Tuesday , 30 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Lipumba aibua mjadala Katiba mpya mbele ya Magufuli
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba aibua mjadala Katiba mpya mbele ya Magufuli

Prof. Ibrahim Lipumba
Spread the love

 

PROFESA Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), amemkumbusa Rais wa Tanzania, John Magufuli kutekeleza ahadi yake aliyoitoa Mwaka 2015 ya kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya wakati wa kuzindua Bunge. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Prof. Lipumba ametoa ombi hilo leo Jumatatu tarehe 1 Februari 2021, katika Maadhimisho ya Miaka 100 ya Mahakama nchini Tanzania, yaliyofanyika jijini Dodoma.

“Pamoja na mengine mengi, ulisema katika kipindi chako cha mwisho, utahakikisha uliyoahidi 2015 nayo yanatekelezwa.”

“…na moja uliyoahidi kwamba, kuna kigogo kiliachwa kukamilishwa, suala ambalo Watanzania wengi walishiriki kutoa maoni yao ili iweze kupatikana Katiba Mpya,” amesema Prof. Lipumba.

Amesema, ahadi hiyo Rais Magufuli aliitoa wakati akifungua Bunge la 11 tarehe 20 Novemba 2015, mkoani Dodoma.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 11 aliyoitoa tarehe 20 Novemba 2015, bungeni jijini Dodoma, alizungumzia Katiba Mpya akisema, “serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika awamu iliyopita kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura.

“Napenda kuwahakikishia kuwa, tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema “tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba.”

Ahadi hiyo ya Rais Magufuli, ilipewa nguvu katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/20, kifungu cha 144 (e) iliposema “mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya umeendeshwa na umefikia hatua ya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba ambayo itapigiwa Kura ya Maoni na wananchi.”

Katika kifungu cha 145 (g), CCM itahakikisha, inakamilisha mchakato wa kutunga Katiba mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Kutokana na kauli hiyo, Prof. Lipumba amemkumbusha Rais Magufuli kwamba “kwenye hotuba yako ya kuzindua Bunge ukawaeleza wabunge pamoja na yale uliyoeleza siku hiyo tarehe 13 Novemba 2020, wazingatie yale yote yaliyomo kwenye hotuba uliyotoa tarehe 20 Novemba 2015.

Rais John Magufuli

“Ulisema hilo utalitekeleza, ulipopokea Ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ulisema kabisa masuala yale ambayo yamo kwenye katiba iliyopendekezwa, serikali yako iko wazi itapokea,” amesema.

Mwanasiasa huyo amemuomba Rais Magufuli katika kipindi chake cha mwisho cha uongozi wake, ahakikishe Katiba Mpya inapatikana ili iwe alama yake kwa Watanzania.

“Viporo ulivyovitoa ambavyo hujavitekeleza, 2015 ulivisema utavitekeleza, natoa wito hivyo viporo vyote katika kipindi hiki uweze kutekeleza.”

“Utakapomaliza kipindi chako, watu watakaoweza kuyalinda mafanikio uliyoyaleta katika nchi yetu ni kuwa na Katiba inayotokana na mapendekezo ya Watanzania,” amesema Prof. Lipumba.

Rais Magufuli aliingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015, baada ya kuapishwa kumrithi Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya nne.

Kwa sasa Rais Magufuli yuko katika kipindi cha mwisho cha uongozi wake wa awamu ya tano, ambapo tamati yake ni 2025.

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein (katikati) wakionesha Rasimu ya Katiba Mpya

“Nina uhakika kwa sababu hili jambo ni la kwako, si la kwetu. Liko katika uwezo wako, naamini utashughulikia, utatuachia urithi wa Katiba inayotokana na wananchi,” amesisitiza Prof. Lipumba.

Wakati huo huo, Prof. Lipumba amemshauri Rais Magufuli kuwatumia waliokuwa wajumbe wa Bunge la Katiba ambao baadhi yao ni wateule wake, kufufua mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya kwa kutumia Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba.

Amewataja wajumbe huo kuwa ni Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi.

Pia, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson aliyeongoza Kamati ya Vyuo Vikuu iliyochambua na kutoa mapendekezo kuhusu rasimu ya Jaji Warioba.

“Kwa bahati ulikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na Mama Samia alikuwa Makamu Mwenyekiti, kuna wazee wazito Prof. Kabudi walikuwa Wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba, kuna vijana wako Polepole (Humphrey) ndio alikuwa mjumbe,” amesema Prof. Lipumba na kuongeza.

          Soma zaidi:-

“Kwa hiyo una watu waliokuzunguka ambao ni wajumbe wa baraza. Ukihitaji vitendea kazi viko vya kutosha, Naibu Spika tena tulikuwa naye kwenye kamati moja na yeye aliongoza kamati ya Chuo Kikuu. Iliyotoa mapendekezo maalumu kuhusu Katiba Mpya na kuichambua Rasimu ya Jaji Warioba,” alisema Profesa Lipumba huku Rais Magufuli akionekana kutabasamu

Tarehe 1 Novemba 2018, akizungumza katika kongamano kuhusu hali ya uchumi na siasa Tanzania, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema, hategemei kutenga fedha kwa ajili ya mchakato huo kwa sasa.

Alisema, kuliko fedha kutumika katika mchakato huo, ni bora zielekezwe katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli.

Rais Magufuli alisema, kama kuna watu wanataka kusaidia kutoa fedha kwa ajili ya mchakato huo, ni bora wasaidie katika ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge-SDG).

“Tusitumie hela ya kupeleka watu bungeni wakalipane posho za kila siku, tunataka hizo fedha zitumike kujenga reli, kuimarika kilimo, na ndio maana kuna mataifa makubwa katiba zao zimeundwa miaka kadhaa zilizopita. Tutakaa kubishana kupoteza pesa ‘for nothing’, huu si wakati wake,” alisema na kuongeza:

“Sitegemei kupanga hela kwa ajili ya watu kula kwa sasa hivi, na kama wako watu wanataka kutusaidia hizo fedha, watusaidie kujenga reli. Lakini sikatai kusikiliza maoni ya watu, kuna ushauri tunapokea, Lakini ninachotaka kuwambia tunaenda vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Mchakato huo, uliishia Katiba inayopendekezwa iliyokabidhiwa kwa waliokuwa marais wa wakati huo, Jakaya Kikwete wa Tanzania na Dk. Ali Mohamed Shein na waliokuwa viongozi wa Bunge Maalum la Katiba, marehemu Samuel Sitta (mwenyekiti) na Samia Suluhu Hassan akiwa makamu mwenyekiti.

Hata hivyo, tarehe 2 Aprili 2015, aliyekuwa mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alitangaza kuahirishwa kwa kura ya maoni iliyokuwa ifanyike 30 Aprili 2015, kutokana na kutokukamilika kwa uandikishaji wa dafatari la wapiga kura.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

Habari za SiasaTangulizi

Samia ataja miradi ambayo Tanzania inashirikiana na IDA

Spread the loveRais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu amehutubia...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

7 wafa Ulanga, mbunge alia kutelekezwa na mawaziri, Tanroad

Spread the loveWatoto saba wamepoteza maisha na zaidi ya kaya 70 kukosa...

Habari za SiasaTangulizi

Wizara Katiba na Sheria yaliomba Bunge Sh. 441.2 bilioni

Spread the love  WIZARA ya Katiba na Sheria imeliomba Bunge liidhinishe bajeti...

error: Content is protected !!