May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wenyeviti wa Bunge Tanzania, giza nene

Bunge la Tanzania

Spread the love

 

LICHA ya Kanuni za Bunge la Tanzania, kutaka kuwepo kwa Wenyeviti wa Bunge, mpaka sasa wenyeviti hao hawapo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Uchunguzi uliofanywa na MwanaHALISI Online kuhusu utaratibu wa kupatikana kwa wenyeviti wa Bunge, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, toleo la Juni 2020, umebaini kutokuwepo kwa wenyeviti hao mpaka sasa ikiwa ni kinyume na taaribu.

Kanuni za Bunge ya saba kinaelekeza, “kutakuwa na wenyeviti watatu wa Bunge ambao wataongoza vikao vya Bunge kwa utaratibu na maelekezo ya Spika au Naibu Spika kwa mujibu wa Kanuni.”

Kanuni ya 13, inaelekeza jinsi watakavyopatikana ambapo kifungu cha (1) kinaeleza “wenyeviti wa Bunge, waliotajwa katika kanuni ya saba watachaguliwa na wabunge kutoka miongoni mwa wenyeviti na makamu wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge.”

Kifungu cha (2) (a) kinaelezea, nyakati ambazo uchaguzi utafanyika ni “katika mkutano wa Bunge utakaofanyika baada ya Kamati za Bunge kuundwa au mapema zaidi baada ya wakati huo”

Steven Kigaigai, Katibu wa Bunge

Kifungu (b) kinasema “baada ya Kiti cha Mwenyekiti wa Bunge kuwa wazi kwa sababu yoyote isiyohusiana na Bunge kuvunjwa.”

Hata hivyo, tangu kuzinduliwa kwa Bunge hilo, tarehe 13 Novemba 2020 na Hayati Rais John Pombe Magufuli, huu ni mkutano wa tatu, unaoendelea na uchaguzi haujafanyika.

Mkutano wa pili wa Bunge, uliofanyika Februari 2021, ndio ambao kamati za Bunge ziliundwa na kila kamati, zina wenyeviti na makamu wenyeviti.

Hadi leo Alhamisi, ni kikao cha 24, mkutano wa tatu unaendelea jijini Dodoma, ambapo umekuwa ukiongozwa na Spika Job Ndugai au naibu wake Dk. Tulia Ackson.

MwanaHALISI Online, lilimtafuta Spika Ndugai, ili kujua sababu za kutokuwepo kwa Wenyeviti wa Bunge mpaka sasa, simu yake iliita bila kupokewa.

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Pia, mtandao huu ulimtafuta, Stephen Kagaigai, Katibu wa Bunge ili kupata ufafanuzi zaidi, naye hakupatikana.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa bunge ambaye ameomba kuhifadhiwa jina lake amesema, tarehe ya uchaguzi wa wenyeviti wa bunge na wawakilishi wengine, itatangazwa wiki ijayo.

Mbali na uchaguzi wa wenyeviti wa bunge, afisa huyo amesema, pia watachaguliwa wawakilishi wa Bunge la Umoja wa Afrika (PAP) na wa Jukwaa la Kibunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Mchakato haujachelewa, tunategemea Jumatatu ya wiki ijayo itatangazwa tarehe ya uchaguzi huo. Pia kuna chaguzi nyingi hazijafanyika ikiwemo wawakilishi wa PAP na SADC,” amesema ofisa huyo.

error: Content is protected !!