CHAMA cha NCCR-Mageuzi nchini Tanzania, kimetangaza kutoyatambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020 kwa madai miongozo mwa kanuni za uchaguzi huo zilikiukwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Msimamo huo umetolewa leo Jumanne tarehe 3 Novemba 2020 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma wa NCCR Mageuzi, Edward Simbeye kwa niaba ya mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.
“Uchaguzi ni mchakato, kanuni na miongozo ya uchaguzi vyote hivi vimekiukwa na vinapelekea matokeo kutokuwa halali ya kinachoitwa uchaguzi. Kwa sasa ni sawa na hakuna aliyeshinda wala aliyeshindwa,” amesema Sembeye.
Akizungumzia ukiukwaji wa baadhi ya kanuni na miongozo uliojitokeza katika uchaguzi huo, Sembeye amesema, kuna baadhi ya maeneo mawakala wa NCCR-Mageuzi walizuiwa kuingia katika vituo ya kupigia kura.
“Ukienda Vunjo, robo tatu ya mawakala hawakuruhusiwa kuingia kwenye vituo.
Mimi na wewe tujiulize kama Mbatia anayesema Tanzania kuhusu muungano na ushirikiano anafanyiwa figisu vipi kwa mtu ambaye hana jina,” amehoji Sembeye.
“Ukienda kituo cha Kawe, mgombea wetu wa ubunge hata kura yake ya majumuisho haipo kuna sifuri. Ukiangalia uchaguzi ni mchakato kwa kuwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho ulikuwa wa makandokando na kusababisha matokeo yake ya uchaguzi kutokuwa halali,” amesema Sembeye.
Kufuatia dosari hizo, NCCR-Mageuzi kimeomba meza ya majadiliano ili kupata muafaka wa sintofahamu ya matokeo ya uchaguzi huo kwa lengo la kurudisha imani ya Watanzania na Taifa lao.
“Nchi inakwenda kupasuka. Turudini kwenye meza ya majadiliano NCCR tuko tayari kupata mufaka wa kitaifa. Miaka yote tukekuwa mstari wa mbele kutangaza amani na kuunganisha nchi, bado tuna nafasi ya kurudisha imani ya Watanzania na nchi yao hasa katika kipindi kilichopo, chuki imepitiliza tunahitaji muafaka wa kitaifa,” amesema Sembeye.
NCCR-Mageuzi kimekuwa chama cha nne kutangaza kupinga matokeo hayo kikitanguliwa na vyama vya Chadema, CUF na ACT-Wazalendo.
Katika uchaguzi huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejizolea viti vingine vya ubunge, udiwani na kuendelea kushinda urais ambapo mgombea wake, Dk. John Pombe Magufuli aliibuka mshindi akiwashinda wenzake 15.
Kufanya maridhiano na mwizi ni kazi pevu