May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Majaliwa aitaka TPA kuongeza umakini

Bandari Dar es Salaam Tanzania

Spread the love

 

KASIMU Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania, ameiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kuimarisha usimamizi wa mitambo ya mita za upimaji wa mafuta ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, serikali inataka kuona makusanyo yote ya mapato kutoka katika bandari zote nchini, yanayokusanywa na TPA yanaingia katika mfuko mkuu wa Serikali.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano tarehe 3 Machi 2021, baada ya kukagua mitambo ya mita ya mafuta Kigamboni na Kurasini (KOJ) kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Pia amesema, ameridhishwa na utekelezwaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali aliyoyatoa katika vipindi tofauti kuanzia mwaka 2016, alipofanya ziara katika eneo la mitambo ya mita ya mafuta Kigamboni na KOJ.

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu,

”Leo nimekuja kuona hatua sahihi tuliyofikia na nimeridhishwa na utekelezaji wake,” amesema Waziri Majaliwa na kuongeza:

”Nimefurahi kupata taarifa kwamba viwanja vimenunuliwa na sasa zabuni ya ujenzi wa matenki mapya inafanywa, tukishafika hapo, Taifa litanufaika sana kuwa na mafuta mengi yaliyopo kwenye akiba yetu.

“Pia hata wateja wanaotaka mafuta watakuwa wanaagiza wakati wowote kulingana na mauzo waliyoyafanya na kiwango wanachokihitaji kwa wakati huo,” amesema.

Mhandisi wa Idara ya Mafuta wa TPA, Yona Malago alimueleza Waziri Majaliwa hatua zilizochukuliwa na TPA ili kuhakikisha ufanisi wa kushusha mafuta kupitia mita ya Kigamboni unafikiwa.

”Hatua ya awali ni ile iliyowezesha mita kufanyakazi bila kusimama, na hatua ya pili ni kufanya ukarabati mkubwa wa mita ikiwemo kurekebisha machujio,” amesema.

error: Content is protected !!