ally, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi; Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri na Prof. Adelardus Kilangi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Aliyekuwa mkuu wa majeshi nchini (CDF), Jenerali Venance Mabeyo

Kwa mujibu wa Ibara ya 37 (5) ya Katiba, ni kwamba “endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobakia…”.

Mara baada ya kifo cha Magufuli, taarifa zinasema, baadhi ya vigogo waandamizi serikalini, walitaka Samia aliyekuwa kikazi mkoani Tanga, asitangazwe kumrithi Magufuli.

Badala yake, vigogo hao walitaka taifa lirejee kwenye uchaguzi wa rais, ambao tayari ulikuwa umefanyika takriban miezi mitano iliyopita.

Katika mazingira hayo, haijaweza kufahamika mpaka sasa, ilikuwaje Majaliwa na Dk. Bashiru, waliokuwa mkoani Dodoma, takribani kilometa 450 kutoka Dar es Salaam, walipewa taarifa na waliwahi kufika kabla makamu wa Rais aliyekuwa mkoani Tanga, ambako ni takriban kilometa 350 kutoka jijini humo.

Kunadaiwa kulikuwa na mvutano mkali uliochagizwa na hisia za jinsia, dini na hofu ya maslahi ya baadhi ya watu waliokuwa karibu na Magufuli, aliyekuwa akikamilisha muhula wake wa pili wa uongozi.

Baadhi yao, wakiwamo wale waliokuwa wameanza mbio za kutaka kumrithi Magufuli 2025, waliamini ujio wa Samia ungetibua mipango yao kwa kuwa atakuwa mgombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

Hofu hiyo, ilitokana na kinachoitwa, “utaratibu” wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumwachia rais aliyepo madarakani kugombea muhula wake wa pili.

“Walishapiga hesabu kwa mujibu wa Katiba, Magufuli angeondoka madarakani 2025 na hivyo wangekuwa na fursa ya kumweka mtu wao na kupanga safu zao za uongozi,” kimeeleza chanzo kimoja cha taarifa kutoka serikalini.

Gazeti hili linawafahamu vigogo kadhaa ndani ya CCM, walioamini kuwa hiyo ndiyo fursa ya kumweka madarakani rais wanayemtaka na kuunda safu yao ya uongozi kwa kuwa chini ya Rais Samia, “wasingeweza kupata walichopanga.”

Aidha, vigogo hao waliamini kuwa Rais Samia ni mwepesi, asingeweza kufanya kazi kubwa kama alivyokuwa mtangulizi wake, aliyeanzisha miradi mbalimbali. Walishindwa kutimiza matakwa hayo, baada ya kuelekezwa “warejee kwenye Katiba.”

Katika mvutano huo, baadhi ya vigogo walijikuta wakijutia uamuzi wa Rais Magufuli kumpendekeza Samia kuwa mgombea wake mwenza wa urais, mwaka 2015 na 2020.

Ugumu uliotokana na kuwapo pande mbili, kwa mujibu wa Mabeyo, ulisababisha kupita zaidi ya saa 48, kabla Rais mpya kuapishwa, jambo ambalo ni kinyume na Katiba.

Muonekano wa kaburi la Hayati John Magufuli

Alichokisema Mabeyo kwa mara ya kwanza tangu alipostaafu Juni 2022, ndicho kilichokuwa kikisemwa wakati zilipoanza kuzagaa taarifa za kifo cha Magufuli na baadaye makamu wa rais (Samia) kulitangazia taifa juu ya kifo hicho.

Swali kubwa linaloumiza vichwa vya baadhi ya watu, ni pamoja na kwa nini mpaka sasa, majina ya waliotaka kumzuia Samia kurithi mikoba ya urais, hayajawekwa hadharani?

Kwa nini wahusika wanaendelea kusalia serikalini na kupewa nyadhifa kubwa, wakati hawaiheshimu Katiba waliyoapa kuilinda na kuitetea?

Figisu za kutaka kumzuia kutangazwa kumrithi Magufuli, ndizo zinazotajwa na wachambuzi hao, kuwa zilimchochea Rais Samia, “kueleza umma kijasiri, aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwenye jinsia ya kike.”

Alitoa kauli hiyo, wakati wa mazishi ya kitaifa ya Magufuli, yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, tarehe 22 Machi 2021.

