Tuesday , 7 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Njaa yatisha, Watanzania waingia Kenya
Habari Mchanganyiko

Njaa yatisha, Watanzania waingia Kenya

Daniel Chongolo, Mkuu wa Wilaya ya Longido
Spread the love

HALI ya njaa inayoelezwa kuwepo hapa nchini kwa sasa inadaiwa kusababisha baadhi ya Watanzania kuvuka mpaka na kuingia nchini Kenya kusaka chakula, anaandika Charles William.

Taarifa kutoka Wilaya ya Longido mkoani Arusha zinaeleza kuwa, wafugaji katika eneo hilo kwa sasa wanalazimika kwenda Kenya kutafuta malisho ya mifugo yao huku pia upatikanaji wa chakula kwa wananchi ikiwa ni shida.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu, Lepilall Ole Moloymet, Luteni Mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), mkazi wa Longido ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo amedai kuwa hali yao ya chakula ni mbaya kufuatia njaa iliyosababishwa na ukame.

“Tuna hali mbaya sana huku, Serikali imetutelekeza, hatuna Mbunge kwasababu aliyekuwepo wamemvua ubunge na matatizo tuliyonayo hakuna wa kuyasemea. Wananchi tunahangaika, mifugo inakufa hovyo na tumeamua kuihamishia Kenya,” amesema.

Luteni Ole Moloymet ambaye ni mkazi katika kijiji cha Isinya wilayani Longido amesema ukame umesababisha mifugo ya wananchi kufa kwa kukosa malisho na hivyo kulazimika kuvuka mpaka na kuingia nchini Kenya ili kunusuru mifugo hiyo.

“Hakuna mvua. Wafugaji tunahangaika tumehamisha mifugo karibu asilimia 80 kwenda nchi jirani ya Kenya, tunaomba serikali itusaidie kwani hata upatikanaji wa chakula kwa wananchi wa wilaya hii ni mgumu sana,” amesema.

Hata hivyo, Daniel Chongolo Mkuu wa Wilaya ya Longido alipotafutwa na mtandao huu kuhusu suala hilo, amesema Serikali inachukua hatua madhubuti ili kushughulikia tatizo la ukame wilayani Longido.

“Wananchi wa wilaya hii kwenda nchini Kenya mara kwa mara si ajabu kwani wanaishi eneo linalopakana na nchi hiyo ingawa ni kweli kumekuwa na ukame. Awamu hii mvua haijanyesha kwa wingi wilayani hapa na hata maeneo mengine ya nchi tofauti na miaka iliyopita.

Suala lingine ni kuwa, mifugo imekuwa mingi kuliko ukubwa wa eneo la wilaya hii kwahiyo lazima pawe na uhaba wa malisho. Hata hivyo, sisi kama serikali tupo katika mpango wa kutafuta mbegu za kuotesha majani ili tuzimwage katika maeneo mbalimbali kwasababu kwa sasa majani hayaoti yakatoa mbegu, yakiota tu mifugo inayala yote,” amesema Chongolo.

Kuhusu uhaba wa chakula kwa wananchi, Chongolo amesema kwamba asilimia 90 ya wananchi wa Longido ni wafugaji na wanategemea chakula kutoka nje ya wilaya hiyo, hivyo wananchi ni kawaida wananchi hao kuuza mifugo ili waweze kununua chakula.

“Ni asilimia tano tu ya wananchi wa Longido ndiyo wakulima. Asilimia 90 ni wafugaji na wanategemea chakula kutoka nje ya wilaya. Ni sawa na maeneo ya wakulima, kwa mfano Njombe ukitaka kupata nyama lazima uuze mahindi ukanunue nyama,” amesema.

Chongolo ameeleza kuwa kuna tatizo la wafugaji kutonunua chakula cha akiba wakati ambao magunia ya mahindi yanakuwa yanapatikana kwa bei rahisi na hivyo kujikuta katika wakati mgumu wakati ambao bei ya mahindi inakuwa imepanda.

“Tatizo linakuja pale chakula kinachosafirishwa kutoka wilaya zingine kuja hapa kinapopanda bei, ndiyo maana tupo kwenye mchakato wa kutengeneza sheria ndogo (by laws) kupitia Halmashauri ya Longido itakayolazimisha wananchi wa jamii ya wafugaji kuwa na akiba ya chakula ambacho watanunua wakati wa mavuno,” amesisitiza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

Habari Mchanganyiko

Mahakama yatoa uamuzi zuio dhidi ya Club House

Spread the loveMAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu jijini Dar es Salaam,...

Habari Mchanganyiko

GGML, OSHA yawanoa bodaboda 200 Arusha

Spread the loveZAIDI ya madereva bodaboda 200 wa jiji la Arusha wamepatiwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Serikali kuwakopesha wajasiriamali 18.5bn/- kupitia NMB

Spread the loveSerikali imetenga kiasi cha Sh 18.5 bilioni kwa ajili ya...

error: Content is protected !!