MOTO uliozuka usiku wa manane katika gereza lenye msongamano mkubwa wa wafungwa huko Jakarta, nchini Indonesia umesababisha vifo vya watu 41 na wengine kadhaa wamejeruhiwa. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi nchini humo imesema moto huo ulizuka mapema leo asubuhi tarehe 8 Septemba, katika gereza la Tangerang lililopo magharibi mwa mji mkuu wa Indonesia.
Mkuu wa Polisi wa Jakarta, Fadil Imran amewaambia waandishi wa habari moto huo umetokea upande wa Block C ambapo ndipo moto ulipozuka kulikuwa na jumla ya wafungwa 122 ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi zinazohusiana na madawa ya kulevya.
“Wafungwa 41 wamefariki dunia, wanane wamejeruhiwa vibaya na 72 wana majeraha madogo,”
Picha za televisheni zimeonyesha maofisa wa idara ya Zima moto wamekabiliana na moto ulioteketeza moja ya majengo ya gereza, ukitoa wingu zito la moshi.
Maofisa wa zima moto wamedhibiti moto huo ambao uliathiri moja ya majengo ya jela hilo, wanakozuiliwa hasa wafungwa waliohukumiwa kwa biashara au utumiaji wa dawa za kulevya.
Mamlaka bado wanachunguza sababu za moto, lakini wengi wamebaini kwamba moto huo ulisababishwa na hitilafu zinazotokana na mifumo duni ya umeme.
Leave a comment