Ingawa Rais Samia hakufafanua ujumbe wake ulilenga nini, wadadisi wa mambo, wanaohusisha zilikuwa salaam kwa wale waliotaka kumzuia kuwa rais na waliokuwa wanamuona mwepesi.

Mara baada ya Rais Samia kuingia Ikulu, ndani ya siku kumi na mbili, alimwondoa Dk. Bashiru kwenye wadhifa wa katibu mkuu kiongozi. Alimteua kuwa mbunge, jambo lililomwingiza kwenye historia ya kukalia kiti hicho kwa muda mfupi.

Dk. Bashiru aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa katibu mkuu kiongozi, tarehe 17 Februari 2021, kuchukua nafasi ya Balozi John Kijazi.

Wakati anateuliwa kuwa katibu mkuu kiongozi, Dk. Bashiru alishaondoka kwenye utumishi wa umma. Alikuwa katibu mkuu wa CCM.

Mbali na Dk. Bashiru, Rais Samia alimwondoa kazini Sirro, mwaka mmoja kabla ya muda wake wa kustaafu. Aliteuliwa kuwa balozi nchini Zimbabwe.

Naye Diwani aliondolewa kwenye wadhifa wa mkurugenzi wa usalama wa taifa na kupelekwa Ikulu, kuwa Katibu wa Rais. Baadaye aliomba kustaafu. Aliondoka kabla ya muda wake.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Prof. Kilangi, pamoja na kwamba hakutajwa na Mabeyo katika safari ya mwisho ya Magufuli na ujio wa Samia, aling’olewa kwenye wadhifa wake kwa kuteuliwa kuwa balozi.

Kwa upande wa Mabeyo, kulikuwa na taarifa za kuongezewa muda wa kutumikia nafasi hiyo, kama ilivyofanyika kwa baadhi ya viongozi wenzake wa vyombo vya ulinzi na usalama, lakini muda wake wa kustaafu ulipofika, aliondoka madarakani.

Mabadiliko ya vigogo hao kwenye nafasi hizo, yalilenga kumwezesha Rais Samia, kuunda safu mpya ya uongozi.

Kupatikana kwa taarifa hizi, kumekuja miaka mitatu baada ya Mabeyo kumweleza Rais Samia, tena mbele ya umma, kwamba  “kuna mambo nitakuja kukuambia.”

Alitoa kauli hiyo, wakati wa mazishi ya Magufuli wilayani Chato, kauli ambayo ilizusha utata kwa jamii kwa kuwa baadhi yao walihoji ilikuwaje kiongozi huyo ametoa kauli hiyo hadharani wakati angeweza kumwona ofisini, kumuandikia barua au kumpigia simu.

Katika mahojiano aliyoyafanya, Mabeyo hakueleza kama jambo alilotaka kwenda kumwambia Rais Samia alishamweleza au bado.

Aidha, Mabeyo katika mahojiano yake hayo, alieleza kuwa saa 24 kabla ya kifo cha Magufuli, yeye na wakuu wenzake wawili wa vyombo vya ulinzi na usalama, walishirikishwa kwa lengo la kujua hali ya Rais inavyoendelea hivyo safari za kuingia na kutoka chumba alicholazwa hazikukauka.

Alisema, walilazimika kumpeleka Magufuli hospitali ya Mzena, kutoka Muhimbili kwa kuwa waliamini kuna utulivu na udhibiti unaomwezesha mgonjwa kupumzika vizuri.

Hata hivyo, katika mahojiano hayo, Mabeyo alishindwa kukata kiu ya wananchi waliotaka kujua, ni sababu gani taarifa za ugonjwa wa kiongozi huyo zilifanywa kuwa siri kiasi cha watu kuanza kutangaza kifo chake siku chache, kabla ya kutangazwa rasmi.

Taarifa zilizokuwa zikisambaa zilidai kuwa kiongozi huyo alifariki kabla ya 17 Machi 2021, lakini kutokana na kuwapo kwa mvutano walilazimika kuvuta muda ili kuweka mambo sawa na kuepusha nchi kuingia kwenye migawanyiko.

Lakini maelezo ya Mabeyo yanafuta uvumi huo, ambapo alisema, hali ya Magufuli ilibadilika tarehe 16 Machi. Alisema, Magufuli aliona hawezi tena kupona, hivyo akaomba arudishwe nyumbani ili kifo kimkute akiwa huko.

