Monday , 22 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Ya TANU, Afro Shirazi sio ya CCM
Makala & UchambuziTangulizi

Ya TANU, Afro Shirazi sio ya CCM

Spread the love

UBINAFSISHAJI ni sera ya Benki ya dunia, ulioanza kutekelezwa toka awamu ya pili ya utawala wetu ikiwa ni kipindi cha mpito cha kuondokana na uchumi wa dola. Anaandika Mbonea Mkasimongwa … (endelea).

Lengo ilikuwa uchumi wetu kuuweka kwenye mikono ya watu binafsi wa mataifa mbalimbali wenye uwezo mkubwa wa mitaji na teknolojia za kisasa.

Mfumo huu wa umilikaji mali ndio uliokuwepo wakati wa ukoloni wa Kiingereza hadi na mwaka 1967.

Ujio wa Azimio la Arusha ulikwenda sambamba na zoezi la utaifishaji wa njia kuu za  uchumi zilizokuwa chini ya watu binafsi kuwekwa mikononi mwa serikali kwa niaba ya umma.

Uwekezaji ni sera ya TANU ya mwaka 1962 iliyokwenda sambamba na huo mfumo wa umilikaji mali wa watu binafsi.

Kwani kabla ya Azimio la Arusha, fursa sawa za uwekezaji vitega uchumi zilitolewa kwa wawekezaji wageni (foreign investors) na wawekezaji wa ndani (Local investors).

Miongoni mwa wawekezaji wakubwa wa  ndani enzi hizo walikuwa vyama vya msingi vya ushirika (Primary Societies).

Tunawakumbuka wazee wetu waliokuwa wakulima wa mazao ya pamba, kahawa korosho na tumbaku, walikatwa fedha zao ambazo zilinunua hisa  kwenye vyama vya ushirika.

Licha ya maarifa madogo ya uchumi wa kisasa wakati ule, bado Ushirika wao uliwekeza hisa kwenye vitega uchumi vilivyolenga kuwaletea faida kubwa.

Jengo la makao makuu ya ushirika hapa jijini lililopo kwenye kona ya mitaa ya Lumumba na Kleist Sykes ni miongoni mwa vitega uchumi vikubwa vilivyojengwa kati ya mwaka 1964 hadi 1966.

Kuna majengo mengi ya ushirika kwenye mikoa ya Arusha, Moshi, Mwanza, Shinyanga, Mbeya na Iringa ambayo yaliwekezwa  kwenye maeneo yenye shughuli kubwa za kibiashara.

Pia vyama vya ushirika vingine vilikuwa na mali zisizoondosheka na viwanda kwa ajili ya kusindika mazao.

Kana kwamba haitoshi, wananchi hao katika miaka hiyo hiyo waliweza kutumia hisa zao kuanzisha benki yao iliyokuwa inajulikana kwa jina la Benki ya Taifa ya Ushirika na Maendeleo (National Cooperative and Development Bank) na ilianza kwa mtaji wa Sh. milion 14.

Watanzania wazawa hao waliathirika na zoezi la utafishaji ambapo mwaka 1972 benki hiyo iliyokuwa inaendeshwa vizuri sana, iliathiriwa na sera za taifa ambapo benki zote zilitakiwa kuwa za umma na hivyo kutaifishwa toka wakati huo umebadilishwa majina mbalimbali hadi kuitwa CRDB.

Leo hii wazee wetu wengi ambao ndio wenye hisa kwenye ushirika hawapo duniani, huku vitega uchumi vyao vinavyoendelea hadi leo haijulikani ni nani mmiliki halali.

Warithi wa wazee hao  pia hawakuonekani kunufaika tunachokiona ni sarakasi tu kati serikali, wafilisi na waliobinafsishiwa.

Rais John Magufuli ambaye ana taarifa fika ya kuuzwa kwa ujanja mali za wanaushirika katika sehemu mbalimbali zikiwemo zile za Nyanza Cooperative Society, naye amekumbwa na kigugumizi licha ya siku za awali alipoingia madarakani alionesha nia ya kuwashughulikia wote waliofisidi.

Yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo na yajayo, hii ni methali inayojaribu kuiasa jamii kuwa si busara kuendelea kukumbusha mambo yaliyopita kwa vile yanaweza kupoteza muda bure.

Taifa halina budi kudurusu  mambo haya ya nyuma ili kufutilia dhana ya ubinafshaji uliodhulumu wavuja jasho. Mpaka sasa waliovuja jasho kuujenga ushirika vizazi vyao bado vinavuja jasho.

