Thursday , 2 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Rais Samia amkabidhi Kikwete nyumba ya kuishi
Habari Mchanganyiko

Rais Samia amkabidhi Kikwete nyumba ya kuishi

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemkabidhi nyumba ya kuishi, Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Ni iliyojengwa katika Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam ambayo imejengwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Nyumba hiyo ni utekelezaji wa kifungu namba 12 cha Sheria ya mafao ya hitimisho la kazi kwa viongozi wa siasa, sura ya 225 na marejeo ya mwaka 2020 ambayo pamoja na stahili zingine za matunzo ya viongozi wakuu wastaafu inaelekeza kuwa Rais anayestaafu anastahili kujengewa nyumba ya kuishi yenye hadhi ya Rais.

Mara baada ya kukabidhi nyumba hiyo, leo Jumapili, tarehe 9 Mei 2021, Rais Samia amempongeza Kikwete kwa kupata makazi hayo na amemhakikishia, Serikali itaendelea kumtunza yeye na viongozi wengine wastaafu kama inavyoelekezwa katika sheria.

Amebainisha Serikali itafanyia kazi uboreshaji wa sheria hiyo pamoja na kuhakikisha wajane/wagane wa viongozi wanatunzwa.

Rais Samia amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa kuanza maandalizi ya kutimiza haki zote anazostahili aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake, Waziri Mchengerwa amesema nyumba hiyo ni ya tatu kukabidhiwa ikitanguliwa na nyumba ya Rais Mstaafu Hayati Benjamin William Mkapa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na kwamba nyumba ya Baba wa Taifa Hayati Mwaimu Julius Kambarage Nyerere ilijengwa na kukabidhiwa kwake na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika shukrani zake, Rais Mstaafu Kikwete aliyeongozana na Mkewe, Mama Salma Kikwete ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutekeleza takwa hilo la kisheria.

Ameishukuru TBA kwa kukamilisha ujenzi tangu ulipoanza mwaka 2018 na amemshukuru Rais Samia kwa kumkabidhi nyumba hiyo.

Rais Mstaafu Kikwete amempongeza Rais Samia kwa uongozi wake tangu alipopokea kijiti kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais Hayati John Pombe Magufuli kwani nchi imetulia, mambo yanakwenda na watu wana matumaini makubwa nae.

Taarifa kuhusu makabidhiano hayo, imetolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yashiriki maadhimisho Mei Mosi Arusha

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeungana na maelfu ya...

Habari Mchanganyiko

Makonda autaka mgodi kubadilisha maisha ya wana-Geita

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ametoa wito kwa...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Je, miji ya Uingereza inafilisika?

Spread the loveMNAMO 1890, mwandishi mmoja wa habari Mmarekani aitwaye Julian Ralph...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Equity Bank yaendelea kusotea mabilioni ya fedha mahakama rufani

Spread the loveBENKI za Equity ya Tanzania na Kenya, zimeendelea kupambana mahakamani...

error: Content is protected !!