Friday , 24 May 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Askofu Bagonza: Potofu huzaa potoshi/ potoshi huzaa potofu?
Makala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Potofu huzaa potoshi/ potoshi huzaa potofu?

Spread the love

Dayosisi 7 za KKKT katika kanda ya Ziwa na Magharibi, kupitia Chuo cha Theologia na Biblia cha Nyakato, zinatekeleza mradi muhimu kuhusu mafundisho ya imani.

Mradi huu unaoitwa “Theologia Potoshi” (Misleading Theology) unagusa nyanja karibu zote za maisha ya mwanadamu. Kupitia mradi huu, mkataba wa ushirikiano umewekwa kati ya Chuo cha Nyakato na Chuo

kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) ili kuwawezesha vijana kutumia fikra tunduizi (Critical Thinking) katika kubaini upotoshaji unaofanywa na sisi wahubiri wa imani. Kwa mfano:

1. Muumini akitaka kupata gari aweke fedha kwenye bahasha alete kwa ninayejiita Askofu Bagonza nimwombee apate gari, LAKINI Askofu Bagonza akitaka gari waumini wakamukiwe kwa michango kununua gari?!

2. Muumini akiugua sana alete sadaka kubwa kwa Askofu Bagonza aombewe ili apone lakini Askofu Bagonza akiugua kikohozi waumini wachange hela ili Askofu akatibiwe Ujerumani.

3. Waumini wenye shida ya hela na umaskini waweke sadaka ya “kujimaliza” kwenye bashasha na kuleta kwa Askofu Bagonza halafu wainue simu juu ili mihamala iingie kwenye simu zao kutoka mbinguni?!

4. Gesi ya kupikia ya muumini ikiisha jikoni aende kwa Askofu Bagonza na kununua “upako” maalum. Kuanzia siku hiyo, gesi haitaisha mtungini.

5. Mtu akiugua akaenda kuombewa na Askofu Bagonza, ataambiwa nyota yake imeibiwa, hatimaye iko mikononi mwa fulani, madhabahu yake imefungwa, ana laana ya kuzaliwa, malango yake yamefungwa, nguvu yake haijaachiliwa mpaka atoe sadaka inayouma nk.

Mwanadamu amekatwa vipande vitatu: cha kiroho mashariki; cha kimwili Magharibi na kiakili kusini. Imani imetumika kudhalilisha utu; kuibia watu, kuvuruga ndoa, kuua maadili ya kazi na sasa yameingia serikalini. Watu wanaoteshwa viongozi wanaofaa na wasiofaa; vyama vinavyofaa na visivyofaa na wanasiasa walio chaguo la Mungu na wa shetani. Taifa haliko salama.

Wanasiasa nao na watawala wetu wametelekeza hatima yao mikononi mwa wahubiri anguko na kugeuzwa mawakala wa “mungu”-tumbo-maokoto. Nafikiri:

a) Tuna tatizo kubwa la afya ya jamii. Wahubiri wagonjwa wanawahubiria wagonjwa wenzao na sasa tuko mlipuko-mpasuko. Nami naweza kuwa humo.

b) Watu wanapendekeza serikali iingilie kati. Wanamtukuza jirani yule kwa kufunga makanisa. Akimaliza kufunga makanisa atafunga midomo kama hajaifunga.

c) Serikali isiyo na dini haiwezi kujiingiza katika masuala ya imani ikawa salama. Wateja wa wahubiri upako wako serikali. Tukikagua mikoba kwenye lango la bunge tunaweza kupata upofu kwa tutakayoyaona.

d) Tujenge hospitali nyingi za afya akili na tuache kuuchokonoa mfumo wetu wa elimu. Tumetengeneza wajinga wengi ambao ni wateja wakubwa wa mafundisho potofu. Hakuna aliye salama.

e) Huduma za afya ni kitalu cha kutengeneza wajasiria mali wa imani za watu. Aliibuka mzee wa kikombe Loliondo. Adui angepenyeza sumu pale tusingepata wa kutangaza siku za maombolezo. Hata madaktari walienda, hata sisi tunaojifanya “wasaidizi” maalum wa Mungu wetu. Tuna matatizo ya kiafya yanayopimika kitaalamu. Hakuna kipimo cha pepo hospitali.

Hubirini, fundisheni, fanyeni maigizo yote lakini acheni kuchonganisha roho na mwili. Mwili usio na roho ni maiti na roho isiyo mwili ni pepo.

Acheni kuibia watu kwa kutumia imani. Himiza watu wafanye kazi, tetea haki za wanyonge, himiza elimu bora, boresha afya. Watakaoshindikana huko, peleka Milembe.

Anayeamini hiyo miujiza aruhusiwe kujifanyia mwenyewe siyo kwa wengine au afanye bure.

Anaandika Askofu Dk. Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe iliyoko mkoani Kagera.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia muonee huruma Dk. Phissoo

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wiki iliyopita baada ya kuwa nimekuandikia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

GGML inavyookoa walemavu dhidi ya dhana potofu

Spread the loveMKOA wa Geita ni mmoja wa mikoa ya Kanda ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 63 ya Uhuru bila katiba ya wananchi

Spread the loveWAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanaharakati...

AfyaMakala & Uchambuzi

Uongo, uzushi, tiba ya matende, ngiri maji

Spread the loveKUNA uongo na uzushi katika jamii kuhusu wanaume, wanawake na...

error: Content is protected !!