PERVES Musharraf, aliyekuwa Rais wa Pakistan (76) amehukumiwa adhabu ya kifo, baada ya kukutwa na hatia ya kosa la uhaini. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Hukumu hiyo imetolewa leo tarehe 16 Desemba 2019, na Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Juu ya Pakistan, huku rais huyo mstaafu akiwa hayupo mahakamani hapo.
Jopo hilo la majaji watatu lilimkuta Musharraf na hatia, kwenye kosa la uhaini pamoja na kuvunja katiba ya nchi hiyo, akiwa madarakani.
Mahakama hiyo imeamuru Musharraf anayeishi uhamishoni, Dubai katika Nchi za Falme za Kiarabu, akamatwe, kama atagoma kurudi nchini Pakistan.
Musharraf amekutwa na hatia kwa kosa la kusitisha matumizi ya katiba ya Pakistan na kuanzisha sheria ya dharula, mwaka 2007.
Makosa mengine yaliyokuwa yana mkabili Musharraf, ni mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Benazir Bhutto, aliyeuawa mwaka 2007 katika shambulio la kujitoa mhanga na mauaji ya halaiki ya watu.
Musharraf kwa mara ya kwanza alifikishwa kortini kwa tuhuma za uhaini, mwezi Desemba mwaka 2013, na kushtakiwa rasmi tarehe 31 Machi 2014.
Musharraf aliingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1999, ambapo alitawala kwa miaka 9, baada ya kujiuzulu urais wa Pakistan mwaka 2008, akikwepa kufunguliwa kesi kuhusu tuhuma zilizokuwa zinamkabili.
Leave a comment