Mtunzi mmoja kisiwani Unguja  anapingana na methali hiyo. Yeye anasema “Yaliyopita yamepita ni msemo wa maliwazo tu, yaliyopita katu hayakupita, kila jana inayo athari kubwa juu ya leo, na leo juu ya kesho.” Usemi huu unabashiri historia ina tabia ya kuhukumu na kusuta wenye kuipuuzia.

Baada ya Azimio la Arusha  la 1967 ambapo njia kuu za uchumi ziliwekwa mikononi mwa umma.

Majengo mbalimbali katikati ya Jiji la Dar es Salaam yalitaifishwa ikiwa ni mojawapo kusaidia taifa kujijengea uwezo wa umma kumiliki mali  kupitia Shirika la Nyumba la Taifa na Msajili wa Majumba.

Moja ya mikataba mibovu ambayo imeendelezwa na NHC ni zoezi la ubinafsishaji la kuingia ubia na wafanyabiashara binafsi ili kuyajenga upya majengo yaliyotaifishwa yaliyo katikati ya jiji kwe mtindo wa ubia ambapo wawekezaji binafsi hupewa hisa kubwa kuliko zile za NHC.

NHC kwa niaba ya Watanzania ambao ndio wamiliki wanabaki na asilimia 20, wabia binafsi wao wanachukua asilimia 80.

Hapa kinachofanyika ni kama  kuwanyang’anya miliki ya mali Watanzania na kuzirudisha kinyemela mikononi mwa kikundi cha watu ambao wazazi wao ndio waliotaifishiwa.

Kinachofuatia baada ya mradi kukamilika yule mwenye hisa nyingi anaweza kumlipa mwenye hisa chache na hatimaye jengo likamilikiwa na mtu mmoja.

Hivi ni  kweli Watanzania wanashindwa kuyajenga upya majengo hayo? kuna vyombo vya fedha na taasisi za umma ambazo zina fedha lukuki.

Mashirika ya mifuko ya jamii yameonesha njia kwa kujenga vitegauchumi katika maeneo hayo ambayo yanalipa.

NHC tulitegemea kuingia ubia na mifuko hiyo ya jamii au mabenki na hata Soko la Hisa kwa kujenga upya na kuyakarabati majengo yaliyopo kwenye maeneo yenye vivutio vya biashara.

Baya zaidi hata miradi mipya iliyobuniwa na NHC imechota mamilioni ya fedha kwenye mabenki na kujenga majumba ambayo ni miradi ya tembo mweupe kwa Watanzania wenye kipato cha chini.

Tunashuhudia wahusika wakisitishiwa ajira zao kama ndio hasira kwa serikali kwa ubadhirifu huu.

Wananchi wanashuhudia CCM ambayo iliahidi kuendeleza mema ya TANU na AFRO SHIRAZI nao wanaonekana kubariki ubinafsishaji huu holela.

Bila aibu wameuziana mali za chama na kuridhia jumuia zao ya vijana (UVCCM) na wanawake  kuingia ubia  kwa mtindo kama huo wa NHC.

Ubinafsishaji  ni sera zilizo kinyume na ile zilizorithiwa na CCM kutoka vyama mama vya TANU na ASP. 

Utaifishaji ulikuwa sera iliyotawala mnyumbuliko wa kiuchumi zama hizo, ikiwa mfumo huo haifai basi ni vyema serikali itamke hadharani  mali zote zilizotaifishwa zinarudishwa.

Wananchi na wanachama wa CCM wa kawaida toka ubinafsishwaji uanzwe kutekelezwa hapa nchini, wamekuwa wakiwalalamikia viongozi wao kwamba zoezi hilo haliwanufaishi wananchi wazawa bali limelenga kuwanufaisha wageni na viongozi wao chini ya mazingira ya rushwa.

Licha ya malalamiko hayo toka kwa wafanyakazi, wakulima na wananchi wengine katika sekta isiyo rasmi ambao wengi wamepoteza ajira, haki na milki zao kutokana na ubinafsishaji usiopangiliwa hawajalipwa fidia zozote hadi leo, lakini wanaona wafanyi biashara wanarejeshewa mali zao kijanja.

Deni lingine kwa Rais Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano kwa Watanzania ni kule kuonekana ni mfuasi wa sera za umma kwa vitendo zinazowakumbatia wanachama wanyonge na maslahi yao kama alivyokuwa Mwalimu Julius Nyerere. 

Vinginevyo Watanzania watamhukumu yeye na wasaidizi wake kuwa ni mawakala na madalali wa sera zinazoendelea kuwanyanga’anya Watanzania umiliki wa taifa lao wa njia kuu za uchumi na raslimali zao chini  na kuendeleza ubinafsishaji usiopangika vizuri ili kujenga ubepari uchwara.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

error: Content is protected !!