Alisema: “Aliniagiza niwaambie madaktari, wamrudishe akafie nyumbani. Nami nikamwambia, hapana hapa upo kwenye mikono salama, madaktari wapo wanaendelea kukutibu.

“Aliniambia siwezi kupona hivyo niwaambie madaktari wamrudishe nyumbani”. Nilimjibu, “sina mamlaka hayo”. Akasema, “yaani CDF unashindwa kuwaamuru madaktari wanirudishe nyumbani?” Nikamwambia “suala la afya yako siyo la CDF mheshimiwa, naomba ubaki utulie, madaktari watatuambia cha kufanya.”

Mabeyo anasema, Magufuli aliomba aitiwe paroko wake wa St Peters (Father Makubi) na akamwomba Kardinali Polycarp Pengo naye aende. Anasema, walipofika walimfanyia ibada kwa taratibu za Kanisa Katoliki na kumpa sakramenti ya upako wa mgonjwa aliyekuwa katika hatari ya kufariki.

Alisema, walipomaliza kumsalia akapumzika. Lakini ilipofika saa nane mchana, walipigiwa tena simu na kuambiwa hali ya mgonjwa siyo nzuri, hivyo waende na walipofika walimkuta ametulia na hawezi kuongea tena.

“Tukawaita madaktari wengine, nakumbuka tulimwita Prof. Maseru, (Lawrence Maseru), Prof. Janabi (Mohamed Janabi) alikuwepo muda wote, kwa hiyo yule aliongezea nguvu wakajaribu kumwangalia. Tukaendelea kukaa mpaka jioni, ikafika jioni saa kumi na mbili na nusu hivi au saa moja kasoro akakata roho, tukiwepo wakuu wa ulinzi wa vyombo watatu mimi (CDF), IJP na DGS,” alisimulia.

Kutangazwa Rais:

Mabeyo amesema, suala la kutangazwa msiba lilikuwa moja, lakini kazi kubwa ilikuwa namna ya kumwapisha Rais, kwani kulikuwa na mawazo ya aina mbili. Alisema, wapo waliotaka rais aapishwe baada ya mazishi wengine kabla.

“Kulikuwa na mjadala mkubwa lakini ‘logic’ ikaja kwamba kuna marais watatoka nje ya nchi kuja kumzika mwenzao, watapokelewa na makamu wa Rais au Rais, lazima awepo Rais.

Alisema: “Ndiyo maana tukapokea maamuzi kwamba lazima makamu wa Rais aapishwe kama Rais. Ndiyo maana ilipita siku mbili, kikatiba hairuhusiwi inatakiwa kabla ya saa 24 awe ameshaapishwa Rais mwingine.

“Sasa ilipita tarehe 17, 18 mpaka tarehe 19 ndiyo akaja kuapishwa kulikuwa na majadiliano hapo lakini tunamshkuru Mungu likapita, lakini namna ya kumwapisha nako ulikuwa mjadala tunamwapishaje.

“Lakini wakasema isiwe sherehe, wengine wanasema iwepo. Kama Mkuu wa Majeshi nikasema paredi lazima iwepo, bendera ya Amiri Jeshi Mkuu lazima ipandishwe kwa gwaride. Lakini kidogo kulikuwa na kamvutano tupo kwenye msiba lakini paredi iwepo kwa nini. Nikasema huyu ni Amiri Jeshi Mkuu anayeapishwa, asipoapishwa kwa taratibu hizo za kitaifa Jeshi halitamtambua.”

2 Comments

  • CDF Mbeyo apewe nishani kwa kulinda katiba na ikiwezikana asimamie zoezi la kuboresha katiba na hatimaye katiba mpya. Swala la mfumo dume lipo sana katika nchi za kiafrika , kwa hiyo ni jambo la busara kwa Mhe Rais kuwapa majukumu wale wote walitoa maoni katika mchakato wa kupokea kijiti ili isionekane analipa kisasi.

  • Naunga mkono hoja. Mabeyo angekuwa natamaa yeye leo angekuwa rais. Tunamwomba mama ampe jukumu la kuandika katiba kwa sababu anaweza kuaminika kabisa kwa ushuhuda huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Samia awataka watanzania kudumisha muungano

Spread the loveRais wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendeleza Muungano kwa...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

error: Content is protected !!