Thursday , 2 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mbowe, wenzake wapangiwa Jaji mwingine, kesi kuanza…
Habari za SiasaTangulizi

Mbowe, wenzake wapangiwa Jaji mwingine, kesi kuanza…

Spread the love

 

KESI ya jinai inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani bchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, sasa itaanza kusikilizwa tena Ijumaa wiki hii, tarehe 10 Septemba, 2021 katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam zinasema, usikilizaji wa kesi hiyo unatarajiwa kuanza tena Ijumaa, baada ya kupatikana kwa jaji mpya wa kuisikiliza.

“Kesi inakuja Ijumaa wiki hii na itasikilizwa na Jaji Mustapha Siyani,” kimeeleza chanzo cha taarifa cha MwanaHALISI Online, kutoka mahakamani hapo.

Jaji Siyani ambaye amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, amepangiwa kusikiliza shauri hilo, baada ya watuhumiwa kumtaka Jaji Elizana Luvanda, kujiondoa kwenye usikilizaji wa kesi yao.

Mbowe na wenzake watatu – Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya, wanashitakiwa kwa makosa sita, likiwamo kupanga njama na kufadhili ugaidi, jambo linalodaiwa na upande wa utetezi, kwamba hati ya mashitaka imepoteza sifa ya kusimamisha kesi hiyo.

Miongoni mwa madai ambayo watuhumiwa wanaelezwa kutaka kufanya, ni pamoja na kutaka kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ambayo imekuwa ikiwashirikisha watu wengi na kudhuru viongozi wa serikali.

Mmoja wa wanaotajwa kutaka kudhuliwa na Mbowe na wenzake, ni aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya. Kwa sasa, Sabaya yuko gerezani jijini Arusha, anakoshikiliwa kwa madai ya wizi wa kutumia silaha na matumizi mabaya ya madaraka.

Kwa mujibu wa Jamhuri, matendo yanayodaiwa kupangwa kutekelezwa na Mbowe na wenzake, yalilenga kusababisha taharuki katika jamii.

“Summons (hati za wito wa kufika mahakamani), zimepangwa kusambazwa kesho Alhamisi asubuhi,” alieleza afisa huyo wa Mahakama na kuongeza, “tayari uongozi wa Magereza umeshaarifiwa ili kuwandaa washitakiwa.”

Katika shauri hili, Mbowe na wenzake, wanatetewa na jopo la mawakili takribani 15, wakiongozwa na Peter Kibatala, Jeremiah Mtobyesa, Fredrick Kihwelo, John Mallya na Boniface Mwambukusi,

Kabla ya Jaji Luvanda kufanya maamuzi ya kujitoa, Mbowe alieleza asivyofurahishwa na mwenendo wake, hasa baada ya kushindwa kufanya maamuzi ya dosari za kisheria, ikiwamo “kutotolea uamuzi pingamizi moja kati ya matatu,” yaliyowasilishwa na mawakili wake.

Mawakili wa utetezi – Kibatala na Mtobesya – waliileza mahakama kuwa wateja wamesomewa hati ya mashtaka kwenye madai batili, kutokana na kuwapo kwa mapungufu ya kisheria.

Mapingamizi hayo, ni makosa kujirudia katika hati ya mashtaka; hati hiyo kutoeleza nia ya washtakiwa kutenda kosa na sheria iliyotumika kuwashtaki Mbowe na wenzake, kutotafsiri makosa ya ugaidi.

Akitoa uamuzi wa mapingamizi hayo, Jumatatu, tarehe 6 Septemba,2021 Jaji Luvanda, alishindwa kutoa uamuzi dhidi ya pingamizi la sheria ya ugaidi, kwa maelezo kuwa anahitaji kusoma kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard).

Freeman Mbowe akiwasili mahakamani Kisutu

Alisema, ni kupitia Hansard ndipo Mahakama yake, yaweza kutambua madhumuni ya sheria hiyo, wakati wa mjadala wa wabunge bungeni.

Alisema, “majibu yanaweza kupatikana katika Hansard ya Bunge ya michango ya wabunge, kuhusu muswada wa sheria hiyo. Kama nilivyosema, jambo hili linachukua muda. Kimsingi sitapenda kuhitimisha katika hatua ya awali.

“Badala yake, nitaliacha uwazi kwa pande zote kutoa ufafanuzi hapo baadae. Hivyo hoja hiyo naiachia hapa.”

Awali, mawakili wa utetezi waliomba mahakama hiyo iwafutie mashtaka wateja wao, wakidai hakuna kosa la msingi baada ya sheria hiyo kushindwa kutafsiri makosa ya ugaidi, kama ambavyo sheria nyingine zinazofanya.

Hata hivyo, Jaji Luvanda alipinga hoja hiyo akisema, kila nchi inatengeneza sheria zake kulingana na mazingira yake.

Alisema, “marejeo yanatakiwa yafanyike kupitia maazimio ya Bunge ya kutunga sheria ya ugaidi, kuona kwa nini walizuia kuweka tafsiri ya vitendo vya kigaidi kwa kuunganisha siasa, dini na itikadi.

“Ninahisi Bunge lilitafakari na kuangalia mazingira ya jamii zetu, dhidi ya miongozo iliyotolewa ili kuzuia haki kutotendeka,” alieleza Jaji Luvanda.

Jaji Luvanda alisisitiza ni maoni yake, kwamba Bunge halikuchagua kufuata mrengo wa mataifa mengine, kutafsiri matendo ya ugaidi bila kuhusisha siasa, dini na itikadi.

Aliongeza, “kwa maneno mengine haitoshi kusema sisi mfumo wetu wa kisheria unafafanana na nchi tatu ili tuwe sawa.”

