December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Hukumu kupinga wanaharakati kutinga kortin kujulikana leo

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, leo Alhamisi tarehe 25 Novemba 2021, inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya kupinga marekebisho ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu, ya 2020, yanayozuia mtu kufungua kesi asiyokuwa na maslahi nayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa mbele ya majaji watatu wa Mahakama Kuu, ambao ni Jaji Elinaza Luvanda, Yose Mlyambina na Stephen Magoiga.

Kesi hiyo ya madai Na. 09/2021, ilifunguliwa na mtetezi wa haki za binadamu, wakili Onesmo Olengurumwa, akipinga kifungu cha nne cha sheria hiyo, kinachoelekeza mtu anayetaka kufungua kesi mahakamani, lazima athibitishe kuathirika moja kwa moja na suala lililosababisha kufungua kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, Olengurumwa ambaye ni Mratibu wa THRDC, anadai kifungu hicho kinazuia wajibu wa mtu na au taasisi, katika kudhibiti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, pamoja na kuilinda katiba na sheria za nchi.

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu

Olengurumwa anadai, kifungu hicho kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, misingi ya mgawanyo wa madaraka, utawala wa sheria na utawala bora, kama inavyoelekezwa na matakwa ya katiba hiyo.

Mtetezi huyo wa haki za binadamu anadai, kifungu hicho kinakiuka mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania iliingia, ikiwemo mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Makataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa.

Hoja nyingine ya Olengurumwa, anadai kifungu hicho kimempa mamlaka makubwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kinyume na katiba.

error: Content is protected !!