Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Rekodi ya watalii kuandikwa Desemba 2023
Makala & Uchambuzi

Rekodi ya watalii kuandikwa Desemba 2023

Spread the love

 

WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema ifikapo Desemba 2023 watakuwa wamefikia malengo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya kupokea watalii milioni 5, huku kwenye mapato wakiomba muda kidogo. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea). 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Hassan Abasi wakati akijibu swali la mwandishi wa habari hii kuhusu uwezekano wa kufanikisha lengo hilo lilotolewa ndani ya Ilani ya CCM 2020/2025.

Alisema kwa miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan idadi ya watalii wa ndani na nje wamekuwa wakiongezeka, hivyo matumaini yao ni ifikapo Desemba 2023 takwimu za watalii milioni 5 watakuwa wamefikia.

Dk. Abasi alisema katika eneo la ukusanyaji wa mapato Dola za Marekani bilioni 6 ifikapo 2025 wanatarajia kufikia ila sio katika kipindi cha Desemba 2023.

“Nitoe taarifa kuwa tulipewa lengo na Ilani ya CCM kuhakikisha kufikisha watalii milioni 5 ifikapo 2025, ila tunapoona sasa ifikapo Desemba 2023 tutakuwa tumefikisha watalii milioni 5, hiyo ikiwa ni miaka miwili kabla ya lengo, ni matumaini yangu na upande wa mapato tutafikia pia, tupewe muda kidogo,” alisema.

Katibu Mkuu huyo alisema kwa uchunguzi wao, kasi hiyo imechangiwa na Filamu ya Royal Tour ambayo imemuhusisha Rais Samia Suluhu Hassan na wadau wengine wa sekta hiyo.

Alisema baada ya Royal Tour kuzinduliwa watalii wa ndani walikuwa milioni 2.3 na wakutoka nje milioni 1.4, hivyo kufikia watalii milioni 3.7, hali ambayo imebakiza watalii milioni 1.3 kufikia milioni 5.

“Takwimu za watalii wa ndani na nje ya nchi hadi sasa tumevunja rekodi ambayo haijawahi kufikiwa katika kipindi cha nusu mwaka kuanzia Januari 2023 hadi Juni. Lakini pia hata mapato ya sekta ya yamevunja rekodi kwani tumekusanya Dola za Marekani bilioni 2.8 ambayo haijawahi kufikiwa kwa kipindi hicho,” alisema.

Alisema wizara kwa sasa inachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni na pato la taifa asilimia 21 na kwamba jitihada zao ni mchango huo kuongezeka miaka michache ijayo.

Dk Abasi alisema kwa hali ilivyo sasa katika maeneo ya vivutio vya utalii na mahoteli kuna wageni wengi ambao hawajawahi kutokea na kwamba ifikapo Desemba 2023 watamkabidhi Rais Samia taarifa rasmi ya watalii milioni 5, huku akisisitiza upande wa fedha wapewe muda kidogo.

Katibu mkuu alisema changamoto katika sekta hiyo ilikuwa ni kuitangaza, ila kwa sasa wamefanikiwa kutumia Royal Tour, hali ambayo imechangia zaidi ya watu bilioni moja kufuatilia vuvutio vya utalii.

Aidha, alisema katika kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa kwa kasi wanatarajia kuzungumza na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ili kuwepo kwa Zoo muda wote katika eneo hilo.

“Tunataka sekta hii iwe ya kwanza katika kuchangia pato la taifa, hivyo TanTrade wakiweka mazingira rafiki ya uwepo wa Zoo hapa sabasaba tunaamini watalii wataongezeka hasa wazawa,” alisema.

Dk Abasi alisema mkakati mwingine ambao wanatarajia kuutumia kuhamasisha utalii nchini ni kupitia utalii wa nyuki, ambapo watalii wanaweza kwenda kung’atwa na nyuki au kutumia vumbi.

Katibu Mkuu huyo alisema eneo lingine ambalo wanatilia mkazo ni idara ya mali kali ambayo ina historia ya muda mrefu ikiwemo kuboresha Karavan Sirai, Tendaguru na kwingine.

Dk Abasi alisema katika kuhakikisha wanaweza kupokea wageni wengi kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na wadau mbalimbali kushiriki ujenzi wa hoteli za kitalii ambapo mwezi wa saba watazindua mkakati wa kuonesha maeneo yote ambayo yana fursa ya ujenzi wa mahoteli ya kisasa.

Halikadhalika Dk Abasi alisema Oktoba mwaka huu wataandaa kongamano ambalo litahusisha wadau mbalimbali wa ndani na nje kutambua fursa zilizopo katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Sisi tunataka sekta hii ya utalii kuwa fursa kwa kila mwananchi, kwani tunaamini kila kitu ni kivutio cha utalii, tutashirikiana na kila mdau kufikia malengo,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Usiyoyajua ziara ya Rais Samia Korea Kusini

Spread the loveMWEI 31 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Local content’ inavyotajirisha Watanzania, wavuna mabilioni

Spread the loveUshirikishwaji wa Watanzania katika shughuli za madini (Local Content) na...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

GGML inavyotumia teknolojia kuigeuza Geita kuwa ya kijani

Spread the loveSHUGHULI za uchimbaji madini hutakiwa kwenda sambamba na urejeshaji mazingira...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Rais wangu mama Samia; Wananchi wa Igoma watendewe haki

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wananchi wa eneo la Igoma Truck...

error: Content is protected !!