Mbali na kuliweka kiporo pingamizi hilo, Jaji Luvanda alitupilia mbali mapingamizi mengine na kuuelekeza upande wa mashtaka kuifanyia marekebisho hati ya mashtaka katika maelezo ya shtaka la kwanza, nne na la sita.

“….nakubaliana na hoja (pingamizi) ya kwanza kuhusu changamoto ya kosa la kwanza, nne na la sita, kwamba makosa yaliyofunguliwa chini ya Kifungu cha nne, waendesha mashtaka kutotumia baadhi ya maneno,” alisema Jaji huyo na kuongeza:

“….nakubaliana na Kibatala hayo maneno yangewekwa ili kuweka mpaka kati ya shauri la ugaidi na makosa ya jinai. Nawaelekeza upande wa Jamhuri ufanye mabadiliko katika kosa la kwanza, nne na sita,” ili kuyatenganisha.

Mara baada ya Jaji Luvanda kutoa maamuzi hayo, Kibatala aliieleza mahakama kuwa wateja wake, wanataka kuzungumza na mahakama.

Ndipo Mbowe kwa niaba ya wenzake, akawasilisha maombi ya mdomo ya kutaka ajitoe ili kuhakikisha kuonekana haki inatendeka.

Mbowe alisema, kesi hiyo imeleta hisia kali kwa jamii na inaweza kuthibistishwa na mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii.

Alisema, mijadala hiyo haiwezi kupuuzwa ikiwemo taarifa zinazosema, “Jaji Luvanda ni Mserikali na TISS (Usalama wa Taifa) na kwamba yupo katika Mahakama ya mafisadi kimkakati. Ameelekezwa kumfunga Mbowe huku msajili akishughulika na Chadema.”

Mbowe aliendelea kunukuu andishi hilo alilodai limesambaaa kwenye mitandao ya kijamii, kwamba “Rais atamuachia baada ya muda. Kila pingamizi atalitupilia mbali haijalishi uhalali wake.

“Naomba niishie hapo katika kunukuu. Jaji haya maneno au hisia za jamii, hatuwezi kupuuza; ni ombi langu ikupendeze kujitoa katika shauri hili, ili kujenga heshima yako na Mahakama, ili usibebeshewe lawama ambayo si sahihi.”

Akitoa maoni yake baada ya hukumu hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, alieleza kuwa Mbowe na wenzake, walistahili kuachiwa huru baada ya hati iliyotumika kuwafungulia mashtaka ya ugaidi, kubainika kuwa na kasoro.

Alisema, Mbowe na wenzake walipaswa kuachwa huru ili Serikali ijipange kurekebisha mashtaka hayo.

Askofu Benson Kagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe

Akiandika kupitia mitandao ya kijamii, Askofu Dk. Bagonza alisema, “serikali ndivyo ilivyoshtaki, Jaji kakubali mashtaka ya serikali yana kasoro. Anaelekeza namna nzuri ya serikali kumshtaki Mbowe. Jaji alipaswa kumwachia Mbowe ili serikali ijipange tena kuleta mashtaka sahihi.

“Mbowe hashtakiwi na Jaji. Anashtakiwa na serikali. Kwa hiyo, si sawa Jaji kuendelea ikiwa anaona Mbowe hana mashtaka sahihi.”

Katika kesi hiyo, shtaka la kwanza, ni la kula njama za kutenda vitendo vya ugaidi, linalowakabili washtakiwa wote. Wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya tarehe 1 Mei hadi 5 Agosti 2020, katika maeneo mbalimbali mkoani Arusha, Morogoro na Dar es Salaam.

Shtaka la nne, ni la kushiriki vikao vya kutenda kosa la ugaidi, linalowakabili wote, wanalodaiwa kulitenda kati ya tarehe 1 Mei hadi 5 Agosti 2020, kwenye hoteli ya Aishi mkoani Kilimanjaro.

Katika shitala la sita, linahusu umiliki wa mali, ambapo linamhusu Bwire, ambaye anatajwa kuwa alikuwa afisa wa jeshi.

Akisoma uamuzi wa kujitoa kwenye kesi hiyo, Jaji Luvanda alisema, “nimekubaliana na maombi ya washitakiwa. Ninajitoa.”

Alisema, “nimesikia hoja za pande zote mbili, niseme msingi wake ni suala la dhana kuliko uhalisia ulivyo. Sina sababu ya kujitetea na siwezi kujitetea katika jambo ambalo kimsingi halipo.

“Kwa kuzingatia kwamba shauri lina maslahi kwa umma, ninajitoa na kuliacha shauri hilo kwa Jaji mwingine kuendelea nalo. Nichukue nafasi hii kuwashukuru wote na kuwatakia.”

Baada ya Jaji Luvanda kumaliza kusoma uamuzi huo, mamia ya wafuasi wa Chadema na mwenyekiti wao Mbowe, walionekana kujawa na furaha. Haikuweza kujulikana mara moja, kipi ambacho kimewafurahisha. Yawezekana ni hatua ya Jaji kuamua kujitoa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kamati ya Bunge yaitaka Serikali ichukue hatua kudhibiti mfumuko wa bei

Spread the love  SERIKALI ya Tanzania imetakiwa kufanya tathimini dhidi ya changamoto...

Habari za Siasa

Bunge lataja kinachokwamisha Mradi wa Mchuchuma na Liganga

Spread the love  MRADI wa uchimbaji chuma cha Liganga na Makaa ya...

Habari za Siasa

Chongolo aagiza watendaji wanaoonyesha mianya ya rushwa wakamatwe

Spread the love   KATIBU mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa...

Habari za Siasa

TRA iweke mfumo wa msamaha wa kodi kutekeleza miradi

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kimeitaka Mamlaka ya Mapato...

error: Content is protected !!