Rais Samia Suluhu hassan amesema Hayati rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi alikuwa ni maktaba inayotembea na iliyosheheni vitabu vyenye mafunzo ya uadilifu, uzalendo, ustahimilivu, mageuzi, ujasiri, unyenyekevu na uchamungu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akizungumza katika shughuli ya kuaga mwili rais huyo mstaafu wa awamu ya pili leo Jumamosi katika uwanja wa Aman Complex Visiwani Zanzibar, Rais Samia amesema hadhani kama anaweza kuvaa viatu vyake.
“Nimeukumbuka msemo wa Kiafrika unaosema anapofariki mzee, maktaba inaungua moto, yaani kila kitu alichonacho mzee anapofariki ni kama maktaba iliyoungua moto kumbukumbu zote zinapotea, mtakubaliana nami kwamba maktaba yetu moja kubwa iliyosheheni hadithi nyingi na nzuri imeungua moto,” amesema Samia.
Hayati Alhaj Ali Hassan Mwinyi anazikwa leo Jumamosi Kijiji kwao Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Wilaya ya Kaskazini B Unguja.
Rais huyo wa awamu ya pili alifariki dunia tarehe 29 Februari mwaka huu katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.
Leave a comment