Friday , 10 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wapinzani wamlilia Rais Mwinyi
Habari za Siasa

Wapinzani wamlilia Rais Mwinyi

Spread the love

VYAMA vya siasa nchini Tanzania, vimetuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, kilichotokea tarehe 29 Februari 2024, akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Kifo cha Hayati Mwinyi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kilitangazwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyesema mwili wake utazikwa tarehe 2 Machi 2024, Unguja visiwani Zanzibar.

Katika nyakati tofauti, viongozi wa vyama hivyo vya upinzani wametuma salamu za rambirambi na kuelezea namna walivyomfahamu kiongozi huyo aliyejizolea umaarufu kwa falsafa yake ya ruksa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia kwa Makamu wake Mwenyekiti Zanzibar, Salum Mwalim, kimesema “Chadema itamkumbuka kwa namna alivyosimamia mageuzi ya sera za kiuchumi za Tanzania na kuruhusu mifumo ya uhuru wa soko, sera ambayo imekuwa ndio msimamo wa Chadema katika kukuza uchumi na kuchochea maendeleo.”

Mwalim amesema Hayati Mwinyi atakumbukwa kwa hekima, busara, uwajibikaji na kujituma kwake wakati akiwa Rais na hata kabla ya kushirikilia wadhifa huo.

Naye Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, ameitaka Serikali ikamilishe mageuzi ya kiuchumi na kisiasa, ili kumuenzi kwani enzi za uongozi wake alihakikisha anaiondoa nchi kwenye mdororo wa kiuchumi.

“Rais Mwinyi amefariki fedha za kigeni zikiwa adimu, hali ya uchumi iko tete yenye kuhitaji mageuzi mengine makubwa. Tumuenzi kwa kufanya mageuzi hayo ambayo pamoja na mambo mengine yatainua uchumi wa watu wengi na kupunguza bei ya bidhaa muhimu na ugumu wa maisha kwa wananchi,” amesema Mnyika.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kifo cha Mwinyi ni msiba mzito kwa taifa.

“Ni msiba mkubwa kwa Taifa letu. Mzee Ali Hassan Mwinyi Atakumbukwa kwa kufungua uchumi wa Nchi yetu na kuongoza mageuzi ya kisiasa kuingia mfumo wa vyama vingi. Alifanya wajibu wake kwa Taifa letu. Aliongoza taifa letu wakati mgumu sana. Pole sana kwa familia, ndugu na Jamaa. Apumzike kwa amani,” ameandika Zitto kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amesema chama chake kimepokea kwa mshtuko kifo cha Hayati Mwinyi, huku akisema kitaomboleza kifo chake kwa kupeperusha bendera nusu mlingoti ndani ya siku saba.

“Marehemu Mwinyi ameweka historia ya kuwa mwalimu wa uwajibikaji pale alipoamua kujiuzulu uwaziri wa mambo ya ndani ya nchi 1977 kutokana na makosa yaliyofanywa na watimishi wa wizara aliyokuwa anaongoza na kusababisha vifo na mateso kwa watu waliotuhumiwa kuua raia kwa imani za kishirikina,” amesema Prof. Lipumba.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kamati Kuu Chadema kuketi Mei 11

Spread the loveKAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inatarajiwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yapunguza kodi ya makampuni kwa 20%

Spread the loveSERIKALI imepunguza kodi ya makampuni kwa asilimia 20, kutoka asilimia...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu, Halima Mdee hapatoshi

Spread the loveVITA ya maneno kati ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Madiwani Msalala wampa tano DED kwa kuongeza mapato

Spread the loveMKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, mkoani Shinyanga, Khamis...

error: Content is protected !!