Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Ukatili waishtua TAMWA, yatoa mapendekezo
Habari Mchanganyiko

Ukatili waishtua TAMWA, yatoa mapendekezo

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben
Spread the love

 

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimeshauri wadau wa masuala ya ukatili wa kijinsia, kukaa pamoja na kupanga mikakati mipya na madhubuti ya kumaliza au kupunguza matukio ya ukatili yanayoendelea nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

TAMWA imejitokeza kuzungumzia matukio hayo ambayo takwimu zinaonesha, uwepo ikiwa dunia inaadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, kuanzia leo Jumatano, tarehe 24 Novemba 2021.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chilo akijibu swali bungeni jijini Dodoma, tarehe 12 Novemba 2021 alisema, kuanzia Januari hadi Septemba 2021, takwimu ya vitendo vya ukatili kwa watoto vilivyoripotiwa vituo vya Polisi inaonesha watoto 6,168 wamefanyiwa ukatili.

Alisema kati ya watoto hao waliofanyiwa ukatili, wanawake 5,287 na wanaume 881. Waliobakwa ni 3,524, waliolawitiwa ni 637 kati yao wanaume 567 na wanawake 70, waliochomwa moto ni 130 kati yao wanaume 33 na wanawake 97, waliopata mimba ni 1,877.

Chilo alisema, kesi na watuhumiwa waliokamatwa na kufikishwa mahakamani ni 3,800. Kesi zilizo chini ya upelelezi ni 2,368 na kesi zilizohukumiwa ni 88 na nyingine ziko kwenye hatua mbalimbali mahakamani.

Takwimu hizi zinaamanisha nini? Zinamaanisha kwamba, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa basi katika kipindi cha mwaka mmoja, zaidi ya watoto 7,000 watakuwa wamebakwa au watoto zaidi ya 12,000 watakuwa wamefanyiwa ukatili.

Takwimu hizi mpya zinaogofya na kuwafanya TAMWA waone wapengine wadau, ikiwamo serikali, wazazi na walezi, wakubaliane na kutamka kuwa; ‘Ubakaji sasa ni janga.’

“Ni muhimu kwa taifa, sasa kuendelea kubuni njia mbadala na mpya za kukabiliana na janga hili. Tunaliita janga kwa sababu, watoto 3,524 kubakwa si lelemama, bali ni tatizo kubwa katika jamii yetu ambalo linaharibu kabisa mustakabali wa maisha ya kizazi kijacho,” amesema, Dk. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA

Aidha, Dk. Rose ameipongeza mahakama kwa kutoa hukumu na kufuatilia kwa ukaribu kesi hizi za ubakaji, kwani ipo mifano ya waliohukumiwa kwa kufanya matukio hayo.

Amesema, tunayapongeza madawati ya jinsia kwa kusimamia upelelezi na kutoa ushauri kuhusu matukio au kesi hizi za ubakaji na ukatili mwingine. Hata hivyo bado matukio haya yanaendelea kuongezeka kila kukicha. Je tatizo lipo wapi?

“Ukatili huu, una madhara ya muda mfupi, muda mrefu, kiuchumi, kimwili na kisaikolojia kwa wanawake na wasichana na watoto wote kwa ujumla, kwani inawazuia kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika jamii yao,” amesema Dk. Rose

Mkurugenzi mtendaji huyo amesema, “hakuna namna nyepesi ya kuelezea madhara haya ya ukatili wa kijinsia, tumewahi kuona, pengine tumesikia lakini bado jamii nzima haijajua madhara yake kwa kina labda kwa sababu, matukio haya hayatokei kwa wingi mara moja. Lakini tungewapata waathirika hawa na kuwakusanya pamoja, basi Tanzania ingelia.”

Amesisitiza akisema “ubakaji huu wa watoto ni janga. Serikali itambue kuwa hili ni janga kwa sababu madhara yake yanaweza yasionekana kwa sasa lakini yataonekana baadaye wakati ambapo kizazi hiki cha sasa kitakapokuwa kimeshika usukani.”

Amesema, TAMWA inaamini kuwa taifa salama ni lile linalojenga kizazi salama, ambacho waliopo wanawalinda watoto na kumlinda mwanamke. Hivyo basi, ili kuwa na jamii hiyo hatuna budi kuchagizana kwani; waswahili walisema; ‘’Kichango ni kuchagizana.

Kidunia hali ni kama hii, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wanawake (UN-Women) zinaonesha ukatili wa wanawake aghalabu hufanywa na mwenza, mume wa zamani au wa sasa. Inaelezwa wanawake zaidi ya milioni 640 wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea waliwahi kufanyiwa ukatili na wenza.

Ukatili huu unatajwa kusababisha msongo wa mawazo, kihoro, mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa ikiwamo UKIMWI na wakati mwingine waathirika kujiua.

Takwimu hizo kadhalika zinaeleza, zaidi ya wanawake 87,000 duniani waliuawa na nusu yao, (50,000) waliuawa na mwenza au mwanafamilia. Zaidi ya thuluthi, waliuawa kwa makusudi na mwenza/mume wa sasa au wa zamani.

“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonesha wazi kuwa anasimamia vyema haki za wanawake na watoto, tumemuona na kumsikia akipinga lugha dhalilishi kwa wanawake na udunishwaji wa kundi hilo katika nafasi za siasa na uongozi. Kongole Rais wetu,” amesema Dk. Rose

Ameongeza “TAMWA hatutaacha kusimamia haki za wanawake, watoto na wanahabari, tutaendelea kupaza sauti hadi tutakapoona amani imetawala tukiendelea kusema “Ewe Mwananchi, Pinga ukatili wa kijinsia Sasa.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

error: Content is protected !!